Advertisements

Friday, August 1, 2014

KUNA KITU ZAIDI YA NENO NAKUPENDA


JAMBO la kufurahisha ni kwamba, ukifungua ukurasa huu, unakuwa na uhakika wa kuongeza kitu kipya katika maisha yako ya uhusiano na mapenzi. Hata kama huna mpenzi kwa sasa, utajiwekea mazingira mazuri ya kupata mwezi sahihi siku zijazo.

Unaweza kunisoma pia kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko katika safu ya Let’s All About Love, Elimu ya Mapenzi katika Gazeti la Championi Jumamosi na Love & Life kwenye Gazeti la Uwazi kila Jumanne.

Oke! Sasa turudi kwenye mada yetu. Ni somo muhimu sana kufahamu kwa wanandoa na wanaotarajia kuingia kwenye ndoa. Kabla ya kwenda mbali zaidi, hebu tujiulize, unaposema; nakupenda, unamaanisha nini?

Tulia kwa muda, tafakari...mpenzi wako anapokuambia anakupenda, unafikiri nini zaidi kichwani mwako? Marafiki hapo ndipo kwenye msingi mzima wa mada yetu. Wengi huishia kufikiri kirahisirahisi tu, kuwa anampenda fulani au mwezi wake anampenda!

Je, umewahi kujiuliza, unampenda mpenzi wako kwa kiwango gani? Je, yeye anakupenda kwa kiasi gani? Upendo wake unamaanisha nini hasa? Upendo wako kwake una maana gani? Ni pendo la ndani kweli au tamaa za mwili?

Unaweza kujiuliza, inawezekana vipi, ukampenda mtu hadi mkafikia kuingia kwenye ndoa, bado ikawa ni tamaa ya ngono tu? Hapa namaanisha kuwa yawezekana vipi, mpendane halafu muingie ndani maelewano yaondoke?

Heshima itoweke? Upendo utoweke? Inawezakana vipi? Wengi wanajiuliza:
“Tumependana na mume wangu kwa miaka mingi, tumeingia kwenye ndoa na tumeishi humo kwa siku nyingi lakini kwa nini leo hii nimuone amebadilika?”

Wasomaji wengi wananiuliza maswali yanayofanana na hayo (hasa wanawake). Ngoja nikupe kisa cha msomaji mmoja mwanamke, kisha tuingie kwa undani zaidi katika mada yetu.

KUTOKA KWA MSOMAJI:
Mimi nipo kwenye ndoa kwa miaka sita sasa, mimi na mume wangu tumejaliwa kupata watoto wawili – wa kike na wa kiume. Miaka mitatu ya mwanzo tuliishi kwa amani na upendo, nilipojifungua mtoto wa pili ndipo mabadiliko yakaanza.

Nimejikuta sina msisimko kabisa na mume wangu. Yaani nikimwangalia namuona wa kawaida tu, hanishawishi kwa chochote. Tatizo ni nini? Naomba ushauri wako.
Ester R, Arusha.

TUJIFUNZE KUTOKA KWA ESTER
Naamini wanawake wengi wana tatizo kama la Ester. Si wanawake tu, hata wanaume nao wapo ambao hawana mvuto tena kwa wake zao. Wanaona wa kawaida kabisa, hakuna msisimko wala ushawishi.

Wanatazamana kama magogo tu, maana hakuna jambo jipya linaloonekana mbele ya uso wa macho yao. Ni kweli, tatizo hili lipo, tena linatafuna sana ndoa nyingi. Swali la msingi hapa, kama Ester anakiri alimpenda mumewe kwa dhati, wakafunga ndoa, iweje leo abadilike?

Ikiwa Ester alikubali kwa hiyari yake kuunganishwa na mumewe, tena hadi wamefikia hatua wamezaa, mapenzi yamekwenda wapi? Hapo ndipo kwenye somo lenyewe ambalo bila shaka ndiyo itakuwa tiba ya wote wanaosumbuliwa na tatizo hili.

KUPENDA NA KUPENDWA
Kitu cha msingi ambacho unatakiwa kujifunza hapa ni kwamba, pendo la dhati huishi ndani. Penzi huwa haliishi, halina muda maalum wa kuishi ndani ya mtu. Kwa maneno mengine ni kwamba, kama ulimpenda miaka 20 iliyopita kwa dhati ya moyo wako, basi leo huwezi kumchukia.

Upendo ukishaingia ndani ya moyo wa mtu hubaki humo milele, ila kuna mambo madogomadogo au pengine yanaweza kuwa makubwa, yanayoweza kusababisha kuuhairisha upendo kwa muda.

Nasema kuuhairisha kwa sababu hauwezi kuondoka. Rafiki zangu, ujue wazi kuwa, hadi mwenzi wako ameamua kuungana na wewe katika ndoa, si bahati mbaya. Hajabahatisha, bali amekuchagua kutoka kwa wengi.

Kama ndivyo, kwa nini penzi liondoke ghafla? Haiwezekani. Kwa maana hiyo, sasa ni wazi kuwa, penzi huharibiwa na sisi wenyewe. Kuna mambo ambayo yakifanyika hupunguza nguvu ya mapenzi na mwisho wake kusababisha matatizo kama nilivyoeleza hapo juu.
Wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.

GPL

No comments: