Advertisements

Wednesday, May 27, 2015

Alichoongea JK wakati akiwaaga mabalozi wa Tanzania

Rais Jakaya Kikwete akiwahutubia mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za nje wakati wa ufunguzi rasmi wa mkutano wa siku tatu ulioanza, Dar es Salaam juzi. Picha na Anthony Siame.

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amewaaga rasmi mabalozi 36 wa Tanzania katika mataifa mbalimbali akiwaeleza kuwa hatakuwa madarakani baada ya Oktoba.
Rais aliwaaga mabalozi hao jana wakati akifungua mkutano wa siku tatu utakaohitimishwa leo, ambao pamoja na mambo mengine, utajadili ‘Diplomasia ya Tanzania Kuelekea Dira ya Taifa 2025.’
“Huu ni mkutano wangu wa mwisho kuzungumza nanyi. Mmenisaidia vizuri katika kipindi chote cha utawala wangu na niwaahidi tu kuwa nitaondoka Ikulu baada ya uchaguzi mkuu ujao,” alisema Rais Kikwete.
Pamoja na kuaga, aliwaachia mambo manne ya kuzingatia ili kuifanya Tanzania iendelee kuheshimika kimataifa. Mambo hayo yanajumuisha; kuwasaidia wawekezaji wa Kitanzania kupata fursa katika nchi wanazoziwakilisha; kuwasaidia Watanzania walioko katika nchi wanakowakilisha kuunda umoja wao;  kuzishawishi asasi za kiraia za kimataifa kuja kuwekeza nchini pamoja na kutengeneza marafiki wa Taifa kwa ujumla.
Rais alieleza kuwa wakati Serikali ikitekeleza mpango wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025, tayari kuna wananchi wenye uwezo wa kiuchumi ambao wameshaanza kuwekeza katika baadhi ya nchi Afrika na hata nchi za Magharibi, hivyo ni vyema wakapewa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha azma zao.
“Niwakumbushe tu kuwa mahitaji yamebadilika nanyi pia badilikeni. Kwa sasa ni vyema vipaumbele vyenu vikawa uwezo wa kuleta mitaji nchini, kiasi cha misaada ya maendeleo mlichochangia, masoko kwa bidhaa zetu mliyoyabainisha na wawekezaji wa nje mliowashawishi kuja kuwekeza,” alisema Kikwete na kuongeza:
“Achaneni na ripoti zenu za kila mwisho wa mwezi mnazoleta za malalamiko mara eeeh wanataka mabadiliko kwenye cyber crime (Sheria ya Makosa ya Mtandaoni) au Sheria ya Takwimu. Hayo masharti wanayotoa ndiyo maana ilifikia hatua nikasema kuwa kama hatuwezi kupata mikopo bila masharti ni bora tusipewe tu.”
Rais pia aliwataka mabalozi hao kuzihoji serikali za nchi waliko juu ya mchango wao katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo athari zake zinaziathiri sana nchi zinazoendelea kama Tanzania.
Alifafanua kuwa kama jotoridi la dunia litaendelea kuongezeka upo uwezekano mkubwa ifikapo mwaka 2030 Mlima Kilimanjaro usiwe na theluji iliyopo sasa, hali itakayopunguza mvuto wake na hivyo kuathiri utalii.
Alisema: “Ukame umeongezeka… mwaka jana hatukupata mvua kabisa za vuli. Mazao yamekauka na ipo dalili kuwa kutakuwa na upungufu mkubwa wa chakula mwaka huu.”
Aliongeza kuwa aliingia madarakani nchi ikiwa haina adui na anaondoka nchi ikiwa hivyo pia na kuwakumbusha kuwa ni vyema kila mmoja akajitahidi katika hilo.
Akimkaribisha Rais kufungua mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita nchi imeshirikiana vyema na mataifa mengi ulimwenguni jambo lililowezesha kufunguliwa kwa Ubalozi wa The Hague pamoja na kufutiwa madeni na ongezeko la misaada ya maendeleo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mussa Azzan Zungu alimweleza Rais kuwa kamati yake imekuwa ikishirikiana vyema na wizara kuifanya Tanzania iendelee kuwa na uhusiano mwema wa kidiplomasia.
MWANANCHI

No comments: