Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo
Na Goodluck Eliona, Mwananchi
Dar es Salaam.
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema kuwa hali ya afya yake inaendelea kuimarika. na kuwataka waumini kuendelea kumwombea.
Akizungumza kwenye Misa Takatifu ya Mavuno na shukurani kwa jimbo hilo, iliyofanyika jana Msimbazi Center jijini Dar es Salaam, Pengo alisema ameamua kuitumia siku hiyo kumshukuru Mungu kwa kuwa ndiye alimfanya kuwa hai hadi sasa.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nawashukuruni nyote kwa sala zenu na dua zenu zilizoniwezesha hata kusimama hapa mbele yenu saa hizi kama mnavyoniona,” alisema huku akishangiliwa na mamia ya waumini wa kanisa hilo.
Alitumia muda huo kuwaasa waumini kuwa na tabia ya kushukuru kutoka ndani ya mioyo yao, akisema ndilo jambo linalompendeza Mungu.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 70, ambaye ameshatangaza kustaafu miaka mitano ijayo, alisema kuwa kila muumini anapaswa kutambua kuwa Mungu humtendea mema mwanadamu hata kama ni dhaifu.
Aliongeza kuwa si vyema kwa mtu aliyepona ugonjwa kusema kuwa amepata nguvu ya kwenda kuiba, kunyanganya watu na kufanya mambo mengine maovu.
Bila kutaja ugonjwa unaomsumbua, Pengo alimuomba Mungu asimrudishe tena kwenye hali ya udhaifu aliyoipitia kutokana na ugonjwa huo.
Akihubiri katika ibada maalumu ya misa iliyoandaliwa na Utume wa Wanaume Katoliki (Uwaka) katika Kituo cha Kiroho Mbagala, Oktoba 14, mwaka huu, alisema kuwa watu wengi hata wasiokuwa wakristo wamekuwa wakimpigia simu kumjulia hali.
“Najua wengine wanashangaa kuona askofu wao akitembea namna hii, kwa mkongojo, hivi ndivyo ilivyo, nilikuwa mgonjwa, lakini nawashukuruni nyote kwa kuniombea, Mwenyezi Mungu awabariki,” alisema kiongozi huyo na kuibua vifijo kutoka kwa mamia ya waumini walioshiriki misa hiyo.
No comments:
Post a Comment