Arusha. Ni nadra siku hizi kuzungumzia nchi kufilisika kiasi cha kukosa uwezo wa kununua mahitaji yake mbalimbali na kutoa huduma kwa raia wake.
Lakini, kwa upande wake, Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Edwin Mtei anaeleza siri kuwa Tanzania ilifikia hatua hiyo miaka ya mwanzo ya 1980.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwake, Tengeru, nje kidogo ya Arusha hivi karibuni, Mtei alieleza kuwa sababu kubwa ya nchi kufilisika ilitokana na fedha nyingi kutumika kwenye Vita ya Kagera baina ya wanajeshi wa Tanzania na wale wa Uganda, chini ya utawala wa Idd Amin Dadaa.
“Tulipoingia vitani nchi yetu ilikuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, lakini matumizi makubwa yakiwamo ya kununua silaha za kivita na kuwalipa askari yakaiacha hazina yetu ikiwa tupu na kavu.
“Nikiwa BoT, nikaenda nje kusaka misaada na hata mikopo ya kunusuru uchumi wetu ambao ulikuwa umevurugika kwa kiasi kikubwa. Huko nikakutana na masharti magumu,” alieleza Mtei na kutaja sababu za Mwalimu Julius Nyerere kutangaza miezi 18 ya hali ngumu.
Alisema mojawapo ya masharti ambayo yalitolewa wakati ule hasa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na hata Benki ya Dunia (WB) ni kushusha thamani ya Shilingi pamoja na kufanya marekebisho kwenye mashirika mengi ya umma, ambayo yalionekana yakijiendesha vibaya.
Hata hivyo, anaeleza kuwa aliporejea nchini na kumweleza Rais (Mwalimu Nyerere), kiongozi huyo alikataa kata kata masharti hayo ya IMF.
“Nikarudi na mapendekezo, nikamweleza Mwalimu, lakini yeye aliyakataa mapendekezo yote, akanieleza kuwa hayuko tayari kuona thamani ya shilingi ikishuka.
“Mwalimu akiwa kiongozi, mkuu wa nchi, akafikia mahali akanieleza, you’ll devalue our shilling over my dead body. Yaani, kama ni kushusha thamani ya shilingi, mtaishusha mimi nikiwa tayari nimekufa,” alieleza Mtei na kuongeza kuwa siku hiyo Mwalimu Nyerere alionyesha kukasirika.
“Mwalimu alisema yeye hayuko tayari kugeuka jiwe, akaniambia ule mfano wa Ruthu na jinsi aliyevyokiuka amri ya Mwenyezi Mungu, akageuka nyuma akageuka jiwe. Mwalimu akasema yeye hayuko tayari kwa hilo,” alieleza Mtei.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment