Muasisi wa Tanu na baadaye CCM, Mzee Peter Kisumo
(pichani) amefariki dunia. Mwanasiasa huyo mkongwe nchini ambaye aliwahi kushika
nyadhifa kadhaa katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, alifariki Dunia jana saa
moja usiku katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mtoto wa marehemu, Michael Kisumo alilithibitishia juu ya kifo cha baba yake akisema kilitokana na maradhi ya figo
ambayo yamekuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.
“Tulikuja hapa Muhimbili kwa ajili ya mzee kufanyiwa
dialysis (usafishaji damu katika figo) sasa ikajitokeza complication (utata)
akaanza kuharisha damu,” alisema.
Michael alisema baba yake alilazwa wodi ya kawaida juzi
ili jana apatiwe tiba hiyo kabla ya hali yake kubadilika ghafla.
“Daktari wake alipokuja leo (jana) na kumwangalia aliagiza
atolewe wodi ya kawaida ahamishiwe ICU lakini ilipofika saa moja usiku
akatutoka” alisema Michael.
Kifo cha mwanasiasa huyo kimekuja takribani mwezi mmoja
tangu arejee kutoka India ambako amekuwa akienda mara kwa mara kuchunguzwa afya
yake. Hali ya ugonjwa wake huo ilifikia katika kiwango cha juu
na kulazimika kufanyiwa uchujaji wa figo mara tatu kwa wiki kila Jumatatu,
Jumatano na Ijumaa.
Kisumo aliwahi kuwa mmoja wa mameneja wa kampeni wa Rais
Jakaya Kikwete mwaka 2005 akisimamia kanda ya kaskazini iliyojumuisha mikoa ya
Kilimanjaro, Arusha na Tanga. Mbali ya kuwa waziri, aliwahi pia kuwa mkuu wa mkoa na
mdhamini wa CCM.

1 comment:
RIP Muasisi
Post a Comment