Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Idris Kikula akimkabidhi Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi nakala ya kitambu kinachoelezea kwa kina historia ya Chuo Kikuu cha Dodoma. Katika Maelezo yake, Prof. Kikula amesema UDOM imeamua kuweka katika maandishi historia nzima ya Chuo hili ili kuepusha upotoshaji na upindishaji wa ukweli na kwamba UDOM inapanga kumuenzi Mhe. Rais Jakaya Kikwete ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuanzishwa na hatimaye ujenzi wa UDOM. wengine katika picha kutoka kushoto ni Naibu Mkuu wa Chuo Prof. Shaaban Mlacha anayesimamia masuala ya mipango, fedha na utawala, Naibu Mwakilishi wa Kudumu Balozi Ramadhan Mwinyi na Bi. Christina Silvester, Katibu wa Baraza.
Makamu Mkuu wa UDOM Prof. Kikula akimkabidhi nakala ya kitambu cha historia ya UDOM, Prof. Estomih Mtui, M.D anayefanya kazi Weill Cornel Medical Collage, Prof. Mtui ni moja kati ya wana-Diaspora ambaye amekuwa kiungo kikubwa katika utafutaji na upatikanaji wa vifaa tiba ,vitabu na wataalam wa fani mbalimbali kwaajili ya kusaidia nchini Tanzania. baadhi ya vifaa na vitabu ambavyo Ujumbe wa Makamu Mkuu wa UDOM wamevikagua vimepatikana kwa juhudi za Prof. Mtui
Na Mwandishi Maalum, New York
Chuo Kikuu cha Dodoma ( UDOM), kinatarajia kufanya hafla
ya aina yake ya kumuenzi Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kama sehemu ya kutambua
mchango wake wa hali na mali uliopelekea kuanzishwa kwa Chuo Kikuu hicho
cha aina yake Tanzania na nje ya Tanzania.
Taarifa ya kusudio la
Chuo hicho kumuenzi Mh. Rais Kikwete imetolewa mwishoni mwa wiki na Makamu
Mkuu wa UDOM, Prof. Idris Kikula wakati
alipokutana na kufanya mazungumzo na
Mabalozi na Maafisa wa Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Profesa Kikula na
ujumbe wake yuko katika ziara ya kikazi nchini Marekani, ziara iliyomfikisha Jijini New York, ambapo ujumbe ulipata fursa ya kukagua vifaa tiba
na vitabu vya kiada na ziada ambavyo
vimetolewa na wadau mbalimbali wenye
mapenzi mema na Tanzania.
Baada ya kukagua vifaa na vitabu hivyo na kijiridhisha, Makamu Mkuu wa UDOM ameushukuru Uwakilishi wa
Kudumu wa Tanzania kwa kuwapatia fursa hiyo ya kujionea wenyewe aina ya vifaa tiba na vitabu ambayo
amesema vitakuwa msaada mkubwa kwa Kitivo cha Sayansi ya Afya cha Chuo hicho.
“Waheshimiwa Mabalozi, mimi na ujumbe wangu napenda kwa moyo
wa dhati kabisa kutoa shukrani zetu kwa
kutuonyesha vifaa na vitabu ambavyo kupitia kwenu wafadhili wamevitoa
kuwasaidia watanzania nanyi mkaona bora
kutushirikisha na kuona namba gani Chuo
chetu kinaweza kunufaika na misaada ya aina hii” akasema Pofesa Kikula
Na kuongeza kwamba Kitivo cha Sayansi ya Afya
na ambacho pia kina Zahanati kinahitaji sana misaada ya kila aina ili kiweze kutimiza lengo lake kuu
la kuwaandaa madaktari na wataalam
mbalimbali lakini pia kutoa huduma
uchunguzi na matibabu siyo tu kwa
wanafunzi na wafanyakazi wa UDOM bali pia kwa watanzania wote.
“ Uongozi wangu unapenda kutambua juhudi
zenu hizi za kushirikiana na wadau mbalimbali kusaidia
siyo tu vyuo vikuu vyetu lakini na watanzania.Mmedhihirisha kwa kwa vitendo na si maneno na hii imetupa faraja sana na kudhihirisha namna
gani tunaweza kushirikiana kwa karibu Zaidi.
Akasema kuanzishwa
kwa Chuo Kikuu cha Dodoma ni
ndoto na hatimaye mbegu iliyopandwa na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete , ndoto uliyoanzia kwenye kampeni yake ya urais mwaka 2005.
“ilianza kama ahadi ya kampeni, ahadi ambayo haikuishia
katika maneno matupu ya ahadi bali aliitekeleza ahadi ile na leo hii tunaiona
mbegu aliyoipanda ikichanua na mavuno yanaonekana”. Akasema Prof.Kikula
kwa msisitizo wa aina yake.
Anasema haikuwa rahisi
kuifanikisiha ndoto ile ya Rais kutokana na pingamizi mbalimbali kutoka nje na ndani ya serikali.
Anaongeza kuwa shauku ya ujenzi na hatimaye uwepo wa UDOM
haukuishia kwa watanzania tu bali hata
baadhi ya Mabalozi wanaoziwakilisha nchi
zao nchini Tanzania ambazo walikuwa
wakimfuata na kutaka kujua tajiri ngani aliyekuwa anafadhiri mradi huu
mkubwa.
Profesa anasema mara zote alikuwa akiwajibu Mabalozi hao kuwa
mradi ule ulikuwa ukijengwa na kufadhiliwa na watanzania wenyewe na serikali
yao.
“Nisema kwamba haikuwa kazi rahisi, tulipata wakati mgumu
na pingamizi hata kutoka ndani ya serikali. Wapo
baadhi ya viongozi ambao hawakutaka
Chuo Kikuu hiki kijengwe Dodoma.
Mimi binafsi nilimuuliza Mhe. Rais kwa nini alikuwa
anataka Chuo Kijengwe Dodoma.
Mhe. Rais alinijibu. “Ninataka kijengwe
Dodoma na si kwingine, kwa sababu kwanza, ya umaskini wa Mkoa wa Dodoma na pili Dodoma ni Makao Makuu
ya Nchi”.
Profesa Kikula
anaeleza kuwa Mhe. Kikwete aliamini kwamba kwa kujenga chuo Kikuu
chenye ukubwa na uwezo wa kudahili
wanafunzi wengi Zaidi, pamoja na
kuongeza udahili wa wanafunzi wengi na kuwapa fursa vijana wengi wa kitanzania kupata elimu ya
juu, lakini pia kungefungua milango ya
kiuchumi na maendeleo ya kijamii,
na hivyo kuwapunguzia umaskini
wananchi wa Mkoa wa Dodoma.
Kwa mijibu wa Makamu Mkuu wa UDOM anasema, maono hayo ya Rais
ya kuongeza udahili wa wanafunzi na kufungua
milango ya uchumi na kupunguza umaskini
kwa wakazi wa mkoa wa Dodoma
yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Ni kwa sababu hiyo, Profesa Kikula anasema, watanzania
hawanabudi kujivunia mafanikio
yanayotokana na utekelezaji wa ahadi na vipambaumbele vinavyowekwa na
serikali yao.
“watanzania ni vema tukajijengea utamaduni wa kujivunia
mafanikio yetu, penye ukweli lazima tusema,
sisi wa Chuo Kikuu cha Dodoma
tuna kila sababu ya kujivunia mafanikio
ya Chuo hiki, na ndio maana
tumeandika kijitabu kinachoelezea
historia ya UDOM na mchango
mkubwa wa Mhe. Rais. tumeweka kwa maandishi
ili kuepusha upindishwaji ukweli na
upotoshaji wa historia ya UDOM”.
Akasema kuwa tayari kijitabu hicho amekabidhiwa Mkuu wa Chuo
Kikuu cha Dodoma Rais Mstaafu wa awamu
ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa kwaajili ya hatua za kuangalia taratibu za kumuenzi Mhe. Rais Jakaya Mrisho
Kikwete.
Kwa upande wake, Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wakudumu wa Tanzania katika Umoja
wa Mataifa, ameushuku uongoziwa UDOM kwa kuitikia wito wa
Uwakilishi wa kutumia ziara yao
ya kikazi, kujionea kukagua vifaa na
vitabu ambavyo vimepatika kwa
ushirikiano wa Uwakilishi na wadau
mbalimbali.
Akasema kuwa Uwakilishi utaendelea na juhudi za kutafuta wadau wanaoweza kusaidia katika maeneo mbalimbali, kutokana kwamba wapo watu wanaopenda
sana kuisaidia Tanzania, akasisitiza haja na umuhimu waufuatiliaji na wepesi wa
kujibu barua au mapendekezo Uwakilishi
unapeleka kwa Taasisi mbalimbali
zikiwa Vyuo vya elimu ya Juu.
No comments:
Post a Comment