Advertisements

Tuesday, April 21, 2015

Zitto atoa masharti kwa Lowassa

Mwanza. Kiongozi wa Chama cha ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe amesema iwapo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa anataka kugombea urais kupitia chama hicho afuate taratibu za chama ikiwamo kutangaza mali zake.
Akiwahutubia mamia ya wakazi wa Jiji la Mwanza kwenye Viwanja vya Furahisha juzi, Zitto alisema hawezi kumzuia mtu anayetaka kujiunga ACT - Wazalendo ikiwa atafuata taratibu zilizowekwa na chama hicho.
“Naomba niwaambie Watanzania kwamba ACT siyo chama cha kumtengenezea mtu mazingira ili agombee urais, lakini kama Lowassa anataka kugombea urais kupitia huku lazima atangaze mali zake na kueleza wapi amezipata kama taratibu za chama zinavyosema,” alisema Zitto na kuongeza:
Zimekuwapo taarifa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuwa baadhi ya wagombea akiwamo Lowassa ambaye anatajwa kuwania urais kupitia CCM, wana mpango wa kutimkia ACT iwapo watakatwa majina yao katika mchujo wa wagombea.
Kwa mujibu wa habari hizo, ACT - Wazalendo imepewa fedha na Lowassa ambazo inatumia katika mikutano hiyo kumwandalia nafasi ya kuwania urais, madai ambayo pande zote zimeyakanusha.
Akizungumzia taarifa hizo kwenye mkutano huo, Zitto alisema chama chake kinaongozwa kwa kufuata taratibu na kitampokea yeyote atakayefuata taratibu hizo.
Kiongozi huyo ambaye hivi karibuni alitangaza mali na madeni yake, alisema iwapo Lowassa atataka kujiunga na chama hicho itambidi atangaze mali zake na kueleza jinsi alivyozipata, kama yeye (Zitto) alivyofanya.
Hata hivyo, akizungumzia kuhusu kauli ya Zitto, msemaji wa Lowassa, Aboubakary Liongo alisema: “Hakipo kitu kama hicho na hakitakuwapo, hatujui habari hii inatoka wapi? Mzee (Lowassa) amekuwa akitumikia CCM maisha yake yote tangu enzi za TANU … yupo na anaendelea kutumikia kifungo chake. Maisha yake yote ni mtumishi wa chama.”
Lowassa pamoja na makada wengine watano wa chama hicho walipewa adhabu ya onyo kali baada ya Kamati Kuu ya CCM kuwatia hatiani kwa kuanza kampeni za urais mapema na kukiuka maadili ya chama.
Mbali ya Lowassa, wengine waliofungiwa ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Licha ya muda wa adhabu hiyo kufikia tamati tangu Februari mwaka huu, chama hicho kilisema kinaendelea kuchunguza mienendo yao na hakijaeleza hatma yao.
Juzi, gazeti hili liliripoti kuwapo kwa mkakati wa chama hicho kukata majina ya baadhi ya wagombea wanaoaminika kuwa na makundi yanayokihatarisha, wakilengwa Lowassa na Membe ili kipitishe mgombea asiyekuwa na kundi.
Ujumbe kwa Mwigulu
Katika mkutano wake uliofurika wakazi wa Mwanza, Zitto pia alikanusha madai kwamba amemwandikia ujumbe Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba kwa njia ya barua pepe kuhusu fedha za ziara, akisema hawezi kufanya hivyo kwamba na hizo ni propaganda za kisiasa.
“Kuhusu mimi kuwasiliana na Mwigulu hizo ni propaganda za kisiasa, siwezi kufanya hivyo kwa mtu ambaye amenikuta bungeni.”
Alisema watu wanaohoji kuhusu ufadhili wa chama hicho ni vyema kwanza wakajiuliza, Chadema kabla hakijaanza kupata ruzuku nani alikuwa akikifadhili.
“Ni jambo la ajabu kuona watu wanahoji kuhusu ACT kufadhiliwa, naomba niwaambie kwamba wawaulize Chadema kabla haijaanza kupata ruzuku ilikuwa ikifadhiliwa na nani, wamulize Mbowe. ACT ni chama cha wazalendo hivyo wananchi ndiyo wanakiendesha,” alisema.
Zitto alisema kuna wanasiasa ambao ni wachanga na amewasaidia kupata ubunge lakini hivi sasa wanamtukana, lakini akasema watambue kwamba amekwepa mishale mingi na ataendelea kupambana kutetea masilahi ya wanyonge.
Alisema awali, alipokuwa akipita Ubungo, Kawe, Singida, Mwanza na majimbo mengine kufanya kampeni kuwasaidia wanasiasa wa maeneo hayo kupata ubunge, alionekana lulu lakini hivi sasa wanamsema vibaya.
“Kama mtu ni msaliti kwa nini mnamuita awasaidie kufanya kampeni, nimekwepa mishale mingi, siasa siyo chuki ni kujibu hoja, naomba niwaambie kwamba ng’ombe anaweza kutingisha mkia wake lakini mkia hauwezi kutingisha kiwiliwili chake,” alisema Zitto huku akishangiliwa.
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Anna Mughwira alisema Mkoa wa Mwanza umepewa kipaumbele na chama hicho, kwani kutakuwa na ofisi kuu ya chama baada ya Dar es Salaam.... “lakini kama tutachukua dola tumekusudia kuhakikisha makao makuu ya nchi tunayapeleka Dodoma.”
Mwananchi

No comments: