Katika kesi hiyo namba 37 ya mwaka huu, mlalamikaji anaiomba mahakama itoe tafsiri ya kifungu cha 104 kidogo cha (1) cha Sheria ya Uchaguzi kama kinazuia ama la wananchi kukaa umbali wa mita 200 baada ya kupiga kura katika vituo vyao. Jana mahakama hiyo iliyoketi chini ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Sakieti Kihiyo, lilimshauri mlalamikaji kupitia wakili Peter Kibatala kubadilisha mlalamikiwa wa pili kwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi siyo mtandaji mkuu wa tume hiyo.
Majaji wengine wanaosikiliza shauri hilo ni Lugano Mwandambo na Aloysius Mujulizi. Baadaye wakili huyo aliwasilisha hati iliyofanyiwa marekebisho ikionyesha kwamba mgombea huyo wa ubunge viti maalum kupitia Jimbo la Kilombero, amefungua kesi hiyo chini ya hati ya kiapo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkurugenzi wa Nec.
Hata hivyo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Obadia Kamea, uliomba muda wa kujibu maombi hayo na ilipofika saa 8:00 mchana uliwasilisha majibu yao mahakamani.
Kwa upande wake, jopo hilo la majaji lilisema leo litasikiliza maombi hayo na kwamba mawakili wa pande zote watatoa hoja zao kuhusu maombi hayo.
Amy ambaye pia ni mpigakura mwenye maslahi na uchaguzi mkuu ujao, anaiomba mahakama kwa mujibu wa kifungu hicho sura ya 343 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 itoe ufafanuzi kuhusu haki ya wapigakura na kutoa tafsiri ya kifungu hicho kinamaanisha nini kufuatia kauli iliyotolewa na Nec pamoja na Rais Jakaya Kikwete kwamba wananchi wakishapiga kura hawaruhusiwi kukaa eneo la vituo vya kupigia kura umbali wa mita 200.
Aidha, anaitaka mahakama itamke kama ni halali kwa Rais na Nec kuzuia wananchi kukaa umbali huo ama la.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment