ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 8, 2015

Sababu 10 kwa nini John Magufuli atashinda uchaguzi Mkuu wa Urais 2015


Uchaguzi Mkuu

1. Tanzania bara na visiwani yako majimbo ya uchaguzi 266, CCM imesimamisha wagombea Ubunge katika majimbo yote 266 huku Chadema na washirika wake wa Ukawa wakiwa wamesimamisha wagombea katika majimbo 211 (138 toka Chadema). Kati ya majimbo hayo 266, CCM tayari imepita bila kupingwa majimbo 7. Ukichukua majimbo 259 yaliyobaki na kutoa 211 ambayo Chadema na washirika wake wamesimamisha wagombea unabaki na majimbo 48 ambayo CCM haina upinzani wa Chadema wala washirika wake wa Ukawa. Majimbo haya 48 CCM ina uhakika wa kushinda walau kwa asilimia 90, ushindi huu si kwa Wabunge tu bali pia kwa mgombea Urais wa CCM.
2. Watanzania waliojiandikisha kupiga kura mwaka 2015 ni milioni 24.2. Takwimu zinaonyesha CCM ina wanachama hai wapatao milioni 8 wenye kadi na wanaolipia ada zao za uanachama kila mwaka. Kuondoka kwa Edward Lowassa katika Chama Cha Mapinduzi kunamaanisha Magufuli hatapata kura zote milioni 8 za wana CCM na pia kihesabu si rahisi wana CCM wote milioni 8 kujitokeza siku ya kupiga kura. Utafiti unaonyesha kwamba wana CCM watakaopiga kura hawatazidi asilimia 90 ya wanachama wake (milioni 7.2) huku milioni 7 kati yao wakimpigia kura John Magufuli. Historia ya CCM inaonyesha ni wanachama wachache sana humpigia kura kada mwenzao anapohama kugombea nafasi kwa chama kingine, hasa nafasi ya Urais (Rejea: Uchaguzi wa Urais 1995, mgawanyo wa kura za Augustine Lyatonga Mrema)

3. Mizunguko ya kampeni huzaa kura za ziada mbali na zile za wanachama. Tayari inaonyesha kwamba Magufuli anapita karibu kila kata ya Tanzania akitumia barabara huku upande wa Lowassa na shirikisho la Ukawa hali ikiwa tofauti, ambako amekuwa akifika sehemu chache akitumia usafiri wa ndege na helkopta na ni wazi hana stamina ya kuzunguka kwa gari nchi nzima kutokana na tatizo la kiafya. CCM ina mizizi kwenye mashina kuanzia ngazi ya nyumba kumi. Mtandao huu wa Chama pamoja na safari za mgombea wao kila kata ni kiashiria kwamba atafikia wapiga kura wengi zaidi hasa sehemu za vijijini na ambazo si rahisi kufikika. Tafiti zinaonyesha huko ndiko kwenye wapiga kura wengi na kuwafikia ni hatua moja kuelekea kuzipata kura zao na kushinda.

4. Chaguzi za Serikali za Mitaa mwaka 2014 zinaonyesha kwamba CCM ilishinda kwa zaidi ya asilimia 80 kwenye nafasi za uongozi za serikali za vijiji na mitaa. Ikumbukwe kwamba CCM ilipata ushindi huu licha ya ushindani mkubwa uliokolezwa na sakata la Escrow wakati huo. Hii inaonyesha kwamba CCM iliweza kushinda hata wakati huo wa changamoto. Ni mwaka mmoja tu umepita tangu chaguzi hizo zifanyike. Kitafiti, hiki ni kiashiria kikubwa kwamba katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, CCM kama chama kinaenda kwenye sanduku la wapiga kura kikiwa na rekodi nzuri kuweza kushinda.

5. Rekodi ya Utendaji ya Magufuli inavutia Watanzania wengi. Utafiti unaonyesha kwamba wapinzani wake majukwaani mpaka sasa wanapata wakati mgumu kutaja jina lake moja kwa moja kumuhusisha na utendaji wa hovyo. Mitandaoni zipo video na nukuu nyingi zikiwemo za Mgombea wa Ukawa Edward Lowassa, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wengineo wakisifia utendaji wa Magufuli. Katika siasa na kampeni, hatua moja kuonyesha mgombea anashinda ni kushindwa kwa wapinzani wake kumnyooshea kidole moja kwa moja au kukosa mabaya ya kusema dhidi yake. Asiye na la kukusema vibaya anawapa wananchi nafasi ya kuona mazuri yako na kushinda.

6. Suala la afya ya wagombea limekuwa gumzo kubwa katika uchaguzi wa mwaka huu. Huku ikiwa wazi kwamba Mgombea wa Ukawa Edward Lowassa anaugua ugonjwa wa Parkinson’s kwa muda mrefu sasa, Magufuli hajawa na changamoto ya afya. Ugonjwa wa Parkinson’s alio nao Edward Lowassa unaathiri ubongo wa kati, moyo, mishipa ya fahamu na uwezo wa kufikiri (Afya ya mwili maeneo hayo ni muhimu kiongozi kuwa nayo). Kwa muda mrefu Lowassa amekuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa huu katika hospitali maarufu ya Franziskus-Krankenhus mtaa wa Budapester jijini Berlin, Ujerumani. Kiumri Magufuli ana miaka 55 huku Lowassa akiwa na miaka 63. Wapiga kura huchagua kiongozi kwa kutazama muonekano na ni wazi kabisa kwamba kwa muonekano na hali ya kiafya ya Lowassa ni dhoofu na inazidi kudorora siku hadi siku na kuwakatisha tamaa hata wanaomuunga mkono. Tangu kampeni zianze hakuna mahala ambapo amewahi kuzungumza kwa zaidi ya dakika 15. Hivyo basi, kwa kadiri siku zinavyoenda Watanzania watazidi kubaini kwamba Lowassa hana afya ya kuhimili vishindo vya kampeni wala uwezo wa kumudu majukumu ya Urais.

7. Nguvu ya vyama, oganaizesheni na ilani. Magufuli anatokea CCM ambayo kama nilivyoeleza juu ina nguvu ya kuwepo kila kijiji na kila nyumba kumi Tanzania; imetoa marais waliotangulia, na hata wapinzani wametoka katika CCM hiyo hiyo baada ya kukosa nafasi za kugombea kupitia chama hicho. Kwa miaka mitatu iliyopita Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amezunguka kila kona ya nchi akikinadi chama chake, hii ni aina ya kampeni ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Kwa upande wa upinzani hali iko tofauti. Mgombea wao, Lowassa alikuwa mwanachama wa CCM miezi miwili iliyopita, kuingia kwake Chadema kumeleta mpasuko huku Katibu Mkuu wake akitokomea kusikojulikana, na Mwenyekiti wa CUF, Lipumba naye akijiuzulu uongozi kupinga Lowassa kukaribishwa Ukawa. Hii inaonyesha hali si shwari katika upinzani. Kwa sasa Ukawa wanaficha mpasuko huo kwa propaganda lakini madhara yatajitokeza kabla ya siku ya uchaguzi. Moja ya viashiria vya mpasuko katika Ukawa ni kuvunjika kwa makubaliano ya kuweka mgombea mmoja wa Ubunge katika kila jimbo. Zaidi ya asilimia 70 ya majimbo yana wagombea Ubunge toka vyama vyote vinavyounda Ukawa. Kwa mfano Lowassa, kama mgombea Urais wa Ukawa, akienda Ubungo ambapo kuna wagombea toka Chadema, CUF na NCCR atamnadi mgombea yupi?

8. Kuondoka kwa Dr Slaa Chadema, tuhuma za Mbowe kuiuza Chadema kwa Lowassa kwa TZS bilioni 10 (ambazo Dr Slaa amezithibitisha) na ukawa kuhama kutoka kumuita Edward Lowassa fisadi mkuu wa nchi miaka michache iliyopita hadi sasa kumfanya kuwa mgombea wao. Hii imewakanganya Watanzania wengi na wote wanaochukua muda kulitafakari wanazidi kupata maswali zaidi. Uamuzi wa mpigakura katika hali kama hii ni kuendelea kulipigia kura zimwi alijualo (CCM) kuliko zimwi jipya asiloelewa (Ukawa).

9. Matumizi makubwa ya fedha katika kutafuta madaraka. Mpaka mwisho wa mwezi Agosti 2015 Lowassa alikuwa tayari ametumia zaidi ya TZS bilioni 106 kwa kipindi cha miaka miwili na nusu kwanza kutafuta nafasi kugombea ndani ya CCM na kisha kuhamia Ukawa. Wananchi wengi wanahoji zinapotoka fedha hizi, wengi wakikumbuka kauli ya Mwalimu Nyerere kwamba “Mtanzania wa leo hawezi kukununua kabla ya yeye kwanza kununuliwa”. Wananchi wanahoji namna gani Lowassa anapanga kurejesha fedha hizi iwe zake (pia wanahoji kazipataje) au za marafiki zake (lengo lao kumpa fedha ni nini). Magufuli hana kashfa ya namna hii na hata kampeni zake za kuomba kuteuliwa ndani ya CCM hazikuwa za matumizi ya fedha kabisa. Kama wananchi watapiga kura kwa kuangalia uadilifu katika kupata na kutumia fedha, na pia kama watapiga kura wakiamini kwamba Ikulu si mahali pa kufanya biashara ili mtu arejeshe fedha alizotumia wakati wa kampeni na kuhonga kupata nafasi basi Magufuli ana nafasi kubwa ya kushinda.

10. Mzimu wa Mwalimu Nyerere: Mwaka 1995 Mwalimu Nyerere alisema wazi kwamba Lowassa hafai kuwa Rais wa Tanzania, alikatwa jina lake kwa haki (video ya Mwalimu akisema haya iko mitandaoni na ni moja ya video zinazotazamwa kwa wingi wakati huu wa uchaguzi mkuu) na hakuna maana kuendelea kumjadili na kwamba chama kisonge mbele. Watu wanaomjua vizuri Lowassa na shughuli anazozifanya wanasema kwa miaka 20 Lowassa hajabadili zile sifa zilizomfanya Mwalimu kutamka maneno yale mwaka 1995. Hata alipoomba familia ya Mwalimu Nyerere kumuunga mkono alipoondoka CCM alijibiwa wazi kwamba yeye hajawahi kuwa chaguo la Mwalimu. Watanzania bado wanamuheshimu na kumuamini Mwalimu Nyerere na ni wazi watachagua kiongozi wakifuata wosia wake. Uadilifu wa Magufuli utamuwezesha kuaminiwa na Watanzania na kushinda nafasi hii.

10 comments:

Anonymous said...

Source please?

Anonymous said...

CCM wewe hoja zako hazina ukweli wowote waTZ wameshoka na chama chako hata ukiwaambia Lowasa atakufa baada ya kuapishwa waTZ watamchagua EL mradi chama chako kidondoke October 25, wewe subiri una mwezi mmoja utapata majibu ya waTZ wanyonge. Wanaoshindwa kupeleka watoto shule sababu ya Ada, hakuna matibabu na dawa hakuna ajirira n.k wakati CCM Richmond, Escrow, Tembo machungu yote haya waTZ wanadawa yake ya kukitibu chama chako October 25. Lakini unaweza kuendelea kujipa moyo kwa hizo ndoto zako za mchana.

Anonymous said...

Tusuburi tarehe 25

Anonymous said...

ASANTE MIMI NINA HOJA MOJA TUU KWA NINI MHESHIMIWA EDWARD LOWASSA ATASHINDA UCHAGUZI MKUU UJAO. NAYO NI; ELIMU BURE KWA WATANZANIA WOOOOTE TANGIA SHULE ZA MSINGI HADI VYUO VIKUU.ELIMU, ELIMU, ELIMU, ELIMU, ELIMU, ELIMU, ELIMU.BILA KIKWETE KUSOMA, TENA BURE, ENZI HIZO ASINGETUONGOZA UPO HAPO?BILA MAGUFULI KUSOMA TENA BURE ENZI HIZO LEO HII ASINGEGOMBEA URAIS ANGEKUA KWAO CHATO AIDHA ANACHUNGA NGOMBE AU MVUVI ANAVUA. SAMAHANI UNANIELEWA LAKINI?KWA HIYO ELIMU NI UKOMBOZI; UTAWAPATA VIONGOZI, WALIMU, MADAKITARI,WANASAYANSI, WAUGUZI, KILIMO BORA, CHENYE TIJA,WAHANDISI,MARUBANI,MADEREVA,MAAFISA UGANI,MATABIBU, NA MADARAJA MENGI YA WAKOMBOZI ;SAMAHANI BADO TUPO PAMOJA AU NIMKUTUPA?LOWASSA OYEEE.NISAIDIE KUIMBA KAMA WALIVYOFANYA WAJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA CCM DODOMA MWEZI JULY 2015.HAYA TUANZE MOJA, MBILI, TATU TWENDE;TUNA IMANI NA LOWASSA,OYA, OYA, OYAAAA.LOWASSA KWELI KWELI KWELI, KWELI KWELI LOWASSA USICHOKE TUENDELEE BADO TUNA SIKU 47 TUU MASADUKU YA KURA YAAMUE. IMBA!

Anonymous said...

Una uhakika gani kuwa serikali ya Ukawa itakuondolea hayo matatizo? Ie,Ada ,ajira nk.
Au ndio biashara ya kurusha mawe gizani ukitegemea ku hit target?

Anonymous said...

Ondoa hiyo socialist mentality ya kupenda vya bure.Tunahitaji elimu bora na sio elimu bure.Bure Aghali!

Anonymous said...

This is BS, at best! Wait and you'll not have to write this BS again when your thug is dealt a debilitating blow on October 25.

Anonymous said...

Hakuna mtu yeyote anayemuombea kiongozi yeyote kufikwa na mabaya kutokana na afya yake kama jamaa yetu aliyeandika hapo juu - September 8, 2015 at 3.02 AM! Pamoja na haya yote kila Mtanzania ana uhuru wake kuelezea yale yanayomsibu pale anapotilia shaka afya ya kiongozi ye yote au kiongozi mtarajiwa. Kwa mantiki hii sioni tatizo liko wapi pale mwandishi wa makala tunayochangia alipoelezea ufahamu wake juu ya afya ya Lowassa. Ni njia kama hizi za uwazi ambazo zinaweza kumsaidia mhusika na huenda hata ufumbuzi wa tatizo, kama lipo, linalomsibu kuweza kutafutiwa ufumbuzi. Ukumbuke msemo wa kiswahili "afichae ugonjwa, mauti yatamuumbua". Tuoombee viongozi wetu wote afya njema bila kujali viongozi hawa wako vyama gani.

Pamoja na haya mimi nina sababu zangu binafsi zifuatazo ambazo zinamzuia Lowassa kuingia Ikulu - sababu ambazo mnaweza kuzikubali au kuzikataa:
1). Lowassa anasema atafuta umasikini na kuwafanya kila mmoja wetu tajiri. Mwenzetu huyu kwa kusema hivi nimekuwa najiuliza kuwa yuko dunia gani sipati majibu. Nachojua tunaweza kupunguza umaskini lakini kufuta! Naomba mtu ye yote anayejua nchi yoyote ile hapa duniani iliyofuta umasikini atupe mfano.
2). Lowassa pia anasema atabomoa nyumba zote za matembe na zilizoezekwa kwa nyasi ili ampe kila Mtanzania nyumba bora za mabati. Naomba mfano wa nchi yoyote iliyofikia hatua ya kumpa kila mkazi mahali bora pa kujihifadhi kama siyo huyu bwana kutaka watu walale nje.
3). Lowassa anasema atalishughulikia na kulitatua swala la maji katika muda wa masaa 48 ambayo ni sawa na siku mbili. Jamani huyu bwana alikuwa Waziri wa Maji zaidi ya masaa 48 wakati wake na hakuweza kutatua tatizo hili leo kuna nini atakachofanya ili kutuletea hayo maji!
4). Pia Lowassa anasema serikali yake itafanya kazi kwa spidi ya mwendo kasi wa 120 na hivyo lazima kutakuwa na maendeleo makubwa kwa muda mfupi. Waswahili wanasema “haraka, haraka haina baraka” na wenzetu kwa lugha yao wansema, “slowly but surely”. Hivi kweli tukienda kwa hiyo spidi anayoisema tutafika kokote! Hivi hata ukisema uchimbe bwawa la maji kwa spidi hiyo si utaishia kuchoka au kugonga mwamba na hivyo usifike kokote! Kama kwake ni sahihi kwa nini hakuweza kwenda spidi hii wakati wa miaka yake 38 aliyolitumikia taifa letu?
5). Mwenzetu ameanza kuomba kura zinazoambatana na udini na ukabila. Kweli Watanzania tunataka kurudi tena nyuma kiasi hicho! Sisi ambao tumeoa mbali na tulikozaliwa na wengine wameoana wakiwa dini tofauti tutaishi vipi? Kweli tutaweza tena kutembelea ndugu zetu bila kuwa na wasiwasi.
6). Huyu mheshimiwa anasema atawafungulia magaidi waliowekwa jela. Hivi anaona hawa wenzetu wanaozikimbia nchi zao shauri ya hawa magaidi wanafanya hivo kwa ajili wanataka kuishi maisha haya ya kinyama! Hivi anajua kuwa Tanzania haina mahali pa kukimbilia kama janga hili likitupata! Tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu apishilie mbali balaa kama hili nchini kwetu.
7). Fisadi. Wengi wameshaongelea hili na naungana nao.

Anonymous said...

kwa ndugu uliyecomment hapo juu, sidhani kama hoja zako zina uhalisia wowote ule au zinahitaji majibu ya point kwa point. Nikutakie siku njema

Anonymous said...

akili yangu haipelekwi kwa pesa ya mtu hata siku moja,mabadiliko sio nje ya nyumba bali hata ndani ya nyumba. nilimkubali sana mzee pindi yupo ccm lakini kakimbia kwa kusaliti chama na ipo siku atasaliti watanzania then after that our country will be betrayed with the same person who betrays his nearby friends. lets wait and see, kula yangu najua itaenda wapi nadhani hata wewe unajua ila sipo kichama ila nipo kimaono zaidi na hata kama kura yangu haitatimiza matakwa yangu sintojilaumu kwa kuipoteza bali nitaumia endapo nitarudi kuwa mtumwa kama kale. ishalah na MUNGU ailinde tnzania milele isichafuke, rais yeyote apite ila asituharibie nchi. madhara ya betrayal yanafahamika ngoja tusubiri kama je! usaliti huu utazaa matunda au utapanua mifuko ya wachache? nikutakie uzima na maamuzi mema ewe mtanzania, sijakuambia mchague nani bali kauli ya NINGE hujamwisho wa safari hivyo sijui ni mimi au wewe ndiye utatamka.