Zanzibar. Mgombea wa Urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amemuomba Rais Jakaya Kikwete na Rais Ali Mohamed Shein kubeba dhamana ya uongozi katika siku hizi chache zilizobaki za uongozi wao kwa kusimamia katiba na sheria za nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mtendeni Maalim Seif amesema marais hao wawili kuheshimu maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba na kuwataka washirikiane nae katika kuinusuru Zanzibar.
“Nawaomba sana Rais Kikwete na Rais Shein kukwepa matumizi ya nguvu na badala yake tushirikiane kutunza amani na haki za wananchi. Mimi niko tayari kushirikiana nao kama ambavyo nimekuwa nikifanya mara zote. Tushirikiane kuiepushia Zanzibar na Tanzania fedheha ya kimataifa”. Alisema Maalim Seif.
Akizungumzia kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi iwapo ni halali au sio halali Maalim Seif amesema lile lilikuwa ni tamko binafsi la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Jecha Salum Jecha ambapo Chama Cha Wananchi (CUF) kimetiwa nguvu na tamko la Makamishna wawili wa Tume waliothibitisha kwamba tamko lile ni lake binafsi.
“Ni kwamba hakukuwa na kikao cha Tume kilichokaa kuamua yaliyosemwa na Jecha, na kwamba hakuna misingi ya kikatiba na kisheria ya tamko lile” alisema Maalim Seif na kuongeza kwamba.
“Jana jopo la wanasheria wa CUF lilikutana kuangalia kwa kina kama kuna misingi ya kikatiba na kisheria ya tamko lile binafsi la Jecha Salim Jecha, na limetoa hoja za msingi zifuatazo kwa kuanzia muundo wa Tume ambapo Kifungu 119(1) kinaanzisha Tume ya Uchaguzi yenye wajumbe saba (7) akiwemo Mwenyekiti wao.
Alisema (1) Kifungu 119 (10) kinatamka kuwa: “Kiwango cha mikutano ya Tume ya Uchaguzi ni Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wane na kila uamuzi wa Tume ni lazima uungwe mkono na Wajumbe walio wengi”.
Aidha alisema (1) Kwa sababu Tume haikukaa kwa pamoja ikiwa na Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti na angalau wajumbe wengine wanne, na kwa sababu maamuzi yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume yalikuwa ni yake peke yake, maamuzi hayo kikatiba ni batili na hayana nguvu zozote.
Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF alisema waangalizi wote wa uchaguzi ikiwa ni pamoja na SADC, AU, Commonwealth Observer Team, European Union Election Observation Team, Waangalizi kutoka Uingereza na Marekani, na TEMCO, wote walisema mbali na dosari ndogo ndogo uchaguzi ulikuwa huru, wa haki na amani.
Aidha aliwaambia waandishi wa habari kwamba Mwenyekiti wa ZEC mwenyewe naye pia alisema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki ambapo Mwenyekiti huyo huyo alisimamia kazi ya uhakikiwa matokeo na kutia saini fomu za matokeo yaliyohakikiwa na kuthibitishwa za majimbo 31 ya Unguja na kuyatangaza matokeo hayo kabla.
“Kwa nini ghafla ilipofika siku ya tatu ambayo ni jana aligeuka na kukataa kuendelea na uhakiki na badala yake kudai eti kulikuwa na mambo kadhaa ya kufanya uchaguzi huo usiwe huru na wa haki? Tena dosari zenyewe za tamko lake eti ni pamoja na wajumbe wake kuvua mashati na kutaka kupigana” alisema Maalim.
Akizungumzia suala la baraza la Wawakilishi jipya Maalim Seif alisema Kifungu 92(1) cha Katiba ya Zanzibar kinaeleza kwamba maisha ya Baraza la Wawakilishi ni miaka mitano tokea lilipoitishwa mkutano wake wa mwanzo hivyo Kifungu 90(1) kinaeleza kwamba mkutano wa mwanzo wa Baraza la Wawakilishi utafanyika si zaidi ya siku 90 tokea Baraza lilipovunjwa kwa ajili ya kuitishwa uchaguzi.
Kuna masuali kadhaa ya kujiuliza alisema Maalim Seif ikiwemo ni “Rais yupi ataitisha Baraza?, Wawakilishi wapi wataitwa (wakati hawapo)?, Yote haya yanaleta mgogogro wa kikatiba ambao umesababishwa na mtu mmoja anayeitwa Jecha Salim Jecha kwa sababu tu ya kufuata maelekezo ya chama chake cha CCM”. Alihoji Maalim Seif huku akionekana kuongea kwa kujiamini.
Hata hivyo alisema kuna suali la muundo wa mpito ambapo kama uchaguzi utarejewa, kama anavyotaka Mwenyekiti wa Tume, jambo ambalo alisema halikubaliki kwa sababu ya kukosa misingi ya kikatiba na kisheria, ina maana kuwa serikali itakuwa haipo.
Akitoa sababu za kutokuwepo Maalim Seif alisema kwanza muda wa Urais ni miaka mitano kuanzia tarehe aliyochaguliwa kwa mujibu wa kifungu 28(2) cha Katiba, Ingekuwa tamko la Jecha Salim Jecha ni halali, basi maana yake hakuna Rais anayefuata kwa sababu ya kufutwa kwa uchaguzi, hivyo hakutakuwa na kiapo cha kumuapisha rais mpya. Kwa msingi huo, msharti ya kifungu cha 28(1)(a) hayana nafasi katika mtafaruku huu uliosababishwa na mtu mmoja.
“Hiyo maana yake, kipindi hicho sasa kitakuwa tete na haijulikani kikatiba ni nani ataongoza nchi? Tunasema hivyo kwa sababu vifungu vya Katiba 33(1) na (2) havitumiki hapa kwa suala la kuwa wazi kwa kiti cha Urais na kukaimiwa kwa nafasi hiyo”. Aliongeza.
Alisema hiyo ni kwa sababu nafasi ya Urais haipo kwa sababu itakuwa imemaliza muda wake ifikapo tarehe 2 Novemba, 2015, siku ambayo Urais wa Dk. Ali Mohamed Shein unakamilisha miaka mitano kamili.
Halikadhalika Maalim Seif alitaka kujua jee katika suala hilo suluhisho ni nini? “Kutokana na hoja tulizozieleza hapo juu, ni wazi kwamba tamko la Jecha Salim Jecha ni lake binafsi na kama tulivyotangulia kusema, halina misingi ya kikatiba na kisheria. Kwenye taarifa yake alisema kuwa “... kwa uwezo nilionao …”. Masuala ya kujiuliza ni uwezo upi? Chini ya kifungu kipi cha Katiba au Sheria ya Uchaguzi?” alihoji.
Katika kutilia nguvu hoja yake hiyo ya kisheria Maalim Seif alisema kwa kifupi, ni kwamba Mwenyekiti wa ZEC uwezo huo hana kikatiba na kisheria na kwa msingi huo, maamuzi yake hayo ni batili.
Kufuatilia masuali hayo ambayo majibu yake yapo kisheria Maalim Seif alisema CUF inasisitiza kile kinachodaiwa na waangalizi wote wa uchaguzi waliotoa taarifa zao kwamba uamuzi wa Mwenyekiti wa ZEC ni uamuzi wake binafsi pekee na haukuwa uamuzi wa Tume, kwani hakukuwa na kikao chochote cha Tume kilichokaa kufikia uamuzi huo.
Alisema uamuzi huo uwekwe upande na Jecha Salim Jecha amepoteza sifa ya uadilifu ambayo ni msingi mkuu wa kazi ya Tume ya Uchaguzi katika kusimamia maamuzi ya Wazanzibari ambao kikatiba (kwa mujibu wa kifungu cha 9(2) (a) ndiyo wenye mamlaka ya kuwaweka madarakani viongozi wa Serikali.
“Hivyo, anapaswa awajibike kwa hatua yake ya kuiingiza nchi katika mgogoro pasina sababu yoyote na ajiuzulu” alisema Maalim Seif huku akionekana na furaha katika mkutano huo wa waandishi wa habari.
Aidha alishauri Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar waendelee na kazi ya kukamilisha uhakiki na majumuisho ya matokeo ya uchaguzi kwa majimbo 14 yaliyobaki na kisha kumtangaza mshindi wa uchaguzi wa Rais wa Zazibar.
Alisema baada ya ukamilishaji huo alisema mshindi wa nafasi ya Urais wa Zanzibar aapishwe, Viongozi wa CUF na CCM washirikiane kuunda Serikali mpya ya Umoja wa Kitaifa itakayoiongoza Zanzibar katika miaka mitano ijayo.
“Kwa maana hiyo, kitumike kifungu 42(6) cha Sheria ya Uchaguzi kinachoeleza kwamba kama kuna matatizo yoyote katika vituo vya kupigia kura a na matokeo hayawezi kutolewa ndani ya siku tatu; basi Tume iendelee kuhesabu na kuhakiki kura na kutangaza matokeo ndani ya siku tatu nyengine na shughuli za kiserikali ziweze kuendelea” aliongeza.
Katika hatua nyengine Malaim Seif alirejea tena kauli yake ya kuhimiza Amani na kuwataka wafuasi wake na wananchama wa CUF na Wazanzibari wote kwa ujumla kuendelea kuwa watulivu na kutunza amani ya nchi yetu huku wakitambua kwamba tutayasimamia maamuzi yao waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment