ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 28, 2015

YANGA YAIKOMALIA TFF

Yanga yaikomalia TFF

KLABU ya Yanga bado imeendelea kulikalia kooni Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF juu ya mabadiliko ya kanuni ya 37 ibara ya 3

KLABU ya Yanga bado imeendelea kulikalia kooni Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF juu ya mabadiliko ya kanuni ya 37 ibara ya 3 ambayo imerekebishwa Februari 8 2015 ikimruhusu mchezaji kuchagua mechi za kucheza ikiwa anatumikia kadi tatu za njano mfululizo .
Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa Yanga Jerry Muro ameiambia Goal kuwa mabadiliko hayo hayakuja wakati muafaka na kuitaka TFF isitishe mara moja matumizi ya kanuni hiyo.

“Klabu ya Yanga tunapinga mchakato na matumizi ya kanuni ya 37 ibara ya 3 kwani mchakato mzima uliopelekea mabadiliko haya na timu nyingine kuanza kuitumia bila taarifa kamili kutolewa kwa vilabu vyote na FA zote haukuwa halali na pia haukuwa na hoja ya msingi,” amesema Muro.

“Pia haukuhusisha wala kuangalia mahitaji ya wadau ambao ni timu zote ambazo zinashiriki ligi kuu ya Vodacom kwa msimu huu wa 2014/2015 kwa sababu zifuatazo, mabadiliko haya hayakutokana na mahitaji wala kuombwa na vilabu husika katika ligi na kwa maana hiyo haikuwa lazima kufanya mabadiliko, marekebisho ya kanuni za ligi hufanywa pale mahitaji yanapotokea,” Muro alisema.

“Lakini hoja ya pili, kamati ya utendaji ya shirikisho la soka nchini (TFF) imefanya maamuzi bila kuhusisha kamati zake muhimu katika kufanya mabadiliko ya kanuni, hususan kamati ya sheria na hadhi. Hii ni kanuni ambayo inahusu sheria, iweje mchakato huu uiruke kamati hii ambayo ndiyo kamati muhimu?,” Muro alihoji.

Sakata hili lilianza kushika kasi pale timu ya Simba SC ilipomchezesha mshambuliaji wake Ibrahim Ajibu kwenye mechi dhidi ya Tanzania Prisons, Hajibu alikuwa anakabiliwa na kadi tatu za njano mfululizo lakini Simba ilimtumia kwa kutumia kanuni hiyo mpya.

Kabla ya hapo Simba ilimtumia pia mchezaji wake Abdi Banda kwenye mechi dhidi ya Stand United kwa kutumia kanuni hiyohiyo.

Uongozi wa TFF ulishalitolea ufafanuzi swala hilo kwamba, kanuni hiyo ilipitishwa na bodi ya ligi na inatumika rasmi kwenye ligi inayoendelea na kusema Simba walikuwa sahihi kuwatumia wachezaji hao kwasababu walifata taratibu, kanuni na sheria.

No comments: