Kocha Mkuu wa timu ya Yanga Marcio Maximo akiuzungumza na vyombo vya habari
Bosi huyo raia wa Brazil amekuwa akitumia nguvu kubwa mazoezini akitaka Yanga ishinde kwa kishindo uwanjani lakini jambo hilo limekuwa kinyume ambapo imekuwa ikishinda kwa mabao machache.
MATOKEO iliyopata Yanga kwenye mechi mbili za awali za Ligi Kuu Bara hayajamfurahisha Kocha Marcio Maximo. Na hata alipokaa chini kutafakari na uongozi akataja mambo kadhaa ambayo Mrisho Ngassa ni miongoni mwa wachezaji wanaohusika.
Bosi huyo raia wa Brazil amekuwa akitumia nguvu kubwa mazoezini akitaka Yanga ishinde kwa kishindo uwanjani lakini jambo hilo limekuwa kinyume ambapo imekuwa ikishinda kwa mabao machache.
Katika mechi mbili ilizocheza Yanga imefungwa mabao 2-0 na Mtibwa mjini Morogoro na iliporudi Dar es Salaam ikaichapa Prisons mabao 2-1 lakini ikacheza kwa kiwango ambacho hakijamuingia akilini Maximo na sasa amewaambia viongozi kwenye mazungumzo ya faragha kwamba atafanya uamuzi mgumu.
Maximo amejitetea kwa viongozi kuwa baadhi ya wachezaji wanacheza vizuri lakini wanaremba sana hata muda ambao haustahili na hilo ameliona kuanzia kwenye video ya mechi ya Mtani Jembe dhidi ya Simba iliyomalizika kwa mabao 3-3. Katika mchezo huo Yanga ndiyo iliyoanza kushinda lakini Simba ikarudisha yote.
Maximo amewaambia viongozi kwamba amebaini wachezaji wanaridhika na matokeo mapema ndani ya uwanja na kushindwa kutafuta ushindi mkubwa. Bosi huyo tayari amekuwa mkali kwa wachezaji wake wazoefu akiwemo Mrisho Ngassa ambaye amemtaka kupunguza kuremba vinginevyo anaweza kuanzia benchi na kutoa nafasi kwa Simon Msuva. Mbali tatizo hilo Maximo ameueleza uongozi kwamba wachezaji wengi wana tatizo la kutokukaba hivyo analifanyia kazi kwa nguvu zote ingawa itatumia muda kulifuta.
Maximo ameonya baadhi ya wachezaji kuachana na mpira wa kufurahisha majukwaa bali watekeleze majukumu yao. “Kocha anataka kama kuna uwezekano wa timu pinzani kufungwa hata saba ifungwe tu lakini sio tukipata bao moja au mawili wachezaji waanzishe mbwembwe ambazo ndizo zimekuwa zikiipotezea timu ushindi mkubwa,”alidokeza mmoja wa vigogo wa Yanga.
“Ametuambia kwamba anataka kutengeneza nidhamu ya timu uwanjani na kwamba wapo wachezaji watakaoathirika na hili endapo atambaini mchezaji yeyote kufanya vituko wakati timu inahitaji ushindi,” aliongeza.
Katika mazoezi ya jana Alhamisi asubuhi Maximo katika kikosi chake cha kwanza ambacho huenda kikaanza kwenye mechi na JKT Ruvu Jumapili, Ngasa hakuwepo kwenye nafasi yake iliyochukuliwa na Msuva aliyecheza sambamba na Jerry Tegete.
Tegete aliziba nafasi ya Genilson Santos ‘Jaja’ aliyekuwa nje baada ya kuumia kifundo cha mguu juzi mazoezini huku mabadiliko mengine yakiwa kwa kiungo wa kati ambapo Salum Telela ambaye alianzishwa ingawa baadaye Hassan Dilunga alirudishwa.
Credit:Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment