ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 21, 2015

Ewe mgombea, Wekeza katika kumwendeleza mtoto akiwa mdogo


Ewe mgombea, Wekeza katika kumwendeleza mtoto akiwa mdogo

Mipango kwa ajili ya watoto wadogo ipo mstari wa mbele katika vita dhidi ya umasikini. Watoto katika jamii zilizo masikini sana wamo katika hatari kubwa za kupata maradhi na utapiamlo na hawafanyi vizuri shuleni. Mipango jumuishi ya watoto wadogo inayolenga watoto walio masikini sana huzisaidia familia kuwa na mwanzo mzuri wa watoto wao na husaidia kupunguza pengo kati ya masikini na matajiri. Uwekezaji kwa watoto wadogo una faida mara saba na una thamani kuliko kuwekeza kwenye mipango ya kunusuru maisha ya mtoto hapo baadaye.

Wazazi fukara wapatiwe msaada wanaohitaji ili kuhakikisha kuwa watoto wao wanakuwa na mwanzo mzuri zaidi katika maisha. Msaada kwa ajili ya miradi ya kijamii ya kulea watoto na ya maendeleo na makuzi ya awali ya watoto itasaidia katika kuhakikisha kuwa watoto wanakua wakiwa na afya, wanapata lishe bora na wametayarishwa vizuri kwenda shule.

Maendeleo ya watoto wadogo yaingizwe katika muhtasari wa mafunzo kazini ya walimu. Yaanzishwe mafunzo kazini ya kitaifa kwa wote wanaohudumia watoto wadogo. Wale wanaofanya kazi katika jamii fukara wapewe kipaumbele katika mafunzo haya.

Zianzishwe kamati za kijamii katika ngazi ya wilaya na kata ambazo zitafuatilia upatikanaji wa huduma na kusaidia uboreshaji wa vituo vya kumwendeleza mtoto akiwa mdogo.

#AjendaYaWatoto

No comments: