Advertisements

Wednesday, March 4, 2015

Sofapaka yatoa siri kwa Yanga

Sofapaka FC

Dar es Salaam. Rais wa Sofapaka ya Kenya, Elii Kalekwa amesema kama Yanga inataka kuifunga Platinum FC ya Zimbabwe ni lazima ijiandae kukabiliana nao kwenye mipira ya krosi, faulo na kona.
Yanga ilikutana na kikosi cha Sofapaka kwenye Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyata ikitokea Botswana kucheza na BDF XI, huku Wakenya hao wakitokea Zimbabwe kucheza na Platinum.
Rais wa Sofapaka, Kalekwa alisema Yanga wanatakiwa kuwa makini na Platinum katika kukabiliana nao hasa katika mipira ya krosi, faulo na kona kutokana na uimara wa Wazimbabwe hao.
“Platinum ni timu nzuri yenye wachezaji warefu ambao wanajua kucheza mipira ya juu, Yanga haitakiwi kuruhusu waruke peke yao wakifanya makosa hayo watafungwa mengi,”alisema Kalekwa.
“Wanatimu nzuri na hasa wana kiungo mmoja mwenye rasta ni kama roho yao anajua kuchezesha timu, lakini nimewaambia wanatakiwa kufanya vizuri nyumbani wasisubiri ugenini kama tulivyofanya sisi,”alisema Kalekwa.
Naye kocha Sam Timbe amewataka Yanga kutofanya makosa kama ambavyo uongozi wake uliyafanya kwa kuchelewa kufika Zimbabwe.
“Platinum ni timu nzuri, lakini Sofapaka tulifanya makosa mechi ya kwanza, mchezo wa pili tukachelewa kufika Zimbabwe na tukalazimika kufika na kucheza mechi siku hiyo hiyo, lakini sijui Yanga sasa wanachezaje, lakini waambie watafute mikanda ya mechi zetu wataona kila kitu,”alisema Timbe.
Wakati huohuo: kocha wa Platinum FC, Norman Mapeza amekiri kuwa kikosi chake kinahitaji kubadilika kama kinataka kupata ushindi dhidi ya Yanga katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Kuelekea mchezo wake wake dhidi ya Yanga, kocha Mapeza amesema hakuna timu ndogo kutoka Afrika Mashariki na anategemea kupata ushindani mkubwa.
“Tumefanikiwa kumaliza vizuri raundi ya kwanza. Ilikuwa rahisi kama ilivyoonekana, lakini kuna kazi kubwa tumefanya. Kila mchezo unaokuja unatakiwa kuandaliwa tofauti.
“Najua kidogo kuhusu Yanga. Si timu ndogo na imekuwa ikishiriki katika mashindano ya CAF kila wakati, itakuwa mechi ngumu tunachotakiwa kufanya ni kujiamini wenyewe.”
“Tunatakiwa kubadilika na kucheza kwa kiwango cha juu tofauti na hivi,” alisema Mapeza.
Yanga na Platinum zitakutana katika mchezo wa kwanza kati ya Machi 13, 14 au 15 na marudiano itakuwa Aprili 3, 4 au 5.
MWANANCHI

No comments: