
Katika kuhakikisha kila kitu kinakaa sawa, mabosi wa timu hiyo wametamka kuwa wamepanga kupata kiasi cha Sh300 milioni kwa ajili ya kufanya usajili katika dirisha dogo kwa nia ya kuimarisha kikosi chao kwa kuleta vifaa vya maana.
Mabosi hao wanasema kama mipango yao itaenda watakavyo, ni lazima wapinzani wao waombe po!
Akizungumza na Mwanaspoti, Rais wa Simba Evans Aveva, alisema kuwa ili waweze kuleta nyota wenye ubora na wanaohitajika kikosini mwao ni lazima wapate ‘mzigo’ huo mnene na kudai kwa sasa wameanza kuzisaka ili pazia la dirisha dogo likifunguliwa wawe kamili gado.
Aveva alisema wakati wakijaribu kumsajili mshambuliaji raia wa Burundi, Laudit Mavugo, iliwapa funzo kubwa kuwa lazima wajipange kweli kweli kiuchumi kwani waligomewa na Vital’O kwa vile hawakuwa na dola 100,000 (karibu Sh200 milioni).
Rais huyo alikiri kuwa sio kazi rahisi kupata kiasi kama hicho wanachohitaji sasa kutokana na hali ya klabu hiyo kiuchumi, lakini uongozi wake utapambana kwa hali na mali kuweza kufanikisha zoezi hilo lengo likiwa kukata kiu ya mashabiki wa timu hiyo.
“Ukiangalia kama tulitakiwa kulipa kiasi cha shilingi 100 milioni kumpata Mavugo ni wazi tunatakiwa kujiandaa vyema sasa kama tunataka wachezaji wasiopungua watatu mpaka wanne ni lazima tujiandae kwa kutafutakiasi hicho,” alisema Aveva.
“Unajua watu hawajui jambo moja wakati tunaingia tulikuta madeni mbalimbali yakiwemo ya wachezaji wetu ambao walikuwa wanadai fedha zao za usajili tulilazimika kumalizia hayo kwanza hivyo nguvu kubwa tukaipoteza huko kitu ambacho kilitungiza katika usajili bila ya kuwa na nguvu ya kutosha, sasa tunajipanga kuhakikisha tunafanya kitu.”
Miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kunyatiwa na klabu hiyo inayokamata nafasi ya nne kwa sasa katika Ligi Kuu Bara ni Mavugo, Kevin Ndayisenga, Brian Majwega na Didier Kavumbangu ambaye anakipiga Azam kwa sasa.
Mchezaji huyo anaelekea kumaliza mkataba wake.
MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment