By Shaban Lupimo, Mwananchi
Makete. Haitashangaza kusikia wakazi wa kata fulani hawajawahi kuona lami tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961 kwani katika hali ya kawaida kunakuwapo miundombinu ya barabara ambayo hata kama si kwa kiwango cha kuridhisha, magari yanafika kila kukicha.
Hata kama hayafiki kila siku, lakini wananchi wana uwezo wa kutumia usafiri mwingine kama pikipiki, baiskeli na mikokoteni kuwahi shughuli zao na kusafirisha bidhaa mbalimbali na kujenga uchumi.
Hata hivyo, hali ni tofauti kwa Kata ya Kigulu, Wilaya ya Makete mkoani Njombe kwani wakazi wake wanaishi katika adha kubwa ya kutokuwa na barabara tangu nchi hii ipate uhuru, hivyo hakuna gari, pikipiki, wala mkokoteni unaoweza kufika katika kata hiyo.
Ndivyo hali ilivyo Miaka 54 ya Uhuru watoto waliozaliwa na kukulia katika kata hiyo yenye kijiji kimoja na vitongoji vinne hawajawahi kuona gari wala chombo chochote cha usafiri kijijini hapo. Hakuna gari wala pikipiki iliyowahi kufika Kugulu.
Maisha ya wananchi wa eneo hilo yanaweza kulinganishwa na yale ya enzi za ujima, ambayo wengi wetu tumeyasoma vitabuni.
Wanaishi wakitegemea nguvu za miili yao kusafirishia mizigo mbalimbali kutoka na kuingia kijijini hapo wakisafirisha mazao na bidhaa nyingine wanazonunua wilaya jirani ya Rungwe.
Kijiografia, kata hiyo imekaa kama kisiwa, kwani pande zote imezungukwa na safu za milima ya Livingstone na Mto Lufirio.
Kutokana na ukweli huo, ili kuweza kufika katika Kata ya Kigulu wananchi hulazimika kutembea umbali wa takribani kilomita 30 kwenda na kurudi, wakitokea vijiji vya Mbigili na Isange vilivyopo Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, ambako ndiko ilipoishia barabara.
Kwa hali hiyo, wakazi wa kata hiyo hulazimika kutembea umbali wa kilomita 30 kufuata huduma mbalimbali za kijamii katika vijiji hivyo vya Mbigili na Isange, ikiwemo bidhaa za madukani na huduma za usafiri ili kwenda maeneo mengine ya nchi.
Wananchi hao hulazimika kutembea kwa kupanda milima yenye miteremko mikali na madaraja yenye kutia hofu yaliyojengwa kwa mbao na mengine miti ya mianzi.
Hakika kama si mjasiri na mara yako ya kwanza kufika maeneo hayo, unaweza kuahirisha safari yako katika kata hiyo kwa hofu ya kuanguka mtoni au unaweza kufika katikati ya daraja na kuogopa kwenda mbele wala kurudi nyuma kwa jinsi yanavyonesa wakati wa kupita huku yakiwa yamechakaa.
Lakini jambo la kushangaza, wakazi wa kata hiyo hawahofii hali hiyo, kwani wamezoea mazingira hayo ambayo ni sehemu ya maisha yao ya kila siku miaka nenda rudi.
Ukifika Kugulu utawaona wakipanda na kushuka huku wakiwa wamebeba vitu vizito kama vile saruji, mabati na bidhaa nyingine muhimu kupitia madaraja hayo.
Wakizungumza na gazeti hili kijijini hapo, wakazi hao wanasema kuwa kilio chao kikubwa ni kuona Serikali ikiwajengea barabara ili waweze kuondokana na adha ya kushuka na kupanda milima na mizigo kichwani.
“Kilio chetu kikubwa hapa barabara. Hospitali tunayotegemea ni zahanati, sasa kama mgonjwa akizidiwa tutamwahisha wapi? …Hakuna uwezekano wa kumbeba kwenye chombo chochote cha usafiri zaidi ya machela na jiografia yetu ilivyo mpaka kuvuka ng’ambo, mtu anaweza kuzidiwa na kufia njiani,” anasema Wangomu Wamanga.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kigulu, Charles Mwaihola anasema yeye ni mtumishi wa muda mrefu katika kata hiyo na kwamba changamoto kubwa anayokutana nayo ni watumishi wa Serikali kushindwa kuripoti kwenye kata hiyo kutokana na mazingira magumu, hivyo wengi huwa tayari kuacha kazi lakini siyo kuishi katika mazingira hayo.
“Watumishi wa Serikali waliopo hapa ni wachache, wengi wanaopangwa kuja kufanya kazi Kata ya Kigulu hushindwa kuripoti kutokana na jiografia ilivyo na mazingira ya kazi yalivyo magumu,” anasema Mwaihola.
Anasema hata ujenzi wa shule unakuwa mgumu kwani wananchi hulazimika kujitolea kubeba vifaa vyote vya ujenzi kichwani wakati mwingine wakisaidiwa na wanafunzi.
“Kama unavyoona hapa tuna ujenzi wa vyoo na nyumba za walimu, mifuko ya saruji tulisomba kichwani kutoka Mbigili, ilinibidi nichukue hata wanafunzi kuifuata. Barabara ikijengwa tutapumzika sana na huduma nyingine kupatikana itakuwa rahisi, maana hata mgonjwa huku akizidiwa tunabeba kwenye machela,” anasema.
Naye Muuguzi wa Zahanati ya Kigulu, Sylivesta Msemwa anasema: “Huku tunaishi katika ukanda wa hatari, maana hata Serikali ikitoa vifaa tiba, tatizo linakuja kwenye kusafisha hadi kuvifikisha hapa, naona changamoto kubwa hapa ni barabara.”
Diwani wa zamani wa kata hiyo, Hebron Kujungu anasema: “Huku bado tuko katika enzi za ujima, maisha ya huku ni magumu sana, wakati nilipokuwa diwani kilio changu katika vikao vya Baraza la Madiwani kilikuwa kuomba tujengewe barabara, hilo likifanikiwa nadhani ndiyo itakuwa faraja yetu.”
Anasema hata daraja wanalotumia sasa kuvusha vitu vizito katika Mto Lufirio limejengwa kwa msaada wa misheni ya Mano iliyoko wilayani Rungwe na kwamba madaraja mengine yote yamejengwa na wananchi kwa miti aina ya mianzi na kwamba mgeni hawezi kuvuka kutumia madaraja hayo kwa hofu ya kutumbukia mtoni.
Kajungu anasema kwa sasa wanasubiri ahadi ya kujengewa barabara iliyotolewa ya mbunge wa jimbo lao la Makete, Dk Binilith Mahenge ambaye pia ni Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira.
Mtendaji wa Kata hiyo ya Kigulu, Suleman Mwakajumilo anasema ujenzi wa barabara katika kata hiyo upo kwenye mpango wa Serikali akieleza kuwa kwa sasa wameanza kujenga madaraja kwa ufadhili wa mfuko wa Tasaf, huku halmashauri ikiahidi kupeleka greda kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.
Kwa upande wake, Dk Binilith Mahenge anasema kuwa Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Makete imeanza ujenzi wa miundombinu ya barabara katika kata hiyo ili kuwaondolea wananchi adha ya kubeba mizigo mizito kichwani kwa umbali mrefu.
Anaeleza kutambua umuhimu wa kata hiyo hasa katika uzalishaji wa mazao akibainisha kwamba miamba imeanza kupasuliwa na kujenga daraja kwa Sh 100 milioni wakisaidiwa na nguvu za wananchi wanaojitolea.
“Wabunge waliotangulia walitaka kata hii ipelekwe Wilaya ya Rungwe upande wa Mbeya, lakini nilipokuja mimi tukaona haina haja kwa sababu hata ikienda Rungwe, bado ujenzi wa barabara uko pale pale. Kwa hiyo mwaka huu kwa kushirikiana na wananchi tumepasua miamba kwa baruti kutumia fedha za Mfuko wa Jimbo, pia tumeshajenga daraja kwa Sh 100 milioni za halmashauri,”anasema.
Anaongeza: “Kazi iliyopo kwa sasa ni halmashauri kupeleka greda kusawazisha, maana mwelekeo wa barabara tayari upo. Ninachoweza kukuthibitishia ni kwamba hadi mwishoni mwa mwaka huu magari yataanza kufika Kigulu.”
Inaelezwa kuwa kihistoria, Kata ya Kigulu inatokana na wananchi waliokuwa wakikwepa kodi katika Kijiji cha Isange, Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya.
Kwa mujibu wa diwani wa zamami wa kata hiyo, Hebron Kujungu kabla ya wananchi hao kuanza kuhamia eneo hilo, awali lilikuwa halikaliwi na binadamu lakini wakati wa utozaji kodi, baadhi ya wakazi wa Isange waliamua kukimbilia eneo hilo ambalo ni vigumu kwa mtu mgeni kufika na waliokimbilia huko waliona ni sehemu salama wanayoweza kuishi bila tatizo kutoka kwa watoza kodi.
“Ilikuwa vigumu kwa mtu kuvuka mto huu na kushuka milima hii, ndiyo maana wakazi wa Isange walikimbia kujificha huku,” anasema Kujungu.
Anasema baada ya watu kuongezeka na kutengeneza makazi, chifu wa zamani wa Isange, aliyemtaja kwa jina la Mwalugaja alimteua mtoto wake aitwaye Mwamatebe kwenda kuwa kiongozi wa eneo la Kigulu.
Anasema kijiji hicho kilihamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya na kupelekwa Wilaya ya Njombe wakati huo kabla ya Makete kuwa wilaya na Njombe ikiwa sehemu ya Mkoa wa Iringa, baada ya watoza kodi wa Rungwe kushindwa kuwakamata na kuwatoza kodi kufuatia ugumu wa kuwafikia wananchi hao na kuiomba Serikali Mkoa wa Iringa iwasaidie.
Kajungu anaeleza kuwa, Mkoa wa Iringa kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Njombe wakati huo, walifanikiwa kuwatoza kodi wananchi hao kupitia Kata ya Ipelele, ambapo watoza kodi walilazimika kutembea kwa zaidi ya sita hadi kufika kijijini hapo kutoza kodi.
Anasema kuwa kutokana na hali hiyo, hata baada ya kuanzishwa Wilaya ya Makete eneo hilo lilibaki kuwa sehemu ya wilaya hiyo kutokana na historia hiyo, licha ya kuwa kijiografia, tabia na mila na desturi, hata ukaribu wa kupata huduma walistahili kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya.
5 comments:
Asante hao ndio CCM wenyewe walewale!! Kampeni za CCM zinasema wataweka umeme vijiji vyote baada ya miaka 2.!!!!!!!. Hapa unatuambia hawajawahi kuwa na barabara tangu uhuru 1961!! Na maisha hata wafanyakazi wakipangiwa inakuwa vigumu maGeographia hayako!! Je Mh. JPM na Makamu huyo umeme atafikaje mahali hapa na hii ni moja vikonvingi mno havina huduma muhimu!! Au hizo nguzo mtawaambia wananchi wakabebe kichwani. Kwa minajili hii basi hata nyumba nora ndio hakuna!! Kweli miaka 50 ya uhuru CCM mmetuwezesha!! Ahadi nyingi kwenye kampeni hebu ziacheni kwani hamna mabadiliko ndani ya wenyewe walewale. Mabadiliko yakonupande mwingine wa shilingi.!!
Inaumaaa!!! Heri kufa kuliko ccm tena!!
Acha kebehi we mdau hapo juu. Huyu Lowasa ambaye Ukawa mnamwabudu si ndo alikuwa Waziri Mkuu chini ya CCM? Jee? alifanya nini Enzi za Uwaziri wake Mkuu kuwakomboa wananchi wa Makete? Eti leo mnamtaka awe Rais? Thubutuu, hatutamruhusu!
Ikifika tarehe 24/ 10/2015 uwe umeshaamua ni namna gani ungependa UFE ,ili usishuhudie yatakayotokea tarehe 25/10
Uwe unakunywa chai kwanza kabla hujaingia mtandaoni.Hueleweki...
Post a Comment