.Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mkuu wa MONUSCO, Bw. Martin Kobler akisisitiza jambo wakati wa mazugumzo yake na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania, Balozi Tuvako Manongi. Bw. Kobler alifika katika Ofisi za Uwakilishi wa Kudumu, kuishukuru Tanzania kwa mchango wake wa ulinzi wa amani katika Mashariki ya DRC. Mchango ambao amesema umeleta tofauti kubwa
"Tafadhali nifikishie salamu na shukrani zangu kwa Mhe. Rais, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri wa Ulinzi" maneno ya Bw. Martin Kobler kwa Balozi Manongi walipokuwa wakiagana baada ya mazungumzo yao mwishoni mwa wiki.
Ushiriki wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Misheni ya kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ( MONUSCO), kumeelezwa kutoa mchango mkubwa katika kurejesha hali ya Amani na utulivu katika baadhi ya maeneo ya Mashariki ya nchi hiyo.
Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki, na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika DRC na Mkuu wa MONUSCO Bw. Martin Kobler, wakati alipofanya mazungumzo na Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Bw. Kobler na ambaye alitumia fursa hiyo kuaga na kuishukuru Tanzania kwa ushiriki na mchango wake, amesema, katika maeneo mengi ambayo walinzi wa Amani wa Tanzania wanayalinda hali ya Amani imerejea kiasi ambacho wananchi waliokimbia vita wamerudi na kuendelea na shughuli zako za kila siku .
“ Katika maeneo kwa mfano la Kamango ambako wapo wanajeshi wa Tanzania, nilipowauliza wananchi wa eneo lile ni nini wanachotaka, jibu lao lilikuwa moja tu, waliniambia wanataka amani na usalama, wanaomba walinzi wa Amani wa Tanzania wasiondoke kwa sababu wakiondoka hawana uhakika wa usalama wa maisha yao” anasimulia Kobler.
Akasema mji huo wa Kamango wenye wakazi wapatao 80,000 ambao ulikuwa magofu na usiokuwa na watu, hivi sasa hali imebadilika, watu wamerejea, mji umestawi biashara zimeshamiri na wananchi wanaendelea na shughuli zao pasipo kuwa na mashaka ya usalama wao.
“ Ninazo simulizi nyingi kuhusu utendaji mzuri wa wanajeshi wenu, ni wazi pia katika utekelezaji wa majukumu yao, wapo waliopoteza maisha, lakini mchango wao na maisha yao hayakupotea bure wamefanya kazi nzuri. Mimi binafsi naomba unifikishie salamu zangu na shukrani zangu za dhani kabisa kwa viongozi wako wakuu, Mhe. Rais Kikwete, Waziri wa Mambo ya Nje na Waziri wa Ulinzi ambao sikupata nafasi ya kuwashukuru mimi mwenyewe”. anasema Kobler.
Jeshi la Wanachi wa Tanzania linahudumu katika Misheni ya MONUSCO kupitia Force Intervention Brigade ( FIB) ambayo inaundwa na wanajeshi kutoka Tanzania, Afrika ya Kusini na Malawi.
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu, amesisitiza umuhimu na nafasi ya Afrika na hususani Nchi za Maziwa Makuu wa kuhakikisha kwamba wanaendelea kuisaidia DRC ili iweze kuwa na Amani ya kudumu.
Kwa upande wake, Balozi Tuvako Manongi amemshukuru Bw. Martin Kobler kwa kuwajibika katika pindi cha miaka miwili ya uwakilishi wake, na mchango wake katika kujaribu kuwakutanisha wadau mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha Amani na utulivu unakuwapo katika DRC.
Akasisitiza kuwa Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine inataendelea kusaidia kwa kadri inavyowezekana na kwa kushirikiana na wadau wengine ili wananchi wa DRC hususani mashariki mwa nchi hiyo na ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu na hatari wanakuwa na fursa ya kuendesha maisha yao kwa Amani na utulivu.
Akaongeza kwamba ili hatimaye Amani ya kudumu iweze kupatikana, utashi na ukomavu wa kisiasa kutoka makundi yanayopigana ndani ya DRC yenyewe unahitajika kwa kuweka silaha zao chini na kuzugumza na kuweka maslahi ya wananchi wao mbele ya kitu kingine.
No comments:
Post a Comment