ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 4, 2014

Kuzagaa kwa silaha nchini, nani anajali?

Sasa nchi yetu imefika mahali ambapo maisha ya watu, hasa jijini Dar es Salaam yanaonekana kuwa ‘roho mkononi’ kutokana na kukithiri kwa ujambazi na kuzagaa kwa silaha ambazo zimo katika ‘mikono haramu’. Kwa maneno mengine, silaha nyingi hazimo katika ‘mikono stahiki’. 
Umilikaji wa silaha hapa nchini ni wa holela na bahati mbaya ni kwamba hakuna mikakati na mbinu za kuhakikisha wamiliki wa silaha ni wale tu waliohakikiwa na kuonekana siyo hatari kwa usalama wa taifa, maisha ya watu na mali zao.
Tumelazimika kusema hayo kutokana na matukio mengi ya ujambazi ambayo yamekuwa yakitokea katika maeneo mengi nchini. Silaha zimetumika katika matukio mengi ya ujambazi na siyo siri kwamba katika baadhi ya matukio silaha za kijeshi zimetumika.

Hali hiyo imejenga dhana miongoni mwa wananchi kwamba enzi zao za kuishi kwa amani bila kuhofia usalama wao zimekwisha. Sasa ni jambo la kawaida kuona polisi wanakamata watuhumiwa wa ujambazi na wanapowafanyia upekuzi wengi hukutwa na silaha.
Tunasema matukio ya ujambazi wa kutumia silaha ni mengi. Katika tukio la usiku wa kuamkia juzi mkoani Morogoro, majambazi walifunga Barabara ya Morogoro – Iringa katika eneo la Njia Panda ya Kilosa wakateka magari na kupora mali za watu baada ya kurusha risasi.
Tukio hilo lilikuja siku moja baada ya polisi mkoani humo kumtia mbaroni raia wa Burundi akiwa na vifaa vinavyotumika katika utekaji wa magari, ikiwa ni pamoja na mabomu ya milipuko, minyororo yenye misumari na darubini. Ni uthibitisho kwamba maisha ya watu popote walipo siyo salama tena.
Hali ni mbaya zaidi jijini Dar es Salaam, ambako matukio ya ujambazi wa kutumia silaha kwa kutumia pikipiki yamekithiri kiasi cha watu wanaopeleka au kutoa fedha benki na kwingineko kuvamiwa , kujeruhiwa au kuuawa mchana.
Wananchi wamekuwa wakihoji, kwa mfano ni kwa vipi majambazi hao hupata taarifa za mtu aliyebeba fedha, anayekwenda kuweka au kutoa fedha benki na kiasi cha fedha alichonacho.
Mapema mwaka huu, gazeti hili lilichapisha habari ya uchunguzi kuhusu jinsi silaha zinavyoingizwa nchini kinyume na sheria, jinsi zinavyouzwa kiholela mitaani na jinsi baadhi ya watumishi katika Jeshi la Polisi wanavyochangia katika uzagaaji wa silaha nchini.
Uchunguzi huo ulibainisha kwamba rushwa ni tatizo katika udhibiti wa silaha. Lakini badala ya kufanyia kazi taarifa hizo, mamlaka husika zilikanusha.
Ni wajibu wa Serikali kukomesha uzagaaji ovyo wa silaha ili kukabiliana na vitendo vya ujambazi.
Mipaka yetu inavuja, hivyo wahamiaji haramu wameendelea kuingia nchini kwa njia za panya, huku mamlaka husika zikiwa hazionyeshi kujali au kujifunza kutoka kwa majirani zetu jinsi ya kuwadhibiti. 
Kwa mfano, ujambazi unaofanywa kwa kutumia bodaboda ungeweza kukomeshwa iwapo Serikali yetu ingejifunza kutoka Rwanda na Uganda ambazo zimefanikiwa, pamoja na mambo mengine, kudhibiti usafiri huo kwa kuhakikisha madereva wake wanahakikiwa na kuvaa sare, huku vyombo hivyo vikisajiliwa na kupewa namba na mwonekano maalumu.
Kuzagaa kwa silaha ni tatizo ambalo Serikali inapaswa kulitafutia dawa sasa.
Vinginevyo vitendo vya ujambazi wa kutumia silaha vitaliweka Taifa mahali pabaya, ambapo wananchi watalazimika kuishi kama wakimbizi katika nchi yao.
MWANANCHI

No comments: