MALALAMIKO YA CCM KUHUSU MATOKEO KWENYE BAADHI YA MAJIMBO
Chama cha Mapinduzi hakijaridhishwa na utaratibu wa kukusanya na kujumlisha matokeo kwenye baadhi ya majimbo. Katika majimbo manne kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa utaratibu wa uchaguzi, hasa katika kujumlisha matokeo, uliopelekea wabunge wa upinzani kutangazwa washindi. Majimbo hayo ni Iringa Mjini, Mikumi, Ndanda na Kawe. Wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo haya wamevuruga uchaguzi. Kutokana na utata uliokuwa umejitokeza wakati wa zoezi la kujumlisha kura, CCM iliomba kura zihesabiwe upya lakini ikanyimwa haki hiyo ya msingi ambayo iko kwenye sheria. Kwenye baadhi ya majimbo, ikiwemo Nyamagana, wapinzani walipewa haki ya kura kuhesabiwa upya. Kwa msingi huo, CCM imeamua kwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi katika majimbo haya. Tunataka sote tujiridhishe kwamba utashi wa wananchi umeheshimiwa. Bado tunaendelea kukusanya taarifa za maeneo mengine kama kulikuwa na ukiukwaji mkubwa uliobadilisha matakwa ya wapiga kura. Hata hivyo, tunakiri kwamba kwenye maeneo mengi tulikopoteza viti vya Ubunge, tumepoteza kihalali, hatuna malalamiko, tunaheshimu maamuzi ya wananchi, na tutafanya tathmini baada ya uchaguzi ili tubaini makosa na kuyarekebisha.
MAONI YA WAANGALIZI WA UCHAGUZI
CCM imepokea maoni ya awali ya waangalizi wa uchaguzi. Tumefarijika kwamba karibu wote wametoa kauli ya pamoja kwamba uchaguzi huu ulikuwa wa haki na huru, uliofanyika kwa uwazi na kwa amani – na kwamba changamoto zilizojitokeza ni ndogo na zimetokea katika maeneo machache kiasi zisingeweza kubadilisha matokeo ya uchaguzi yanayotangazwa sasa. Tumepokea mapendekezo waliyoyatoa kwa wadau mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha mchakato wa uchaguzi kwa miaka ijayo, na hivyo kuimarisha demokrasia nchini mwetu. Kwa kauli za waangalizi hawa, kwamba, kwa jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa, matokeo yanayotangazwa sasa ni kielelezo sahihi cha utashi wa Watanzania kuhusu viongozi wanaowataka.
MALALAMIKO YA UKAWA
Tumesikia malalamiko ya viongozi wa UKAWA kupitia mkutano wao na waandishi wa habari jana. Tumeshangazwa na kauli kwamba hawakubali matokeo ya Urais yanayotangazwa na Tume. Hata hivyo, matokeo ya Ubunge wanayakubali na, kule wanakoshinda, wanayasheherekea. Tunashangazwa kwasababu Tume iliyoandaa uchaguzi wa Rais ni hiyo hiyo iliyoandaa uchaguzi wa Wabunge, wasimamizi ni walewale, vituo ni vilevile, na sheria na taratibu zilizotumika ni zilezile. Hata fomu ya matokeo walizosaini wakala wao kwenye vituo vya kupiga kura, zimegawanywa katika sehemu (columns) tatu: Urais, Ubunge na Udiwani. Mawakala wao walisaini fomu hizo kwenye vituo vya kupiga kura. Wameanza kuwa na matatizo na matokeo haya baada ya kuona mwelekeo wa kushindwa. Kama mwelekeo ungekuwa tofauti, wangekuwa na imani na Tume, wasimamizi na taratibu zote.
Tunaomba ifike pahala sasa kwamba, katika kuijenga demokrasia yetu na kuliimarisha taifa letu, tuanze utamaduni mpya wa anayeshindwa kunyanyua simu kumpigia anayeshinda na kumpongeza. Nafasi ya mwisho aliyonayo Mgombea wa UKAWA kuendelea kujijengea heshima katika jamii yetu, na kuwa mwanademokrasia, ni kwa kufanya hivyo siku Dkt. Magufuli atakapotangazwa mshindi.
Kwetu sisi CCM, kuchagua wagombea bora na kuwanadi na kutengeneza sera bora na kuzinadi, pamoja na rekodi yetu katika uongozi wa nchi, ndio njia zetu pekee za ushawishi. Katika uchaguzi huu, wananchi wamefanya maamuzi yao kwa uhuru na utashi, ikiwemo kuwaangusha mawaziri sita ambao tuliwasimamisha kama wagombea wetu katika majimbo mbalimbali. Nguvu na utashi wa wananchi umejidhihirisha katika uchaguzi huu.
Mchakato wa uchaguzi sasa unakaribia kufikia ukingoni, tutawapata madiwani, wabunge na Rais, tunapaswa kuendelea na maisha na tuwape nafasi watutumikie. Jitihada tunazoziona sasa za viongozi wa UKAWA za kuendeleza siasa za uchaguzi kwenye mitaa ya miji yetu kwa njia za vurugu na maandamano hazikubaliki hata kidogo. Tunalaani kitendo cha wafuasi wa UKAWA kuchoma ofisi za CCM katika Wilaya ya Mbozi. Amani ya nchi hii ina thamani kuliko hitaji la madaraka la mtu yoyote. Wenzetu wa UKAWA wana haki ya kulalamika lakini hawana haki ya kuiingiza nchi yetu machafukoni kwa kuwakusanya vijana na kuwaingiza mitaani wafanye vurugu na kuhatarisha maisha, kuharibu mali na kusimamisha shughuli za watu wengine. Tunawaomba Watanzania waendelee na shughuli zao kama kawaida huku kila mmoja akitambua wajibu wake wa kuilinda amani ya nchi yetu.
January Makamba
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM
28.10.2015
2 comments:
ccm ni nyie ndio mnaosababisha vurugu. Mbona Ndg Makamba huzungumzii kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar kitendo kilichofanyika kinyume kabisa cha sheria. Mpaka Marekani inakilaani kitendo hicho. Mbona huzungumzii kitendo kiovu cha polisi kuwakamata vijana wa UKAWA na kuwaweka ndani bila makosa yoyote. Mbona huzungumzii kuhusu numbers au digits kubadilishwa na taasisi yenu ya nec ili kuwapa ccm ushindi. Ni nyie nyie ccm wa kunyooshewa vidole endapo Tanzania itaingia katika shimo la vurugu ikiongozwa na wewe Makamba. Ccm ndio chanzo cha matatizo yote haya. Pia msisahau kuwa mliwaapia wananchi kuwa mtafanya chochote liwezekanavyo ili muweze kubakia madarakani ikiwa ni pamoja na kufunga kwa goli la mkono. Acheni kuwalaumu wapinzani. Ccm mjiangalie mlikotoka. Mnawaona Wananchi watanzania kuwa ni wajinga hivyo mnaweza kufanya chochote mtakacho. Waswahili walisema kila chenye mwanzo hakikosi kuwa na mwisho. Angalieni sana nyie ccm amani yetu msije mkaiingiza katika usemi huu.
Tanzania haingii kwenye vurugu na hayo ni mawazo yako tu. Watanzania wanaelewa sana wanachokifanya ila ni watu kama ninyi tu ambao mnafikiria kuwa ni mambumbumbu. Mtu yeyote anayesoma maandiko yenu anaona jinsi yalivyo jaa matusi , kashfa na kejeli za kila aina na huku mnajidai ati mmesoma sana. Sawa CCM haina wasomi lakini kwa hali ilivyo na kama mtaendelea kulalamika tu bila kutoa hoja za maana wananchi hawatawapa kura zao na hivyo CCM itaendelea kutawala.
Unaongelea kuwa kosa kwa Polisi kukamata vijana wa Ukawa kama vile hujui kuwa walikuwa wanashirikiana na mamuluki mlioleta kutoka nchi za nje mnawaita wataalam wa IT kuja kufanya vitendo viovu vya kubadilisha na kupotosha idadi ya kura zinazotangazwa na NEC kwa ajili ya manufaa yenu. Tushukuru vyombo vya usalama wetu viko makini kugundua yote haya na watu wenu hao ambao hawana hata vibali vya kufanya kazi nchini sasa wanasota gerezani. Kama kufunga goli la mkono nyinyi ndiyo hasa mlikuwa mmepania kufanya hivyo ndiyo maana mkalata mamluki wenu.
Post a Comment