Advertisements

Wednesday, July 29, 2015

SAFARI YA MATUMAINI YAMFIKISHA LOWASSA CHADEMA

Yametimia! Waziri Mkuu aliyejiuzulu katika wadhifa huo, Edward Lowassa, amejiunga rasmi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinachofungamana na vyama vinavyounda vuguvugu la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Je, hadhi ya kisiasa ya Lowassa itapanda na kuzidi kufikia ndoto za utumishi wake, ama atakuwa anaanguka kiasi cha kufikia hatua ya kusahaulika kwa jamii?

Kwa namna yoyote, hatua ya Lowassa kujiunga Chadema itachagiza kazi ya mageuzi ya kisiasa hasa katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu na `kukitikisa’ Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho nguvu zake za kisiasa zinaendelea kupungua kutokana na sababu kadhaa ikiwamo kushamiri kwa vyama vingi vya siasa.

Yanayotokea baada ya Lowassa kujiunga upinzani ni mwendelezo wa mageuzi yaliyowahi kutokea mwaka 1995 hasa baada ya kufikiwa hatua kama hiyo kwa aliyekuwa Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana, Augustine Mrema.

Ingawa kuondoka kwa Mrema kutoka CCM `kuliitikisa’ nchi na kuiathiri CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo, lakini historia inaonyesha kuwapo pia aliyekuwa Waziri wa Fedha, Profesa Kighoma Ali Malima (marehemu) aliyefikia hatua kama hiyo kwa kujiondoa CCM na kujiunga na NRA, baada ya kutoteuliwa kuwa mgombea mwaka 1995, ingawa hakushiriki zaidi siasa za upinzani kutokana na kifo kilichomkuta akiwa jijini London, Uingereza.

Mbali na Mrema, ikumbukwe pia kwamba kugombea urais kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, katika kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, kulileta mageuzi mengine yaliyosababisha waliokuwa wagombea kupitia CCM, wakiwamo mawaziri waandamizi kushindwa.

Ingawa ni hivyo, ukweli ni kwamba zipo tofauti nyingi za kijamii kati ya wakati Mrema alipojiondoa CCM kujiunga National Convention for Construction and Reform – Mageuzi (NCCR-Mageuzi) na wakati huu anapoondoka Lowassa.

Miongoni mwa tofauti hizo ni kwamba Mrema `alikorofishana’ na mawaziri wenzake katika Baraza la Mawaziri kiasi cha kufukuzwa kazi na aliyekuwa Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, wakati Lowassa ‘ametoswa’ katika mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi.

Inaweza kuainishwa kwamba Mrema (kwa wakati huo) hakupata fursa pana ya kuwaunganisha wafuasi wake katika mpango wa kuondoka katika CCM, hata kama wapo waliotoka kwenye chama hicho wakamfuata NCCR-Mageuzi na baadaye Tanzania Labour Party (TLP).

Kwa upande wake, Lowassa anaondoka baada ya kuaminika kuwa na kundi kubwa la wafuasi wanaomuunga mkono ndani na nje ya CCM. Mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia CCM uliompa ushindi Mbunge wa Chato, John Magufuli, ulikuwa kielelezo cha kuwapo idadi hiyo ya watu wanaomuunga mkono Lowassa.

Kwa hali hiyo, kama Lowassa atafanikiwa kuondoka na wafuasi wake walio ndani ya CCM, wakamfuata na kujiunga Chadema ni dhahiri kwamba uhai wa CCM unaweza kuwa katika hatua za mwisho katika siasa za nchi hii.

KUKUA KWA UPINZANI
Lowassa anaondoka katika CCM akiwa na nguvu kubwa kisiasa. Lakini pia anajiunga katika upinzani ambao unazidi kupata nguvu za kisiasa hasa kupitia Ukawa.

Hatua hiyo inaweza kuibua tofauti kubwa kwa hali ya kisiasa kati ya ilivyokuwa wakati wa Mrema na sasa. Hivyo matokeo yake itakuwa ni kuzidi kuiathiri CCM.

Nguvu za upinzani katika siasa na chaguzi zimekuwa zikiongezeka kupitia viashiria kama ongezeko la kura za urais na idadi ya wabunge na madiwani wanaotokana na vyama hivyo.

Kwa mfano, Mrema alipojiunga NCCR-Mageuzi na kukiongoza chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 1995, kumbukumbu zinaonyesha kuwa kilifanikiwa kuwapa wabunge 28 wa majimbo, ukiacha wale wa viti maalum.
Yalikuwa ni mafanikio makubwa kwa chama cha upinzani upande wa Tanzania Bara, ingawa baadaye chama hicho kilikumbwa na mgogoro uliokisababisha kupoteza umaarufu wake.
Lakini kwa ujumla, upinzani ulizidi kuimarika huku Chama Cha Wananchi (CuF) kikiimarisha ngome yake visiwani Zanzibar hususani Pemba na Chadema ikiongeza uwakilishi mpana upande wa Tanzania Bara.

Kwa mfano, baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, Chadema ilipata ushindi mkubwa kwenye majimbo ya miji mikubwa kama Moshi, Iringa, Arusha, Mbeya, Mwanza na jijini Dar es Salaam, japo kutaja kwa uchache.

Lakini yapo maeneo ya vijijini kama jimbo la Mbulu lililokuwa linawakilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Philipo Marmo, akashindwa na aliyekuwa mgombea kupitia Chadema, Mustapha Akoonay.

Hivyo mazingira hayo yanayoashiria kushamiri kwa upinzani na nguvu za kisiasa za Lowassa, linaweza kuufanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kuzidi kuwa mgumu katika ngazi zote na si urais pekee kama inavyotarajiwa na wengi.

VYOMBO VYA HABARI
Uhuru wa vyombo vya habari katika kutoa taarifa kila zinapotokea ni sehemu ya nyenzo ya hamasa inayochochea kukuza shughuli za kisiasa zikiwamo zinazofanywa na wapinzani.

Mathalan, tukio la kujiondoa katika CCM kwa Lowassa na kujiunga Chadema lilitanguliwa na tangazo la mara kwa mara kupitia vituo vya runinga, hivyo kuufanya umma wa Watanzania kujiandaa kwa kushuhudia tukio hilo.

Hata hivyo, inawezekana Chadema na Ukawa wasiishie katika kutangaza ujio wa Lowassa pekee, bali kumtembeza kwenye maeneo tofauti ya nchi kwa ajili ya ‘kumtambulisha’ kwa wananchi kama inavyofanyika kwa mgombea urais kupitia CCM, John Magufuli.

Ikiwa Chadema na Ukawa vitafanikiwa kumfikisha Lowassa kwa wananchi, wakitumia mkakati kama ilivyokuwa wakati alipokuwa akitafuta wadhamini katika kuteuliwa na CCM ili awanie Urais, hali hiyo itaibua hamasa kubwa na kuvipa nguvu za kukubalika zaidi vyama vinavyofungamana katika Ukawa.

NGUVU ZA UKAWA
Jambo jingine linalochagiza mageuzi makubwa ya siasa kutokana na Lowassa kujiunga Chadema ni kuimarika kwa Ukawa.

Awali Ukawa ilifananisha na mipango iliyoshindwa mwaka 1995 na 2000 kwa upinzani kukusudia kusimamisha mgombea mmoja katika chaguzi za miaka hiyo.

Hata hivyo, ingawa hali hiyo ilitokea na kila chama kugombea kivyake, lakini mwaka huu vyama vinne, Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na CUF vilikuwa na chanzo cha kuunda umoja wao. Chanzo hicho ni msingi walioubaini katika kuunganisha nguvu za pamoja kwenye Bunge Maalum la Katiba.

Umuhimu wa umoja ulipojidhihirisha ndani na nje ya Bunge hilo, vikawa mwendelezo unaochagizwa na Lowassa kujiunga Chadema.

KUHAMA NA WAFUASI WAKE?
Hofu iliyopo Lowassa atafanikiwa kuwashawishi wafuasi wake wakiwamo waliokuwa wabunge kupitia CCM, wakitose chama hicho na kuelekeza maisha mapya ya kisiasa kwa Chadema na Ukawa?

Ikumbukwe kwamba wakati akirejesha fomu za kuomba kuteuliwa na CCM kuwa mgombea urais wake, Lowassa alisindikizwa na wenyeviti 15 wa chama hicho wakati wabunge waliokadiriwa kufikia 150 waliwahi kuripotiwa kukutana mjini Dodoma wakionyesha kumuunga mkono (Lowassa).

Wapo watumishi wengine katika halmashauri za wilaya, wakuu wa wilaya na taasisi nyingine za utumishi wa umma, waliaminika kumuunga mkono Lowassa, wakiwa pamoja na muasisi wa CCM, Mzee Kingunge-Ngombare Mwiru.

Je, makundi hayo na wengine waliokuwa pamoja na Lowassa ndani ya CCM watabaki ndani ya chama hicho ama watakuwa tayari kujitangaza katika maeneo yao siku baada ya siku, kama ilivyokuwa kwa madiwani 20 wa kata za jimbo la Monduli ambalo dalili zimeshaonyesha wazi kuwa ngome ya Chadema!

Lowassa akifanikiwa kuyashawishi makundi hayo yamfuate Chadema, bila shaka atazidi kuwa na nguvu kubwa na kukiathiri chama chake cha zamani-CCM.

Lakini kama wafuasi hao watamuacha kama ilivyokuwa kwa Mrema mwaka 1995, Lowassa atabaki na mtaji mkubwa atakaoukuta Chadema na Ukawa, na hilo halitakuwa na maana sana kwake kisiasa.

Ingawa ni hivyo, dalili zinaonyesha wazi uwezekano kwa umma kushuhudia makundi ya wafuasi wake kumfuata kutokana na hofu ya kutengwa, `kuzibwa’ midomo, kunyanyaswa ama kudhibitiwa watakapoendelea kubaki ndani ya CCM.

CCM INAVYOWEZA KUMDHIBITI LOWASSA
Mrema alipoihama CCM palikuwa na matumizi makubwa ya vyombo vya dola hasa polisi kumdhibiti, ikiwamo kuisambaratisha mikutano yake kwa mabomu ya machozi.

Kutokana na mabadiliko kadhaa yaliyotokea tangu 1995 hadi sasa, njia hiyo haitakuwa muafaka kwa CCM na serikali kumdhibiti Lowassa, badala yake chama hicho kinaweza kuhakikisha wanachama waliokuwa watiifu (kwa Lowassa)na ambao wameonyesha nia ya kuwania ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na udiwani, wanapata fursa hizo.

Kama hali hiyo itatokea, CCM inaweza kudhibiti wimbi la wanachama wake wanaomtii Lowassa kumfuata katika Chadema, ingawa swali litabaki kuwa ni kwa namna gani hata wakibaki ndani ya CCM watajiweka kando na ‘siasa za Lowassa’?

Kwa vile hali ya kisiasa imeanza kubadilika sasa, ni wajibu wa umma kufuatilia ili utakapofika Uchaguzi Mkuu, kila mpiga kura afanye uamuzi ulio sahihi.
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

Mimi sielewi ujinga wa hali gani Chadema, CUF, na vyama vingine viunavyounda UKAWA wanao. How on Earth baada ya kazi ngumu waliyoifanya kwa miaka mingi kuvijenga vyama vyao, now all of a sudden wana-surrender na kumpa nafasi muasi ambaye amekataliwa na kupondwa na CCM, chama ambacho kilikuwa kinampa posho yake? Tunajua wazungu wanayo nahau isemayo "One man's TRASH is another man's TREASURE" but Why are Ukawa leaders brainwashed by a stranger? Honestly, najua akina Dr.Slaa na Prof. Lipumba roho zao zinawakera na wanaumia kimya kimya. Wanajua wamewekwa chini na huyu jamaa Lowasa huku akiwakanyaga na viatu vyake, licha ya wao kuvijenga vyama vyao kwa jasho kubwa. Slaa na Lipumba were the shining stars of Ukawa, and their demise at the hands of Lowasa should be unforgivable and unforgettable. I feel your pain Dr. Slaa and Prof. Lipumba, maybe you should rethink about your future with Ukawa. Lowasa has diminished your political muscles and recognition. Hypothetically, what will happen to your status and prestige should Lowasa under Ukawa flag, loose the election? Be mindful that, Dr. Magufuli will launch a fierce election campaign, and he is a fighter, as demonstrated by his work ethics and diligence. Have Ukawa leaders thought about the aftermath of a defeat? Do you think Lowasa will stay with ukawa, once Magufuli hand him a beating? Heck NO! the guy will probably RETURN to CCM or retire. RETHINK YOUR DECISION UKAWA LEADERS, YOU HAVE MISLED YOUR FOLLOWERS, IT IS NOT TOO LATE TO REVERSE AND SALVAGE YOUR UNITY, OTHERWISE THIS WILL FOREVER HAUNT YOUR POLITICAL CAREERS!

Anonymous said...

This is the only way to get ccm out of the way. Cmm is the first enemy, and then we will come back to the table once the enemy is defeated