ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 4, 2014

`Ukawa hawajaafikiana kusimamisha mgombea mmoja`

Mkurugenzi wa Halmashauri na Bunge wa Chadema,John Mrema.

Wakati vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vikishirikiana kusaka maridhiano baina ya makundi yanayohasimiana kuhusu mchakato wa katiba unaoendelea, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema bado havijaafikiana iwapo vitasimamisha mgombea mmoja anayekubalika katika nafasi yoyote ya uongozi kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Mkurugenzi wa Halmashauri na Bunge wa Chadema, John Mrema, alisema hayo jana mjini hapa alipotakiwa na wakazi wa Jimbo la Vunjo kutoa ufafanuzi iwapo vyama hivyo vimekubaliana kumsimamisha mgombea mmoja wa kiti cha ubunge jimbo hilo katika uchaguzi mkuu wa 2015.

Waliotangaza nia ya kugombea ubunge jimboni humo hadi sasa ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, John Mrema na Exaud Makyao (Chadema).

Jimbo hilo kwa sasa linawakilishwa bungeni na Augustino Mrema wa TLP aliyeshinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

John alisema kilichoafikiwa na Ukawa ni kila mtu kujenga chama chake na kwamba, hakuna makubaliano hadi sasa ya kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi ya urais, ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu ujao.

“Ieleweke kwamba, hatujakubaliana hadi sasa kumsimamisha mgombea mmoja wa urais, ubunge wala udiwani. Tulichokubaliana ni kila mtu aende akajenge chama chake. Kwa hiyo, niwatoe wasiwasi kwamba, NCCR–Mageuzi hawana mpango wa kutusaliti. Wanachofanya ni kujenga chama chao,” alisema Mrema.

Awali, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Taifa, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Kiwelu, akizungumza katika mkutano wa uchaguzi wa jimbo hilo, aliwataka wanachama wa Chedema kuhakikisha katika uchaguzi ujao wanawachagua watu waadilifu na siyo kuchagua marafiki zao kwani msingi wa chama unaangalia utendaji na siyo urafiki.

Katika matokeo ya uchaguzi huo yaliyotangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi, Kiwelu Herman Chenona alichaguliwa kuwa Mwenyekiti, wakati Katibu akichaguliwa Emanuel Mlacky na Katibu Mwenezi ni Charles Kaviche.
CHANZO: NIPASHE

No comments: