ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 10, 2015

MIAKA 20 BAADA YA BEIJING WANAWAKE WAMEPIGA HATUA-BAN KI MOON

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akifungua Mkutano wa 59 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hadhi ya Wanawake ( CSW), Mkutano huu wa wiki mbili ulioanza siku ya jumatatu, unafanyika ikiwa ni miaka 20 tangu kufanyika kwa mkutano wa kihistoria wa wanawake uliofanyika Beijing, China mwaka 1995. Mkutano huo uliokuwa chini ya Ukatibu Mkuu wa Dr. Gertrude Mongella, uliweka misingi mbalimbali iliyolenga katika kusimamia na kutetea haki mbalimbali za mwanamke zikiwamo za usawa wa kijinsia na uwezeshwaji.
Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akiwa na sehemu ya Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa 59 wa Kamisheni kuhusu Hadhi ya Wanawake ulioanza jana jumatatu hapa Umoja wa Mataifa
Sehemu wa washiriki wa mkutano wa 59 wa Kamisheni kuhusu Hadhi ya Wanawake wakifuatili hotuba za ufunguzi zilizotolewa na viongozi mbalimbali akiwamo Katibu Mkuu Ban Ki Moon na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Bw. Sam Kutessa

Na Mwandishi Maalum,  New York

Mkutano wa  59 wa Kamisheni  ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hadhi ya Wanawake  maarufu kama  CSW umeanza rasmi siku ya jumatatu kwa hotuba  za ufunguzi kutoka kwa  viongozi mbalimbali akiwamo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon
Mkutano huu wa wiki mbili,   unafanyika  sambamba na  maadhimisho ya  miaka 20 tangu kufanyika  mwaka 1995  huko  Beijing , China, mkutano wa kihistoria  uliowakutanisha wanawake kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Dr. Gertrude  Mongela,  ndiye aliyekuwa Katibu Mkuu wa mkutano huo wa Beijing,   uliotoka na  tamko lililoweka misingi  iliyolenga pamoja na  mambo mengine, kutetea na  kuimarisha hadhi  ya mwanamke,  usawa wa kijisia na  uwezeshwaji wa wanawake. 
Katika siku ya kwanza ya mkutano huo, wajumbe pamoja na kusikiliza hotuba za ufunguzi pia walipitisha kwa kauli moja,  Tamko la Kisiasa   linalosisitiza dhamira ya ya matokeo ya mkutano wa  kihistoria wa wanawake uliofanyika  Beijing mwaka  1995.

Akifungua mkutano huo,  Katibu Mkuu,  Ban Ki Moon,   anasema tangu kufanyika kwa mkutano wa  Beijingi miaka 20 iliyopita hali ya wanawake imeimarika katika maeneo   mengi  kama vile    kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi, upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii  pamoja na   watoto wa kike kuwa na fursa ya kupata elimu.
Hata hivyo  Mkuu huyo wa  Umoja wa Mataifa, anasema  pamoja na mafanikio hayo na mengine mengi,  bado  kasi ya  utekelezaji wa haki za wanawake na watoto wakike  unakwenda kwa kusua sua   na wakati huo huo  wanawake na watoto wa kike wakiendelea kukabiliwa na changamoto nyingi.
Anazitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na mabadiliko ya  tabia nchi,  mdororo wa uchumi, wanawake na watoto wa kike kuendelea kunyanyaswa  na kukandamizwa ,   kupoteza maisha yao wakiwa mikononi mwa makundi mbali mbali ya kihalifu au wakikimbia machafuko.
Na kwa sababu hiyo Ban Ki Moon anasema wakati Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha  miaka 20 tangu kufanyika kwa mkutano  huo wa kihistoria inatakiwa kufanya kazi  kwa karibu na kushirikiana ili kukamilisha kazi iliyoanzia Beijing.
Vilevile Akazitaka Serikali duniani kote  kushirikiana na  makundi mbalimbali ya wanawake pamoja na  Taasisi zinazotetea  haki za binadamu. Huku akikaribisha  utashi unaoonyeshwa na serikali hizo wa kufikia uwiano wa 50:50 ifikapo mwaka 2030.
 Ban Ki Moon akasisitiza kuwa  katika kipindi hiki ambacho  jumuiya  hiyo  ya kimataifa inaendelea na maandalizi ya  malengo mapya ya maendeleo baada ya 2015,  mwanamka na mtoto wa kike wanapashwa   kuwa sehemu kamili  ya  malengo hayo.
Katika mkutano huu wa 59 wa Kamisheni kuhusu Hadhi ya  Wanawake, wawakilishi wa serikali,  Asasi   za kiraia na wataalamu mbalimbali, watajadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu  utekelezaji wa  makubaliano yaliyofikiwa  Beijing, mafanikio yake na changamoto zake.

No comments: