ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 27, 2015

ACHA KUSHOBOKEA MAGARI!

MAISHA yana-badilika kwa kasi sana kwani kadiri siku zinavyokwenda, mapenzi yamebadilika kutoka katika upendo hadi kuwa kitu ambacho kwa mujibu, asilimia kubwa ni fedha.

Watu hawavutiki tena katika uhusiano wa kimapenzi kwa sababu ya kuthamini na kupenda , bali kwa kutazama kitu kutoka kwa anayehitaji na magari yanatajwa kuwa ulimbo mkali unaowanasa vijana wengi.

Jamii tunayoishi hivi sasa imezoea kuona wanawake wakiwa ndiyo wababaikaji au kama watoto wa mjini wanavyosema washobokaji wakubwa wa fedha au hali za wanaume wanaowataka, lakini katika miaka ya karibuni, kibao kimeonekana kugeuka na hivi sasa, siyo jambo la ajabu kumkuta kijana wa kiume akijiuza kwa shugamami!

Masistaduu wengi wanapenda wanaume wenye magari, hata kama hawana uhakika wa fedha, kwani kitu cha msingi wanajua watafanya mitoko ya kwenda huku na kule.Vijana wa kiume nao, ambao mara nyingi huwa hawana kazi, lakini wanajipenda kwa mavazi, nao wameingia katika mtego wa kuwasubiri wanawake wenye fedha, ambao huwapa magari yao wazunguke nayo mjini, ambao wamepewa jina linalowakaa sana la Mario.

Vijana wadogo akina Mario wanapoteza mwelekeo wa maisha baada ya kurubuniwa na jimama lenye gari na fedha, hivyo kuingia kichwakichwa wakisahau masomo na ndoto za maisha yao.

Siyo tu vijana wadogo, bali hata wanaume wanaojitambua nao wamejikuta wakiangukia kwa wanawake hawa kutokana na tamaa, malengo yao hutibuka na wanapokuja kushtuka, malengo yao ya muda mrefu yanakuwa yameshatoweka.

itaendelea wiki ijayo GPL

No comments: