Advertisements

Friday, September 19, 2014

Polisi, Chadema kivumbi

Jeshi la Polisi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana walitunishiana misuli na kusababisha kivumbi katika miji ya Dodoma na Dar es Salaam.

Kivumbi hicho kilitokana na Jeshi la Polisi kutaka kuzuia maandamano yaliyotangazwa na Chadema mikoa yote nchini bila kikomo kwa lengo la kupinga kuendelea kwa vikao vya Bunge Maalum la Katiba (BMK).

Jijini Dar es Salaam, zilizohusisha wafuasi wa Chadema na baadhi ya waandishi wa habari kukimbizwa ovyo na wengine kushambuliwa na kujeruhiwa kwa kupigwa virungu na mateke na askari polisi wa kikosi cha mbwa, jana ilizuka makao makuu ya Jeshi la Polisi, jijini Dar es Salaam na kuzua tafrani kubwa miongoni mwa watu waliokuwapo katika eneo hilo na maeneo ya pembezoni mwake.

Mwandishi aliyejeruhiwa, amefahamika kwa jina la Josephat Isango, wa kampuni ya Free Media.

Hali hiyo, ambayo ilidumu kwa takriban saa moja, ilizuka muda mfupi baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na masafara wake ulioshirikisha jopo la wanasheria, kuwasili kwa lengo la kuitikia wito uliomtaka afike eneo hilo ili akahojiwe na polisi.

Wito huo ulitokana na Mbowe kutuhumiwa na polisi kuchochea vurugu kwa kuitisha maandamano na migomo isiyokoma nchini kote ili kushinikiza Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea mjini Dodoma lisitishwe mara moja kabla ya Oktoba 4, mwaka huu.

Mbali na vurugu hizo, polisi pia walifunga barabara ya Ohio iliyotumiwa na Mbowe na msafara wake kufika makao makuu ya jeshi hilo.

Kabla ya Mbowe kuwasili katika viwanja vya makao makuu ya jeshi hilo majira ya saa 5.00 asubuhi, baadhi ya wafuasi wake walitangulia kufika katika eneo hilo.

Ulinzi mkali wa polisi, wakiwamo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliojiandaa kwa mapambano uliimarishwa katika eneo hilo.

Wanasheria wa Mbowe; Mabere Marando na Profesa Abdallah Safari walianza kuwasili eneo hilo saa 4.50 asubuhi na kuruhusiwa kuingia.

Vurugu hizo zilianza baada ya Mbowe na msafara wake kuwasili.

Alipofika katika lango kuu la kuingilia, wafuasi wake walianza kushangilia.

Hata hivyo, msafara wake ulikwama kwa takriban dakika 30 kabla ya kuruhusiwa kuingia katika eneo hilo.

Polisi waliokuwa wametanda katika lango hilo, wakiwamo wa kikosi cha mbwa, walianza kubishana na wafuasi wa Chadema baada ya kumzuia Mbowe kuingia na gari ndani ya eneo hilo.

Kutokana na mabishano hayo kuwa makali, polisi walilazimika kutumia mbwa kuwafukuza wafuasi hao wa Chadema kabla ya kumruhusu Mbowe na msafara wake kuingia na magari yao.
Pia waliwazuia baadhi ya wanasheria kuingia ndani hali iliyosababisha vurugu kati ya wafuasi na polisi.

Wengine waliozuiwa kwa muda katika lango la kuingilia walioongozana na Mbowe, ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Tanzania Bara, John Mnyika na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu.

Wanasheria wengine waliozuiwa kwa dakika kadhaa na baadae kuruhusiwa kuingia, ni Nickson Tugala, John Mallya, pamoja na baadhi ya wabunge, akiwamo Ezekia Wenje (Nyamagana) na Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) .

Majira ya saa 6:14, polisi walianza kuwafukuza wafuasi waliokuwa wamefurika eneo hilo, huku mmoja wa maofisa wa polisi akisema amri hiyo imetoka kwa uongozi wa juu.

Polisi hao walitumia mbwa, virungu na mateke kuwafukuza wafuasi hao na kumkamata mmoja wa wafuasi hao aliyejitambulisha kwa jina la Kamugisha Ngaiza.

Waandishi wa habari waliokuwa wamesimama eneo la karibu na lango la kuingilia walianza kufukuzwa na polisi kwa kutumia mbwa hali iliyosababisha baadhi yao kuanguka na kuumia.

“Wamenikuta ninaandika, wakanza kunipiga kwa marungu na mateke. Hata nilipowaonyesha kitambulisho, bado waliendelea kunishambulia kabla ya waandishi wenzangu hawajafika kuanza kunitetea,” alisema Isango, ambaye alikuwa akitembea kwa kuchechemea kutokana na kujeruhiwa mguuni.

Kitendo hicho kiliwaghadhibisha waandishi wa habari, ambao baadhi waliangua kilio.
Baadhi walilaumu kitendo cha jeshi hilo kutumia nguvu kubwa hata kwa waandishi wa habari huku wakifahamu kuwa wako kazini na hawafungamani na upande wowote.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari huku akilia kwa uchungu, mpigapicha wa magazeti ya Habari Leo na Daily News, Yusuph Badi, alisema vitendo vya polisi kunyanyasa waandishi wa habari vimezidi.

Alisema licha ya Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, kushauri jeshi hilo kushirikiana na wandishi wa habari katika kufanya kazi, polisi bado wameendeleza vitendo vya unyanyasaji dhidi ya waandishi.

Majira ya saa 7: 15, Mnyika alitoka nje na kuzungumza na waandishi wa habari akisema mahojiano kati ya polisi na Mbowe yalichelewa kuanza.

Alisema mahojiano yalipoanza, polisi walionyesha video ya mkutano mkuu wa Chadema uliohutubiwa na Mbowe na kudai kuwa hotuba yake inachochea vurugu.

Mnyika alisema walimtaka Mbowe kuandika maelezo ya kuchochea vurugu, lakini mawakili wake walimkataza kuandika maelezo hayo wakidai kwamba alichokifanya siyo uchochezi.

Baada ya kukataa walimtaka aandike maelezo ya kukataa kuchochea vurugu ambayo hayo ndiyo mawakili wake walimruhusu.

Saa 8:30 mchana, jopo la mawakili wake walitoka na kuzungumza na waandishi wa habari baada ya mahojiano kumalizika.

Akizungumza na waandishi wa habari, Lissu alisema mahojiano yalifanyika vizuri na kwamba Mbowe yuko salama na kuwataka wafuasi wake waondoke.

“Mahojiano yameenda salama na mwenyekiti atatoka kwa dhamana muda si mrefu. Hivi sasa dhamana inaandaliwa,” alisema.

Aliongeza: “Mwenyekiti akipewa dhamana atasindikizwa na ‘Eskoti’ ya polisi mpaka nyumbani au Chadema makao makuu, lengo wanasema ni kuzuia kusitokee vurugu kwa sababu mkiandamana naye wanaweza kutumia nguvu.”
Saa 9: 9 alasiri, Mbowe alitoka na kusindikizwa na magari mawili ya polisi; moja mbele na nyingine nyuma.

ENEO LA BUNGE ULINZI MKALI
Mjini Dodoma umeimarishwa ulinzi katika njia zote za kuingilia jengo la Bunge, huku barabara kutoka mjini hapa kwenda Dar es Salaam inayopita jirani na jengo hilo ikifungwa, wakati polisi wenye silaha za moto, mbwa, farasi na virungu, wakiwa wametanda kudhibiti wafuasi wa Chadema waliopanga kufanya maandamano ya amani.

Jana NIPASHE ilishuhudia watu kadhaa wakiwa wamekamatwa na kuingizwa ndani ya gari la polisi lenye namba za usajili PT 1980 kwa madai ya kutaka kufanya maandamano wakipelekwa makao makuu ya polisi mkoa. Kwa mujibu wa ratiba ya shughuli za BMK jana Kamati ya Uandishi ilikuwa ikikamilisha kazi ya kuandika Ibara za Rasimu ya Katiba.

Kazi hiyo inatarajiwa kukamilika Septemba Jumanne ijayo na siku itakayofuata itawasilishwa bungeni ili kuwapa wajumbe muda wa kutafakari Rasimu ya Mwisho ya Katiba.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Lukula, juzi alizuia kufanyika kwa maandamano hayo akisema ye yote atakayethubutu kushiriki anapambana na mkono wa dola. Mapema asubuhi jana, polisi walifunga barabara hiyo kwa utepe maalum wa rangi ya njano, huku wakiyazuia magari yote yaliyokuwa yakitumia barabara hiyo.

Askari wa Usalama Barabarani walikuwa na kazi ya ziada kuyaelekeza kutumia barabara mbadala na mengi yalikuywa yakipita barabara itokayo stendi kuu ya mabasi kupitia Chuo cha Ufundi Stadi hadi Chuo cha Biashara Dodoma na kuingia tena barabara kuu.

Magari ya polisi yalikuwa yakizunguka mitaani kufanya doria na katika wengine walikuwa wameweka kambi jirani na ofisi ya Chadema mkoa iliyopo mtaa wa Makumbusho na ofisi ya wilaya iliyopo eneo la Mji Mpya.

Baadhi ya magari hayo ni yenye namba za usajili PT 1153 Land Rover, PT 1980 Toyota Land Cruizer na T 213 Land Rover ambalo lilikuwa na polisi waliokuwa wamevaa kiraia huku baadhi yao wakiwa na bunduki.



Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Dodoma, Jela Kherry Mambo, aliliambia NIPASHE nje ya ofisi yake kuwa maandamano waliyopanga bado yapo palepale ingawa hakusema walitarajia kuanza saa ngapi.

“Maandamano yetu ya amani yapo pale pale, sasa hivi tunapanga mikakati ya namna gani tutashiriki…unajua eneo ambapo tulipanga kuanzia maandamano limezingirwa na polisi wenye bunduki, mbwa na farasi.

“Sasa lazima tujipange upya tuone tunaweza kufanyaje, lakini maandamano ya amani yapo pale pale kama tulivyokusudia.

“Tunaweza kufanya muda wowote, iwe mchana au hata usiku, ni lazima tupinge ufisadi huu unaofanywa wa kupoteza fedha za wananchi katika BMK,” alisema na kuongeza: “Wakati bunge hilo likiwa linaendelea, tunapenda kupeleka ujumbe wa amani kabisa, hatuna ugomvi.”

Alidai kuwa iwapo watafanikiwa kuandamana, polisi ndiyo watakaoleta vurugu kwa kusababisha mauaji au majeruhi kwa wananchi kwa sababu wameajiandaa kwa kuwa na silaha za moto.

“CCM ndiyo watakaoleta vurugu kwa kutumia vyombo vya dola…wanatumia nguvu kubwa mno kwa watu wanataka kufanya maandamano ya amani, tazama hatuna hata rungu,” alisema.

Wakati magari ya polisi yakizunguka hapa na kule, gari la Chadema (M4C) lenye namba za usajili T 792 CAX, lilikamatwa dakika chache baada ya kutoka ofisini hapo.

Hata hivyo, watu waliokuwa ndani ya gari hilo walidai kuwa walikuwa wakielekea Tabora kwa kazi za chama, lakini baadhi yao walionekana kuwa na mabango yaliyosomeka, “Tunapinga ufisadi unaofanya na Bunge Maalum la Katiba.”

Bango lilingine lilisomeka, “Samwel 6 No.”
Shughuli za kibiashara katika eneo la Nyerere Squire zilisimama jana, huku mfanyabiashara wa hoteli ya City Garden, Said Hassan Kaombwa, akilalamikia kupata hasara kubwa.
“Hakuna biashara leo, tunakula wenyewe chakula, hakuna wateja, ingawa polisi wanaruhusu watu kuja kupata chai na chakula, lakini wateja wanasita kuja katika hali kama hii ya ulinzi mkubwa.

“Tuliandaa vyakula kama kawaida, vipo, lakini hatukujua kama hali hii ingetokea,” alisema na kuongeza: “Hata hivyo, tuna imani hali hii pengine haitaendelea hadi jioni.”
Wafuasi na wanachama wa Chadema, juzi walipanga kufanya maandamano hayo kushinikiza Bunge Maalum la Katiba kusitisha shughuli zake kwa kuwa wajumbe wake hawajadili rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

Wanadai kuendelea kwa bunge hilo ni kupoteza bure fedha za wananchi kwa kuwa katiba itakayopatikana haitakuwa ya wananchi baada ya maoni yao yaliyokuwa kwenye rasimu hiyo kutupwa.

WATATU MBARONI
Jana jioni Jeshi la Polisi mkoani Dodoma lilitoa taarifa likisema kuwa liliwatia mbaroni watu watatu kwa tuhuma za kutaka kuandaa maadamano hayo.
Waliokamatwa ni Laurent Mangweshi (36), mkazi wa Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi;
Agnes Stephano (26) mkazi wa Dar es Salaam na Elisha Daudi (49), mkazi wa Tabora.
Taarifa hiyo ilieleza pia kuwa polisi walikamata gari lenye namba za usajili T.792 CAX aina ya Pick up Ford Ranger, mali ya Chadema iliyokuwa ikiendesha na Christopher Nyamwinja, mkazi wa Tabora.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, gari hilo lilikamatwa mtaa wa Kuu karibu na kituo cha mafuta cha Gapco likiwa na watu wengine watatu.

ARUSHA KUANDAMANA KESHO
Katika hatua nyingine, Chadema mkoani Arusha, kimeomba wananchi wote wakiwamo wale wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wajitokeze kesho katika maandamano ya kupinga Bunge Maalum la Katiba kuendelea.

Akizungumza jana na waaandishi wa habari jijini Arusha, Katibu wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Calist Lazaro, alisema maandamano hayo yataanza asubuhi eneo la Philips kwa kupita barabara ya Sanawari, Mianzini, Florida, Kituo Kikuu cha Mabasi, Uhuru Road, Kona ya Nairobi na kuishia Uwanja wa Samunge saa 10:00 jioni.

Alisema maandamano hayo yatapokelewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ambaye ni Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Calist alisema tayari barua zimeandikwa na Makatibu wa Majimbo ya Arusha yote tangu Septemba 17, mwaka huu na kupelekwa Polisi kutaarifu maandamano hayo na wanaomba ushirikiano wa Polisi, kwani hakutakuwa na uvunjifu wa amani.

NAPE: WANANCHI MSIANDAMANE
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM), Nape Nnauye, amewataka wananchi wasikubali kuandamana kama viongozi wa Chadema wanavyotaka.

Akizungumza akiwa wilayani Kisarawe jana, alisema kama Mbowe au kiongozi yeyote atawataka kufanya hivyo, wamueleze kuwa atangulize mkewe na watoto wake kwenye maandamano ambayo ameyaitisha kwa nchi nzima.

Nape alisema Chadema imekuwa na utamaduni wa kutumia damu za Watanzania kama sehemu ya mtaji wake kisiasa na kwa kuwa wanaokufa si wao wala familia zao, ndiyo maana wamekuwa wakiona fahari watu wanavyokufa.

Imeandikwa na John Ngunge, Editha Majura, Augusta Njoji, Paul Mabeja, Dodoma; Mary Godfrey, Kisarawe, Cynthia Mwilolezi, Arusha na Elizabeth Zaya, Dar.
 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: