Advertisements

Friday, August 1, 2014

Stars yakwepa hujuma Msumbiji

Wachezaji wa Taifa Stars wakiwa mazoezini jana asubuhi katika viwanja vya Bedford Country Club Jijini Johannesburg wakati maandalizi ya mechi yao ya marudiano dhidi ya Msumbiji mjini Maputo.

Kikosi cha timu ya soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), kinatarajiwa kuwasili leo jioni mjini Maputo tayari kwa mechi yao ya marudiano dhidi ya wenyeji Msumbiji (Mambas) itakayochezwa Jumapili Agosti 3, mwaka huu, huku kikiwa kimejipanga vema kukwepa 'fitna' za ugenini.

Katika kuhakikisha kikosi cha Taifa Stars kinakuwa kwenye mazingira yenye usalama na kuepuka 'hujuma' ya aina yoyote kutoka kwa wenyeji, Shirikisho la Soka nchini (TFF) limetanguliza ujumbe maalumu ili kuweka mipango ya mapokezi vizuri.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya TFF, Wilfred Kidao, alisema Stars itawasili jioni Maputo na kila kitu wamekiandaa wao ili kuhakikisha kikosi kinakuwa kwenye mazingira salama.


Mjumbe huyo alisema wanajua mechi hiyo itakuwa na ushindani mkubwa ndiyo sababu wamejipanga kukabiliana na hali hiyo ndani na nje ya uwanja.

"Kila kitu ni cha kwetu, tumeamua kujipanga wenyewe kwa ajili ya timu yetu, hii ni mechi ya kufa au kupona, " alisema kwa kifupi kiongozi huyo bila kueleza kama wameikataa hoteli waliyoandaliwa na wenyeji wao au la.

Alisema pia hali ya hewa ya Maputo kwa sasa inafanana na ya jijini Dar es Salaam wakati kikosi cha Stars kilikuwa kimeweka kambi Tukuyu mkoani Mbeya kwenye baridi na juzi na jana kilikuwa Johannesburg, Afrika Kusini ambapo kwa sasa hali ya hewa ni nyuzi joto 15.

Stars ikiwa Johannesburg, jana ilifanya mazoezi mara mbili (asubuhi na jioni) kwenye Uwanja wa klabu ya Bedfordview Country na leo itafanya mazoezi ya mwisho asubuhi kabla ya kuondoka jioni.

Pia jana jioni wachezaji wa Stars na timu ya vijana umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) walitarajiwa kukutana na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Razia Msuya.

Mabao yaliyofungwa na kiungo, Khamis Mcha, yaliifanya Stars kumaliza mechi ya kwanza kwa sare ya mabao 2-2, hivyo inahitaji ushindi wa aina yoyote ili iweze kusonga mbele.

Serengeti Boys iko Johannesburg tangu Jumatatu Julai 27, mwaka huu kwa ajili ya kujiandaa na mechi yao dhidi ya yosso wa nchi hiyo (Amajibos) itakayochezwa kesho Agosti 2, mwaka huu mjini Soweto kuwania nafasi ya kushiriki michuano ya Mataifa ya Afrika chini ya miaka 17 itakayofanyika nchini Niger mwakani wakati Stars yenyewe inasaka tiketi ya fainali za Mataifa ya Afrika zikazofanyika Morocco 2015.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: