ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 5, 2014

UNAPOKUWA FARAGHA NA MWENZA WAKO, NI MAZUNGUZO GANI YAFAA -2

Tunaendelea na mada yetu tuliyoianza wiki iliyopita ya mazungumzo yanayofaa unapokuwa faragha na mwenza wako.Nianze kwa kuwashukuru nyote mliochangia mada hiyo kwa njia ya ujumbe mfupi kwa lengo la kupanuana mawazo.

Siwezi kuwataja kwa majina lakini nauheshimu mchango wa kila mmoja katika kuwekana sawa katika ulimwengu wa mapenzi ambao wengi wetu tunaishi ndani yake.Tunaendelea kuchambua mazungumzo yanayofaa ukiwa na mpenzi wako, ambayo yatamfanya apende kuendelea kukusikiliza na kupiga stori na wewe kila siku, hata kama mmeshakaa kwa muda mrefu katika uhusiano wa kimapenzi.

MKUMBUSHE JINSI MLIVYOKUTANA
Mkumbushe jinsi ulivyojisikia siku ya kwanza mlipokutana. Ni wazi kwamba kila mmoja alikutana na mpenzi wake katika mazingira tofauti kabisa. Hebu jaribu kukumbuka mambo mazuri yaliyotokea siku hiyo na mkumbushe mpenzi wako jinsi ulivyojisikia tangu mara ya kwanza ulipokutana naye.

Bila shaka mada hiyo itamfurahisha sana. Hata kama yapo mambo yasiyofurahisha ambayo yalitokea siku hiyo, usiyazungumzie badala yake mwambie jinsi moyo wako ulivyojawa na upendo wa dhati. Utashangaa jinsi hisia zake zitakavyorudi nyuma na kuwa mpya. Hata kama mmeishi miaka mingi, atakuona kuwa mpya kwake.

ZUNGUMZIA KUHUSU VITU ANAVYOVIPENDA
Imezoeleka katika jamii kwamba wanawake ndiyo watazamaji wazuri wa vipindi vya TV au tamthiliya huku wanaume wengi wakipendelea muvi au soka. Jenga utaratibu wa kuwa unafuatilia vitu anavyovipenda mwenzako.

Kwa mfano, kama wewe ni mwanaume na unajua mpenzi wako anafuatilia tamthiliya nzuri inayooneshwa kila wiki, jitahidi kuijua japo kidogo kisha mkiwa wawili, anzisha mazungumzo na mwenzako kuhusu tamthiliya hiyo.

Utashangaa utakavyoukonga moyo wake, kwani atakusimulia kuanzia mwanzo hata vitu ambavyo huvijui. Atajisikia raha kuzungumza na wewe kwa sababu atajua unajali vitu anavyovipenda.

Kama wewe ni mwanamke na unajua mumeo anashabikia timu fulani ya soka, jitahidi japo kuwajua wachezaji wachache wa timu husika na ratiba zake kisha ukiwa na mumeo, anzisha mada hiyo. Atafurahi sana na mtazidi kuuboresha ukaribu wenu.

WAJUE MARAFIKI ZAKE
Kuwajua marafiki wa mpenzi wako, huwa ni hatua nyingine ambayo itakusogeza jirani zaidi na mpenzi wako. Simaanishi kwamba uanze kuchunguza udhaifu wa marafiki zake, uwe na mazoea nao au uwe na namba zao za simu! Hapana.

Wajue kwa majina, kazi wanazozifanya na maisha yao japo kwa kifupi ili mpenzi wako anapokupigia stori za rafiki yake fulani, uwe angalau unamjua kidogo na kuchangia naye mazungumzo.

Kuwajua marafiki zake, kunaweza pia kukusaidia kuijua vyema tabia ya umpendaye na kuweza kumdhibiti mapema au kumpa msaada pale anapohitaji ili wasije wakavuruga uhusiano wenu (maana marafiki wengine hawaaminiki).

MUULIZE MATUKIO YALIYOWAHI KUMFURA-HISHA
Unaweza kuona kama masihara lakini utafiti unaonesha kwamba mtu yeyote anaposimulia historia ya maisha yake, hasa matukio yaliyowahi kumfurahisha sana alipokuwa mdogo, huzirudisha nyuma hisia zake na kumuona mtu anayemsikiliza kama sehemu ya kumbukumbu hizo nzuri.

Muulize umpendaye kuhusu mambo ambayo huwa akiyakumbuka yanamfurahisha sana kisha msikilize kwa makini. Atajisikia raha sana anapokusimulia na wewe ukaonesha kufurahi kama yeye alivyowahi kufurahi. Ukaribu wenu utazidi kushamiri.

MFANYIE MAMBO MAZURI
Binadamu wengi tunapenda kufanyiwa mambo mazuri hasa na watu tunaowapenda. Mwenzi wako naye yupo hivyohivyo, hata kama hakuambii elewa kwamba anatamani sana kufanyiwa mambo mazuri na wewe.

Mnunulie zawadi ndogondogo, mtoe ‘out’ kila unapopata nafasi, mshirikishe kwenye mipango yako ya maendeleo na mambo mengine yanayokuhusu, utashangaa jinsi atakavyozidi kukupenda na kutamani muda wote awe pembeni yako.

Epuka mambo ya kumuudhi kama kumtukana, kumpiga, kumfokea au kumsema vibaya kwa watu wengine kwani utakuwa ukiurudisha nyuma moyo wake na kasi ya kukupenda na kupenda kukaa karibu na wewe, itapungua.

Ni hayo tu! Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Kama kuna mada ungependa tuijadili, nitumie sms kwa namba za hapo juu.
GPL

No comments: