Advertisements

Friday, September 19, 2014

Watoto wadaiwa kumuua baba yao Kagera

Kagera/Katavi. Polisi Wilaya ya Kyerwa, Mkoa wa Kagera wanawashikilia watoto watatu wa Kijiji cha Mkunyu, Kata ya Kikukuru wilayani Kyerwa kwa tuhuma za kumuua baba yao, Henry Siliakus (62) kutokana na mgogoro wa kifamilia.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Gilles Muroto alisema mauaji hayo yalifanyika Jumatatu wiki hii kijijini hapo.
“Uchunguzi wetu wa awali unaonyesha kulikuwa na ugomvi wa kifamilia, watoto walikuwa wanamlalamikia baba yao kwa kuuza chakula na kusababisha kukumbwa na njaa. Lakini kama hiyo haitoshi, baba yao alikuwa akitumia vibaya fedha hizo,” alisema Muroto na kuongeza;
“Wakati wa ugomvi huo, watoto walimshambulia baba yao kwa fimbo. Walimpiga kichwani na kusababisha kifo chake, tunasubiri taarifa ya daktari ili kujua aina ya kesi wanayotakiwa kufunguliwa na bado tunaendelea na upelelezi kabla ya kuwafikisha mahakamani.”
Alisema kuwa mmoja wa watoto hao anasoma kidato cha pili katika Sekondari ya Mkunyu, wengine wawili wanasoma Shule ya Msingi Mkunyu.
Adaiwa kuua mkewe kwa nyundo
Katika hatua nyingine, mwanamume mmoja mkoani Katavi anasakwa na polisi akidhaniwa alimuua mkewe kwa kumpiga nyundo kichwani kisha kuufungia mwili wa marehemu ndani ya nyumba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema tukio hilo lilitokea kijijini hapo Septemba 14, mwaka huu saa 1.30 asubuhi ambako mwanamke aitwaye Bernadeta Bwetel (38) mkazi wa Kijiji cha Uruwila Wilaya ya Mlele aliuawa.
Alisema kabla ya kifo hicho, enzi za uhai wake mwanamke huyo alikuwa akiishi pamoja na mume huyo na watoto wao wawili lakini mume wa marehemu alikuwa na mazoea ya kumpiga mara kwa mara.
Kidavashari alisema siku ya tukio, majirani zao Raphael Antony na Albert Mayamba wakielekea shambani walipita jirani na nyumba ya marehemu, walishtushwa na hali ya hapo ilivyokuwa, tofauti na siku zote ambazo huwa wanaikuta familia hiyo ikiwa hapo nyumbani na kuhisi kuna tatizo.
Majirani hao walikwenda kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa kijiji, ambaye aliongozana nao hadi kwa Mtendaji wa Kata, Didasi Buyaga.
Alisema baada kufika nyumbani kwa marehemu, walikuta mlango umefungwa kwa kamba kama ishara ya kuonyesha ndani ya nyumba hiyo hakuna mtu.
“Walipiga hodi lakini hawakujibiwa ndipo walipoamua kuvunja mlango na kuingia ndani na kukuta mwili wa marehemu ukionekana alipigwa na kitu kizito kichwani kinachodhaniwa kuwa ni nyundo lakini hawakumkuta mumewe wala watoto na hadi sasa hawajulikani waliko,” alisema.
Mwananchi

No comments: