Advertisements

Thursday, November 27, 2014

Emerson: Nina habari za Simba

 Mchezaji mpya wa Yanga,Emerson Oliveira Neves Roque (kulia) akiwasalimia mashabiki wa timu iyo,baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere na mchezaji mwenzake Andrey Coutinho.
 Emerson Oliveira (katikati) na Couthno (kushoto), wakipokelewa uwanja wa ndege jana mchana siku ya  Jumatano Novemba 26, 2014 

Kiungo mkabaji, Mbrazil Emerson De Oliveira Neves Rouqe amewasili nchini na kupokewa na mashabiki wachache wa Yanga kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam (JNIA) jana alasiri akitokea Brazil huku akiweka wazi kuwa amekuja kupambana.

Kiungo huyo alitua JNIA majira ya saa nane alasiri akiwa pamoja na Wabrazil wenzake, Kocha Mkuu wa Yanga, Marcio Maximo na kiungo Andrey Coutinho ambao walirejea kwao kwa ajili ya mapumziko baada ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) kusimama Novemaba 9, mwaka huu kupisha usajili wa dirisha dogo na michuano ya Kombe la Kagame iliyobuma.

Watatu hao walipokewa na Meneja wa Timu ya Yanga, Hafidh Saleh aliyekuwa amefuatana na kocha msaidizi wa timu hiyo, Mbrazil Leonardo Neiva.

Mara tu baada ya kutoka kwenye vyumba vya abiria wanaowasili vya uwanja huo saa 8:17 alasiri, Emerson alizungumza na waandishi wa habari na kuweka wazi kwamba amekuja Tanzania kwa lengo moja tu la kufanya kazi akiwa na Kikosi cha Yanga.

"Nimefurahi kuja Tanzania, nimekuja kwa lengo moja tu la kufanya kazi. Nimeambiwa kwamba soka la Tanzania kuna timu mbili kubwa, Simba na Yanga zinazolitawala. Nitapambana nikiwa na Yanga," alisema Emerson.

Kiungo huyo aliyeteka vichwa vya magazeti nchini tangu uongozi wa Yanga ulipoanika ujio wake Jumamosi, hajui Kiingereza wala Kiswahili, hivyo alizungumza Kireno huku Coutinho alitafsiri kwa Kiingereza.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, uongozi wa Yanga ulitangaza kuwa kiungo huyo atakuja nchini kwa ajili ya majaribio katika klabu hiyo na endapo atafuzu, moja kwa moja atajiunga na mabingwa mara 24 wa Tanzania Bara.

Emerson (24), ambaye kwa sasa ni mali ya Klabu ya Bonsucesso inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini kwao Brazil, msimu uliopita alikuwa akicheza soka la kulipwa nchini Poland katika Kikosi cha Piotrkow Trybunalski FC iliyopo Ligi Daraja la pili nchini humo.

Ujio wa Emerson Yanga, unakuja kutokana na mshambuliaji wa kimataifa wa timu hiyo, Mbrazil Geilson Santos Santana 'Jaja' kushindwa kurejea nchini baada ya kwenda kwao Brazil na kutoa taarifa kwamba hataweza kurejea tena nchini kutokana na matatizo ya kifamilia yanayomkabili.

Awali ilikuwa familia ya Jaja ije nchini katika kipindi cha mapumziko, lakini waliomba Jaja aende Brazil na mara baada ya kufika huko matatizo ya kifamilia aliyokutana nayo yamesababisha asirejee nchini kuitumikia klabu yake na kuomba abakie kwao kwa ajili ya kutatua matatizo hayo, hii ikiwa ni kwa mujibu wa taarifa ya mtandao rasmi wa Klabu ya Yanga, lakini hata hivyo habari za ndani zinadai kiwango kibovu ndicho kimemuonda katika klabu hiyo.

Kuondoka kwa Jaja kunafanya klabu ya Yanga kubakia na wachezaji wanne wa kigeni ambao ni Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima, Hamis Kiiza na Coutinho, hivyo Emerson ana nafasi kubwa ya kusajiliwa Jangwani endapo akifuzu majaribio na vipimo vya afya na kuifanya idadi ya wachezaji watano wa kigeni kukamilika.

MAXIMO AMWAGIA SIFA
Akizungumza na waandishi wa habari mara tu baada ya kutua JNIA jana, Maximo alimwagia sifa kiungo huyo akidai ana uzoefu mkubwa wa mechi za kimataifa na atakuwa msaada mkubwa kwa Yanga kwa vile ni mzuri wa kupandisha mashambulizi na kuilinda timu kushambuliwa.

"Kabla sijarejea Brazil, nilisema Yanga ina washamabuliaji wengi lakini inahitaji viungo wenye uzoefu na wenye nguvu. Emerson ana sifa hizo ndiyo maana nimeamua kuja naye afanye kazi. Kinachofuata atazungumza na uongozi, kisha programu nyingine zitaendelea," Maximo alisema.

"Jaja nimepata taarifa kwamba ana matatizo ya kifamilia na hataweza kuja tena Tanzania lakini bado sijapata rasmi taarifa kutoka kwake ama wakala wake."

MECHI MBILI KIMATAIFA
Aidha, kocha huyo wa zamani wa Taifa Stars alisema ameuagiza uongozi wa Yanga kuhakikisha timu yake inapata mechi mbili za kimataifa za kirafiki kabla ya kuikabili Simba katika mechi ya 'Nani Mtani Jembe 2' itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Desemba 13, mwaka huu.

Emerson, mzaliwa wa Rio de Janeiro, anatarajiwa kuanza majaribio leo, kabla ya kufanyiwa vipimo vya afya na kusajiliwa kuchukua nafasi ya Jaja, ambaye atakumbukwa kwa mabao yake mawili mazuri aliyofunga wakati Yanga ikiiadhibu Azam FC mabao 3-0 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii Septemba 14, mwaka huu.

Katika mechi 11 ambazo Jaja alipangwa katika Kikosi cha Yanga, alifunga mabao sita, moja katika mechi saba zilizopita za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na matatu katika mechi za kirafiki pamoja na mawili ya 'video' yaliyowapa Wanajangwani Ngao ya Jamii.
CHANZO: NIPASHE

No comments: