Advertisements

Monday, October 20, 2014

Ali Ameir: Sitasahau mauaji ya Mwembechai

Asema alipata wakati mgumu akitishiwa itikafu
Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani katika serikali ya awamu ya tatu, Ali Ameir Mohamed, amesema hatasahau vurugu za Mwembechai zilizohusisha Jeshi la Polisi na baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu mwaka 1998 kwani ndiyo mgogoro mkubwa uliotokea chini ya uongozi wake wakati akiwa mtumishi wa umma.

Akizungumza katika mahojiano maalum na NIPASHE nyumbani kwake Donge Kichavyani, katika Shehia ya Mbiji, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ameir alisema alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alikumbana na changamoto nyingi lakini tukio hilo kwenye eneo la Msikiti wa Mwembechai hatalisahau na kwamba hadi sasa bado linamsononesha kwa vile mauaji yalitokea baada ya watu kupotoshwa.

Katika vurugu hizo zilizotokea Februari 13, 1998, watu wawili walidaiwa kufariki dunia baada ya kupigwa risasi na polisi huku wengine kadhaa wakijeruhiwa, akiwamo kijana aliyepata ulemavu, mwanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya Sekondari ya Al-Haramain ya jijini Dar es Salaam, Chuki Athumani. Hata hivyo, jeshi hilo lilisema kuwa aliyeuawa ni mtu mmoja na wengine kadhaa walijeruhiwa.

Ameir ambaye pia aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, alisema kuwa alisikitishwa na vurugu hizo kwani kuna watu walitumia imani kupotosha na mwishowe kusababisha watu wengine wapoteze maisha na wengine kujeruhiwa vibaya.

“Kuna kijana mpaka leo ananijia machoni. Siwezi kumsahau, aliumizwa kwa risasi katika mgogoro huo… mtoto yule mpaka leo namkumbuka. Ni kijana mdogo ambaye alikuwa anasoma (sekondari) Al-Haramain. Alipoteza viungo vyake vya mwili na kuwa mlemavu,” alisema Ameir.

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Al Haramain ya jijini Dar es Salaam aliyepata ulemavu baada ya kujeruhiwa kwa risasi katika tukio la Mwembechai ni Chuki Athumani, ambaye wakati huo alikuwa akisoma kidato cha pili.

TISHIO LA ITIKAFU
Ameir alisisitiza kuwa vurugu za Mwembechai ndiyo mgogoro pekee asiousahau katika maisha yake ya utumishi wa serikali na kwamba, alijikuta akiwa katika wakati mgumu kutokana na vitisho alivyokuwa akipokea baada ya kutokea kwa mauaji.

Alieleza zaidi kuwa kuna watu walimtishia kuwa watamkalia itikafu (kikao cha kufanya maombi maalum) ili adhurike, lakini Mungu alimsaidia na kwamba kuna watu walikuwa wakimpa moyo na kumtaka aendelee kutekeleza majukumu yake ya uwaziri.

“Yupo Sheikh alinitia moyo kuwa nitimize wajibu wangu wa uwaziri kwa kuwa itikafu ina miiko yake,” alisema Ameir na kuongeza: “Mgogoro huo ulinisononesha na unaendelea kunisononesha hadi leo.”

Kwa mujibu wa wanazuoni wa Kiislamu, kilugha neno itikafu lina maana kuu mbili, ambazo ni kuzuia na kukaa. Kadhalika, inaelezwa kuwa kisheria, Itikafu” ni kitendo cha kukaa msikitini kwa mfumo maalumu uambatanao na nia ya kujikurubisha kwa Allah (Mwenyezi Mungu) kwa kutekeleza ibada mbalimbali.

Wanazuoni wanaeleza zaidi kuwa miongoni mwa mambo anayotakiwa kuyafanya mtu mwenye kukaa itikafu ni pamoja na kusoma Qur-an Tukufu, kuleta nyiradi mbalimbali (kumdhukuru Allah kwa wingi), kuleta istighfaari (kumuomba Allah msamaha wa dhambi), kumswalia Mtume Muhammad (S.A.W) na kuomba dua.

UTUMISHI SERIKALINI
Alisema katika uongozi wake wa nafasi mbalimbali ikiwamo ya uwaziri wa Mambo ya Ndani, jambo ambalo ulikuwa akilipigania zaidi ni kuwatumikia wananchi vizuri kutokana na nafasi aliyopewa.

Alisema alifanya hivyo ili kufanikisha utendaji kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za kazi alizopangiwa, huku akiepuka uonevu na upendeleo na kuhakikisha kwamba daima haki inatendeka.

“Naweza kujisifu kwamba niliondoa kabisa ubinafsi. Hata siku moja sikufikiria kuwa kazi ya umma ni mbinu au ndiyo kazi ya kujitajirisha. Nilijitahidi sana kukwepa hilo na kwa kweli, mimi ni miongoni mwa wastaafu ambao hawana kitu… ni kwa sababu nilikataa vishawishi vyovyote. Kwanza vya kuviibia vyombo nilivyovifanyia kazi, lakini pia vya kupokea vishawishi vya rushwa na hongo ili nimpendelee mtu.

Kwa kweli nimejitahidi sana, na nimemaliza bila ya kunyooshewa kidole,” alisema Ameir, ambaye wakati wa awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa aliwahi pia kuwa Waziri wa Habari.

Alisema ingawa alipata matatizo ya hapa na pale wakati wa kulitumikia taifa, lakini hakujali kwa kuwa lengo lake lilikuwa ni kuitumikia nchi na wananchi kwa ujumla, hivyo hakujali yote yaliyotokea.

KUGOMBEA UONGOZI
Alisema ingawa bado ana nguvu na akili yake ingali ikifanya kazi vyema, lakini kwa sasa hana nia ya kutaka kugombea nafasi yoyote ya uongozi kwani ameridhika na kustaafu kwake, isipokuwa yupo tayari kutoa msaada kwa taifa na chama chake.

Alisema amekuwa akitoa mchango wake kwa chama chake kutokana na kuitwa katika vikao vya mkoa na kwamba mara kadhaa amekuwa akisaidia kuipa serikali ushauri kwa mambo anayoweza.

TUHUMA ZA UFISADI ZANZIBAR
Akizungumzia madai ya kushamiri kwa vitendo vya ufisadi vinavyofanywa na baadhi ya watu wasio waaminifu ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Ameir alisema ni kweli kuna kilio hicho cha kukithiri kwa vitendo vya ufisadi katika baadhi ya ofisi za umma Zanzibar, jambo ambalo linarudisha nyuma jitihada za Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) katika kuwaletea maisha bora wananchi wake.

Hata hivyo, alisema vitendo vya ufisadi siyo changamoto kwa Zanzibar tu, bali ni kwa Afrika nzima, ingawa ni kwa viwango tofuti.

“Duniani watu wote wameumbwa na ubinafsi fulani. Lakini nchi za wenzetu (zilizoendelea) wamejiwekea misingi inayowazuia watu kuendeleza ubinafsi wao zaidi na kudharau umma… lakini tatizo hili bado tunalo Afrika,” alisema.

Alieleza kuwa baadhi ya viongozi waliopewa madaraka katika nafasi mbalimbali wameweka ubinafsi mbele ikiwamo katika vyama vya siasa na matatizo yanayotokea Afrika leo hii. Moja ya chimbuko lake kubwa ni hilo kwa sababu wananchi waliwapa madaraka.

“Wanapofika mahala wakiona hawawatumikii, na wakianza kuchukia, ndipo wanapoanza vurugu. Ndiyo maana Bara la Afrika limebaki kuwa ni Bara la machafuko,” alisema na kuendelea:

“Mimi ni miongoni mwa wananchi wanaosikitika kwa sababu viongozi wanapopewa madaraka huwa wanalipwa, lakini (baadhi) huwa hawatosheki. Ubinafsi ni moja ya maumbile ya binadamu, lakini tumetofautiana na wenzetu (nchi zilizoendelea) kwa sababu taratibu zao za kisheria na kikanuni zinawadhibiti.”

Alishauri kuwa ni vizuri kama Katiba itafanikiwa ikafuatiliwa vizuri kuwadhibiti wahalifu na kujaribu kutengeneza sheria na kanuni ambazo mtu mwenyewe zinambana, hivyo ataamua kufanya kazi za umma au kukaa nje.

“Unapopewa utumishi wa umma ni vyema kuweka mbele maslahi ya wananchi na ndiyo maana unalipwa, lakini wengi wao hawafanyi hivyo, ndiyo kwanza wanaona kuwa hiyo ndiyo ngazi ya kuwa matajiri, hadi familia yao,” alisema.

UTAWALA BORA
Akizungumzia utawala bora, Ameir alisema lengo lake ni kuleta haki kwa kila mtu na siyo kwa maslahi binafsi na baadhi ya watu kuwadhulumu wengine.
Alisema: “Kama kuna fursa ya elimu na afya, basi kila mtu apate. Lakini pia kuwapo na uwajibishaji kwa mafisadi. Na tunaposema tumepiga hatua katika utawala bora, basi tulinganishe tulipo na tulipotoka.”

Alisema Zanzibar japo nchi ni ndogo, lakini yeyote akisikia kiwango cha ufisadi unaoendelea sasa atasikitishwa.
Alisema kuwa awali Zanzibar hapakuwa na ufisadi na kwamba, siri yake wakati huo ni vijana kuwa wakilelewa na kukulia katika misingi ya maadili.
“Hata mlevi wa zamani Zanzibar alikuwa hajionyeshi maana aliona atatengwa... Lakini sasa hivi hali imebadilikia. Jitihada za kuiibia serikali ni kubwa, ndiyo maana zipo shughuli zimekwama kwa sababu ya ufisadi. Mimi nafikiri vyombo vya sheria vijitengenezee utaratibu bila ya kuoneana haya na kuyabana mambo ya ufisadi,” alisema Ameir.

MATUMAINI
Kwa mujibu wa Ameir, Zanzibar inaweza kuendelea kwa muda mfupi kwani ina watu wachache ikilinganishwa na nchi nyingine. Hata hivyo, alisema hilo litawezekana ikiwa hatua zitachukuliwa kuhakikisha kuwa na sera nzuri zitakazotekelezwa kwa uaminifu na kuziba mianya yote ya ufisadi.

“Sasa kuna minong’ono mingi, hata kama ni siyo sahihi au siyo sahihi, lakini lisemwalo lipo na kama halipo linakuja, hivyo ni vyema ukafanywa uchunguzi maalum na kubaini kuwa ni wapi kuna mianya ya ufisadi,” alisema.

UCHUMI
Akizungumzia uchumi, Ameir alisema: “Ni tatizo la Afrika na hata Tanzania, waziri akisoma Bajeti atakwambia uchumi umekua. Lakini ukimuuliza mwananchi wa kawaida, atakwambia haoni uchumi kukua, na atakwambia umaskini (ndiyo) unaongezeka.”

Alisema linaonekana lipo tatizo katika Afrika kuhusiana na namna ya kukua kwa uchumi na kushauri kuwa sasa kukua kwake kunapaswa kutafsiriwa katika hali ya maendeleo ya wananchi na wananchi wakaridhika. Alisema siyo mtaalamu wa uchumi, lakini anaona hilo bado halijafanyika Afrika.

Alisema tatizo lililopo ni mipango mingi ya serikali kutoeleweka kwa wananchi, uchumi unakua vipi na kwamba katika Afrika kitu kinachowaathiri wananchi ni bei za mahitaji ya msingi kama nguo na chakula.

“Kama mwananchi kila akienda katika bucha akakuta bei ya nyama inaongezeka, huwezi kumwambia kuwa uchumi unakua. Wakati sasa (Zanzibar) nyama kilo Sh. 10,000… huwezi kumwambia (mwananchi) uchumi umekua akakuelewa,” alisema Ameir.

Alisema mwananchi anaridhika kuona bei ya bidhaa hazipandi au zinapungua, lakini akiona zinapanda hawezi kuelewa kukua kwa uchumi.

MAFUTA
Akizungumzia kuhusu Zanzibar kuwa rasilimali ya mafuta na neema hiyo imekuwa chanzo cha kutetereka kwa mahusiano baina ya Zanzibar na Bara, alisema hana uhakika na hilo, lakini kuna watu wanaosema wana ushahidi kuwa mafuta yapo.

Alisema katika miaka ya karibuni, walifika wataalalamu kutoka nchi mbalimbali na kusema yapo mafuta na zipo nchi zimeonesha kuwa na hamu ya kuchimba, lakini kikwazo zaidi ni suala la Muungano.

Alisema bahati nzuri suala hilo limekuwa miongoni mwa masuala yaliyokuwa yakizungumzwa katika mikutano mbalimbali, lakini jambo zuri ni kwamba sasa mchakato wa katiba mpya unakaribia kumalizika na kwamba ana imani tatizo hilo litaondoka.

“Kwa kweli moja ya hoja kwa Zanzibar kuipitisha rasimu japo ina kasoro fulani ni hilo la kiuchumi … kwa sababu Katiba ile sasa ikipita, basi siku ya tatu (tu) Zanzibar inaweza kuchimba mafuta kama kweli yapo. Kama hiyo Katiba ina uwezo huo, suala hili litakwisha maana suala la mafuta limetuletea matatizo ya kisiasa,” alisema.

Aliwataka Wazanzibari waipigie Katiba inayopendekezwa kura ya ndiyo ili kuyapata hayo mafuta na penye manufaa waweze kunufaika.

“Mimi kama Ali, nasema mafuta siyo mwarobaini wa matatizo ya watu, tutajidanganya tukifikiri kwamba mafuta ndiyo yataweza kuondoa matatizo yote, yangeondoka nchi za arabuni, Nigeria, Libya na kadhalika. Inabidi tuwe waangalifu. Pengine hayo mafuta yapo, (lakini) kama hamna utawala bora, na kama hatuna viongozi wazalendo, yanaweza kuwa chanzo cha machafuko zaidi,” alisema.

Alisema kama mafuta yapo na kama Katiba itapitishwa, anawaomba viongozi watakaokuwapo wazingatie utawala bora ili mafuta hayo yawe neema na siyo laana.

“Yawezekana mafuta haya yakaja, lakini wakaja wajanja wakaona mafuta hayo ndiyo nafasi ya kujitajirisha wao, ndiyo itakapotokea, tujifunze kwa nchi za wenzetu ambazo hazikaliki na chanzo ni hayo mafuta kama Iraq, Nigeria na Libya ambazo zina utajiri mkubwa wa mafuta, lakini hakukaliki,” alitahadharisha.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Huyu jamaa anaakil safi na mawazo safi