ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 10, 2015

Chadema wamshukia Nape.

Kufuatia kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, (pichani) kudai vijana wa ‘Red Brigade’ wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanaandaliwa kijeshi kwa lengo la kufanya ugaidi, chama hicho kimeibuka na kumkemea kiongozi huyo wa chama tawala.

Akizungumza na vijana wa chama hicho mjini Tabora juzi, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, alisema mafunzo yanayotolewa kwa vijana wa chama hicho ni ya kuwajengea ukakamavu na ujasiri ili wawe wazalendo wa kweli wa nchi yao.

Mbowe alisema mafunzo ya vijana hao yatasaidia kuimarisha ulinzi na usalama katika mikutano ya chama hicho pamoja na ulinzi wa mali za chama.

“Shutuma zinazotolewa na Nape ni uoga wake tu, anataka kueneza uzushi na upotoshaji mkubwa kwa wananchi ambao wengi wao wanaelewa lengo la vijana hao wa Red Brigade,” alisema Mbowe.

Mbowe pia alisema vijana hao wameanza kupewa mafunzo hayo mapema ili kuimarisha ulinzi na usalama ndani ya chama, ikiwamo
kuwajengea ujasiri na moyo wa kizalendo kwa nchi yao tofauti na CCM ambao huwafundisha vijana wao mbinu za kijeshi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: