Advertisements

Friday, November 28, 2014

CHENGE, CHENGE, CHENGE TENA?

Makala: Ojuku Abraham wa GPL
KAMA Mwalimu Julius Kambarage Nyerere angekuwa bado anatawala nchi hii, ni watu wachache sana wangeweza kulijua jina la Andrew Chenge, yule mwanasheria mkuu wa zamani wa serikali, aliyekaa katika ofisi hiyo kubwa na yenye heshima, kuanzia mwaka 1993 hadi 2005.

Lakini katika nchi ambayo inaendeshwa kwa hila na dili, jina hili linajipatia umaarufu na kuenziwa, bila kujali ni kwa kiasi gani, Watanzania zaidi ya milioni 45 wanaishi kwa dhiki na mateso kutokana na yeye kuitumia vibaya ofisi ya umma kujinufaisha.

Ni katika kipindi chake akiwa mwanasheria mkuu wa serikali, ndipo nchi yetu imeshuhudia kashfa za mikataba mingi mibovu, isiyo na tija kwa nchi, ikisainiwa. Siyo tu mikataba bali hata sheria nyingi zisizofaa zikilazimishwa kutumika.

Orodha ya kashfa zake ni nyingi, lakini hapa nitatoa chache, ili tujiulize, kwa nini mtu huyu bado anaaminika kiasi eti cha kupewa hadi uenyekiti wa kuandika Katiba Mpya Inayopendekezwa?

Huyu ndiye alikuwa mwanasheria mkuu wa serikali katika skendo zote kubwa zinazohusu fedha za umma kuibiwa, kuanzia Meremeta Gold Mine, ununuzi wa ndege ya rais, ununuzi wa Rada na EPA. Katika skendo ya Tegeta Escrow, ambayo imeibuka akiwa nje ya ofisi, amepewa mgawo kwa sababu anajua kila kitu kuhusu IPTL, maana wakati ‘wezi’ hawa wanakuja, alikuwa ofisini.

Siyo hivyo tu, huyu jamaa akiwa mwanasheria mkuu wa serikali, ndiye aliyeshinikiza kupitishwa kwa sheria mbovu ya takrima, ambayo kimsingi ni rushwa. Wakati sheria ya kupinga matokeo ya ubunge

mahakamani ikimtaka anayepinga kulipia shilingi milioni tano inapitishwa, alikuwa pale akiiwakilisha serikali!Kama Jaji Frederick Werema katika skendo moja tu ya Tegeta Escrow amesababisha serikali kukosa shilingi bilioni 20 kama kodi, huyu mtu aliisababishia nchi hii hasara ya mabilioni mangapi katika mandingo yake yote? Kwa nini bado anapeta?

Kama tutasema kila kitu ambacho Chenge amekifanya katika kuharibu uchumi wa nchi hii, hatuwezi kumaliza, lakini lugha yake ya kejeli wakati akiulizwa kuhusu fedha alizoweka katika Kisiwa cha Jersey kule Uingereza katika ile skendo ya ununuzi wa Rada, yanaonesha kuwa ana fedha nyingi alizochota.

Zaidi ya shilingi bilioni moja aliziita vijisenti, akimaanisha alikuwa na zaidi ya hizo na kwamba hata wenzake nao wanazo nyingi pia.

Halafu, CCM inamteua kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Katiba Mpya Inayopendekezwa. Ndiyo maana akabariki viondolewe vifungu muhimu kabisa kama vya maadili, ukomo wa ubunge na kuondoa nguvu ya wapiga kura katika kuwawajibisha wabunge wao.

Katika nchi ambayo inajali wananchi wake na inayopinga kwa nguvu zote vitendo vya ufisadi, Chenge hakutakiwa kuonekana akidunda mtaani. Alitakiwa awe amerudisha mali zote ambazo zilipatikana kwa kutumia vibaya ofisi ya umma. Nakaa na kujiuliza, ni nani anamlinda na kwa maslahi gani? Inakuwaje anaendelea kuaminika katika masuala yanayohusu uhai wa taifa?

Inakuwa vigumu kidogo kuamini kama yuko peke yake kwenye haya mambo na kama analindwa na tunaowaamini, basi kama taifa, bado tuna safari ndefu kufikia maendeleo tunayotaka!

No comments: