Advertisements

Tuesday, July 7, 2015

Okwi auzwa Denmark.

Klabu ya Simba imemuuza mshambuliaji wake kutoka Uganda, Emmanuel Okwi, katika klabu ya Sonderjyske ya Ligi Kuu ya Denmark, uongozi wa klabu hiyo ya Msimbazi umesema jana.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe, alisema jana kuwa Okwi ambaye kwa sasa Mauritius kwa ajili ya fungate baada ya kufunga ndoa, ameuzwa kwa ada ya uhamisho ambayo haitajwi.

"Ndiyo tumemuuza Okwi. Haendi kufanya majaribio, tumeshamuuza rasmi. Kuanzia sasa hivi si mchezaji wa Simba," alisema Hanspoppe katika mahojiano na kituo cha radio cha jijini Dar es Salaam jana usiku.

Hanspoppe alisema badala ya Okwi, watamsajili mshambuliaji kutoka Brazil anayeenda kumfuata hivi karibuni, ambaye ametamba kwamba atakuwa ni 'kifaa'.

Kauli ya Hanspoppe ilitofautiana na alichokisema Rais wa Simba, Evans Aveva, alipozungumza na NIPASHE mapema jana alipodai kwamba Okwi anaenda kufanya majaribio ya muda wa siku 14 ambayo yataanza rasmi leo.

Aveva alisema kwamba barua ya klabu ya Sonderjyske ilieleza kwamba wanamhitaji Okwi kuanzia leo hadi Julai 22 mwaka huu kwa majaribio ambayo yatahusisha pia wachezaji kutoka nchi nyingine.

Rais huyo ambaye Juni 30 mwaka huu alitimiza mwaka mmoja wa kukaa madarakani, alisema kwamba mara baada kukamilika kwa majaribio hayo, Okwi atarejea nchini na kuungana na wenzake kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.

"Akimaliza majaribio yake atarejea na kuungana na wenzake huku akisubiri majibu kutoka katika ripoti itakayotumwa na klabu hiyo," alisema Aveva.

Aliongeza kwamba Simba imefurahishwa na nafasi aliyoipata Okwi kwa sababu inaonyesha wazi kuwa klabu hiyo ina wachezaji wenye viwango vya kucheza soka Ulaya na inamtakia kila la heri kwenye majaribio yake.

"Kupata nafasi kama hii ni habari njema, ni kitu cha kujivunia na chenye kuleta mafanikio kwa mchezaji husika," alisema Aveva.

Hata hivyo, fursa hiyo imepokewa tofauti na wanachama na mashabiki wa timu hiyo ambao wanaamini kuondoka kwa kwa mchezaji huyo anayependwa zaidi na mashabiki wa Simba kutaacha pengo kubwa na wana shaka kwamba kuna pesa yoyote ambayo klabu itapata.

"Itakuwa kama ilivyokuwa wakati ule (alipokwenda Etoile du Sahel)," alisema mdau mkubwa wa klabu hiyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.

Okwi ambaye alirejea Simba akitokea Yanga, alikuwa na mkataba na Wekundu wa Msimbazi wa Mei mwakani.
CHANZO: NIPASHE

No comments: