Mwanza. Umoja wa Watu wenye Ulemavu katika Mkoa wa Mwanza unaojulikana kwa jina la ‘Walemavu tunaweza’, umesema nchi inapaswa kuongozwa na mtu mwenye uelewa wa masuala ya gesi ili atumie nishati hiyo, kuwaletea wananchi maendeleo.
Umoja huo umeenda mbali zaidi na kumtaka aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo agombee nafasi hiyo kwa kuwa ana uwezo, hekima na utalaamu wa kutosha kuhusu masuala ya gesi na kuongoza nchi.
Mwenyekiti wa bodi ya umoja huo, Makubi Makubi alisema wamekaa chini na kutafakari kwa muda mrefu na kubaini kwamba Muhongo anaweza kuwa chaguo sahihi kwa Watanzania, kwani anaweza kutumia utaalamu wake wa gesi kuibadilisha nchi na kuifanya iwe na maendeleo endelevu
“Sisi watu wenye ulemavu Mwanza, kupitia umoja wetu, tumekaa kwa muda mrefu na kutafakari kwamba nani anaweza kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao. Tukaona mtu sahihi ambaye anaweza kuwaletea maendeleo Watanzania ni Muhongo, kwani katika utendaji wake wa kazi ana maamuzi sahihi,” alisema Makubi.
Mwenyekiti wa umoja huo, Veronica Mtiro alisema kuwa Muhongo ni mtaalamu wa gesi na kwamba kutokana na utaalamu wake anaweza kuchochea maendeleo ya taifa.
Hii ni mara ya pili wakazi wa Mwanza kumtaka Profesa Muhongo agombee urais. Hivi karibuni Wazee wa Mkoa huu nao walijitokeza kuzungumza na waandishi wa habari na kumtaka Muhongo achukue fomu ya kuwania nafasi hiyo ndani ya CCM.
MWANANCHI
1 comment:
Bora Muhongo kuliko Lowassa
Post a Comment