Rais Kikwete anatarajiwa kuchukua Uenyekiti wa EAC baada ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki uliopangwa kufanyika jijini Nairobi, Kenya, Novemba 29 na 30 mwaka huu.
Mwenyekiti wa sasa wa EAC, Rais Uhuru Kenyatta, wa Kenya anamaliza muda wake mwezi huu na Raia Mwema limeelezwa kwamba mtihani wake wa kwanza utakuwa namna atakavyotatua mzozo uliopo sasa miongoni mwa wabunge wa EALA.
Bhanji, mbunge kutoka Tanzania, anadaiwa na baadhi ya wabunge, hasa kutoka nchi za Rwanda, Kenya na Uganda, kutoa lugha chafu dhidi yao na viongozi wa kitaifa wa nchi zao, tuhuma ambazo mwandishi huyo wa habari wa zamani anazikanusha.
“Baadhi ya wabunge wako tayari kulizungumza suala hili na kulimaliza lakini wapo wabunge ambao wanasema haliwezi kuisha bila ya Bhanji kuondolewa kwenye ubunge wake.
“Vikao vya Bunge vilivyopangwa kufanyika Rwanda havikufanyika mwezi uliopita. Wabunge wa Rwanda walisusia vikao vilivyofanyika Dar es Salaam. Huku Kenya hatujui kama vikao vitafanyika ingawa kuna watu wanataka suluhu ifanyike.
“Hoja inayotolewa hapa ni kwamba; Hivi hawa wabunge walichaguliwa kwa ajili ya kujadili watu? Kuna mambo ya msingi ya kujadili na kuyaacha kwa sababu ya mtu mmoja tu itakuwa dhambi kubwa kwa Watanzania,” alisema mmoja wa wafanyakazi katika Sekretarieti ya EAC iliyoko Arusha kwa masharti ya kutotajwa jina.
Raia Mwema lina taarifa kwamba lipo kundi la wabunge ndani ya EALA linaloshinikiza hata vikao vilivyopangwa kuanza Nairobi wiki hii visifanyike, ili iwe rahisi kwa Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard Sezibera, kumpa ripoti Kikwete kwamba shughuli za EALA zinakwama kwa sababu ya Bhanji.
Wabunge, hasa wa nchi hizo tatu, wanadai kwamba Shy-Rose aliwatolea maneno machafu wao binafsi na marais wa nchi zao wakati wakiwa safarini kwenda Makao Makuu ya Bunge la Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) jijini Brussels, Ubelgiji hivi karibuni.
Katika mahojiano aliyofanya na gazeti hili wiki hii, Bhanji alikiri kuwepo kwa kupishana lugha baina yake na wabunge wenzake wakati wa safari hiyo ingawa hakumtukana kiongozi yeyote na kwamba suala hilo limekuzwa kwa sababu nyingine.
Bhanji anaeleza kwamba matatizo yake na wabunge wa Uganda, Rwanda na Kenya yametokana na msimamo wake wa kumtetea Spika wa Bunge hilo, Margaret Zziwa, ambaye sasa hatakiwi na baadhi ya wabunge wa nchi hizo.
Alisema wapo wabunge katika nchi hizo ambao wanamuunga mkono na akasema juhudi za wabunge hao kumng’oa Zziwa zinaongozwa na Mbunge wa EALA kutoka Uganda, Dorah Byamukama, ambaye aliwania Uspika na Zziwa na kushindwa katika uchaguzi uliofanyika mjini Arusha.
“Kwenye ajenda ya kumuondoa madarakani Zziwa, nilisimama kidete kwa kutounga mkono kwa sababu haikuwa na maslahi ya Tanzania na yalikuwa kinyume cha malengo ya ushirikiano wa Jumuiya nzima.
“Hoja ya kumuondoa Spika ilikuwa ni sehemu ya ‘mchezo mchafu’ wa ajenda ya siri ya kumweka kwenye nafasi hiyo mjumbe mwingine kwa maslahi ya wachache.
“Jaribio hili la kumuondoka Spika lilifanywa na kushindikana mara tatu baada ya kukosa sahihi za kutosha kutoka Tanzania, ikiwamo ya kwangu.
“Baada ya kampeni ya kumwondoa Spika kushindwa, wabunge kadhaa walikuwa wanasusia vikao vya Bunge wakati wameshachukua posho za vikao. Kwa mfano kikao kilichofanyika hivi karibuni hapa Dar es Salaam.
“Malumbano ndio yamekuwa yakitawala na kuinyima Bunge akidi ya kuendelea na ajenda za mtangamano. Huu ni usaliti wa wazi kwa nchi zilizowachagua na kuwatuma katika Bunge la EALA.
“Kwa mfano, shutuma kwamba nililewa pombe ndani ya ndege, kuvunja chupa, kufanya fujo na kufungwa pingu wakati wa safari ya Ubelgiji si kweli hata kidogo.
“Kama hizi tuhuma ni za kweli, kwanini hazikupelekwa polisi, serikalini au vyombo vingine vya sheria baada tu ya tukio?
“Ninayo heshima kubwa sana kwa marais wa nchi zote tano na raia wa nchi wanachama ambako mara zote nimepokewa na kuishi kwa amani na upendo katika nchi hizo. Naahidi kuedeleza heshima hii. Hainiingii kichwani ni wapi nilipoteza heshima hii isipokuwa kwa wale
“Mimi ni Mtanzania na ni Mbunge wa Tanzania. Hivyo nina wajibu wa kulinda na kutetea maslahi ya Watanzania ili kuleta mtangamano wenye uwiano sawa kwa nchi zote wanachama.
“Ninaahidi nitaendelea kuwatumikia Watanzania kwa nguvu zangu zote na kutoa ushirikiano kwa wabunge wengine wa EALA kwa manufaa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Nimeyasema haya nikiamini kuwa: ‘Uongo ukiachwa usemwe mara nyingi unaweza kuaminiwa kuwa ni ukweli’, alisema.
Tanzania ina wabunge tisa EALA na katika hao ni wawili tu ndiyo wanaodaiwa kuunga mkono Zziwa kuondolewa madarakani, huku wengine saba wakipinga hatua hiyo.
Kwa mujibu wa kanuni, ili wabunge wafanikiwe kumuondoa Spika ni lazima wabunge wanne kutoka katika nchi tano wanachama wa EAC wapige kura ya kutokuwa na imani naye na kwa idadi ya wabunge wa Tanzania wanaopinga, hatua hiyo imeshindikana.
Ingawa wabunge hao wamechachamaa kutaka Bhanji aondolewe kuwa Mbunge, hatua hiyo ni ngumu kwa vile uamuzi kama huo unatakiwa kuchukuliwa na mamlaka iliyomchagua.
Bhanji pia anaweza kukoma kuwa Mbunge endapo Rais Jakaya Kikwete atamteua kuwa Waziri katika Serikali ya Tanzania au kumpa wadhifa mwingine wowote utakaomfanya ashindwe kutimiza majibu yake ya kibunge.
Gazeti hili limeambiwa ndiyo sababu wabunge hao wameamua suala hilo likabidhiwe kwa Kikwete wakati atakapopewa Uenyekiti wa EAC.
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz
No comments:
Post a Comment