ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 28, 2015

Obama akutana na mfalme mpya wa Saudi Arabia

Rais Obama akizungumza na mfalme mpya wa Saudia, Salman bin Abdul Aziz huko Riyadh, Jan 27,2015
Rais Obama na mkewe Michelle wakiwa na mfalme Salman huko Riyadh

Rais wa Marekani, Barack Obama alisafiri kwenda Saudi Arabia jumanne kutoa heshima zake kufuatia kifo cha wiki iliyopita cha mfalme Abdullah wa nchi hiyo aliyekuwa na umri wa miaka 90.

Bwana Obama alisimama muda mfupi katika mji mkuu Riyadh, huku akiongoza ujumbe wa watu 30 ambao ulijumuisha maafisa na wabunge pamoja na maafisa waandamizi kutoka utawala wa marais waliotangulia. Akiwa mjini Riyadh, Rais Obama alikutana kwa mara ya kwanza na mfalme mpya wa Saudi Arabia, Salman bin Abdulaziz kabla ya kuondoka nchini humo.

Ofisa mmoja wa Marekani alisema viongozi hao wawili walizungumzia masuala mbali mbali ya usalama huko mashariki ya kati na uthabiti kwenye soko la mafuta. Ofisa huyo alisema bwana Obama pia aliongelea suala la haki za binadamu.

Awali msemaji wa Obama, Ben Rhodes alisema Saudi Arabia inahitaji kufanya kazi zaidi kuboresha haki za binadamu.

Kufuatia kifo cha mfalme Abdullah wiki iliyopita makundi ya haki za binadamu yalielezea historia ya Saudi Arabia ya kunyonga wafungwa, ubaguzi dhidi ya wanawake na makundi ya walio wachache na kuwazima wapinzani wa kisiasa wakati wa utawala wake wa kifalme wa miaka tisa.

Marekani, Umoja wa Mataifa na makundi ya haki za binadamu wameelezea wasi wasi kuhusu adhabu iliyotolewa na Saudi Arabia kwa mwana blog, Raif Badawi ambaye alihukumiwa viboko 1,000 baada ya kukutwa na hatia ya kuutusi uislam. Adhabu ya viboko 50 vya kwanza alipigwa hadharani mjini Jedda lakini mzunguko wa pili uliakhirishwa baada ya daktari mmoja kusema vidonda vya Badawi kutokana na mzunguko wa kwanza wa viboko havijapona.

Chanzo:VOA

No comments: