Advertisements

Saturday, February 21, 2015

ALBINO KUANDAMANA KWENDA IKULU KUPINGA VITENDO VYA MAUAJI DHIDI YAO‏

Mjumbe wa Chama cha Maalbino Tanzania, Sophia Mhando (katikati), akizungumza kwa uchungu katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa pamoja na maandamano hayo ya amani ya kwenda Ikulu. Kushoto ni Mkurugenzi wa Action on Disability & Development (ADD), Mathew Kawongo na Ofisa Habari Mahusiano ya Umma wa Chama cha Albino Tanzania Josephat Torner. 
Ofisa Habari Mahusiano ya Umma wa Chama cha Albino Tanzania Josephat Torner (kushoto), akizungumza kuhusu maandamano hayo. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Gabriel Aluga na Mtunza Hazina, Abdillah Omari. 
Wanahabari na watu wenye ulemavu wa ngozi Albino wakiwa kwenye mkutano huo.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
 
Dotto Mwaibale
CHAMA cha Albino Tanzania kimeandaa maandamano ya amani nchi nzima ikiwa ni njia mojawapo ya kulaani mauaji yanayoendelea nchini pamoja na kumlilia Rais Jakaya Kikwete kwa kile kinachodaiwa kushindwa kutokomeza mauaji ya albino.

Maandamano hayo yanayotarajiwa kufanyika tarehe 2/3/2015 ambapo yataanzia ofisi za chama hicho zilizopo Ocean road kuelekea ikulu na ikiwa ni maandamano ya tatu kufanyika tangu mwaka 2008, kipindi amabcho mauaji ya watu wenye ualbino yalizuka na kuenea kwenye mikoa mbalimbali nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Ofisa Habari Mahusiano ya Umma wa chama hicho, Josephat Torner alitoa wito kwa wazazi na mashirika ya umma na binafsi kuwaunga mkono katika maandamano hayo ili kutokomeza suala zima la mauaji ya maalbino yanayoendelea

"Zaidi ya watu 76 wameuwawa na majeruhi zaidi ya 56 na makaburi 18 kufukuliwa na watu kuachwa na ulemavu wa viungo 11 kati yao na watoto", Torner alisema

Torner aliendelea kusema kuwa analiomba jeshi la polisi kutoa kibali na ulinzi na kwamba hawapo tayari kuwa wakimbizi katika nchi yao.

Nae Mkurugenzi wa Action on Disability & Development (ADD), Mathew Kawongo alisema kuwa atakuwa mstari wa mbele na kushirikiana nao kuhakikisha suala zima la kutetea haki zao

"Aidha Kawongo alitoa wito kuwa waandishi wa habari kuwaanika hadharani wale wote wanaofanya vitendo hivyo vya ukatili kwa albino bila kujali vitisho.

Pia,Sophia Mhando mwanachama wa Umoja wa albino Tanzania aliwaomba wazazi na jamii kwa ujumla kuwa na moyo wa huruma kwa kile kinachodaiwa baadhi yao kuwa chanzo cha mauaji hayo, na pia watasubiri kwa muda wa miezi mitatu mbali na hapo watakwenda Umoja wa mataifa kwa mashitaka zaidi.

No comments: