ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 28, 2016

Nnauye ajikoroga bungeni Dom.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye jana alitoa kali bungeni baada ya kukosea kueleza kirefu cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakati akijibu swali la mbunge.

Badala yake, Nape alisema TFF ni Chama cha Soka Tanzania, akimaanisha FAT ambayo kimfumo ilishabadilishwa kutoka chama na kuwa shirikisho.

Nape yalimkuta hayo wakati alipoulizwa swali na Mbunge wa Jimbo la Konde (CUF), Khatibu Haji aliyetaka kufahamu mipaka ya utendaji ya TFF kama inahusisha na Zanzibar.

Haji alitaka kufahamu hatua zinazochukuliwa na serikali dhidi ya watu wanaopeleka mahakamani masuala ya michezo, jambo kinyume na Sheria za Shirikisho la Soka Ulimwenguni (Fifa).

Alisema uamuzi huo unaweza kuilazimu Fifa kuifungia Tanzania kushiriki michuano ya kimataifa, jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa michezo nchini.

“Naomba kupata jibu, TFF ni Tanzania Football Federation au ni Tanganyika Football Federation? Kama ni Tanzania, suala la michezo siyo la muungano na kama ni Tanganyika, kwanini TFF inaingilia masuala ya ZFA?” alihoji.

Akijibu swali hilo, Mnauye alijichanganya nakujikuta akisema TFF ni Tanzania Football Association, badala ya Federation.

Hata hivyo, baada ya kutoa jibu hilo, kuliibuka manunguniko, huku baadhi ya wabunge wakimkosoa kuwa amechemka kuelezea kirefu cha TFF.

Baada ya manunguniko hayo, Nnauye alilazimika kubadilisha kauli yake na kueleza kuwa TFF ni Tanzania Football Federation.

Kabla ya kujisahihisha wabunge walisimama kuomba mwongozo wa Spika, wakidai kuwa waziri amesema uongo bungeni kwa kusema TFF ni chombo cha muungano.

Akiendelea kujibu maswali, waziri huyo alisema kuwa taratibu za michezo zinafahamika duniani kote.

Mnauye alisema suala la viongozi kupeleka masuala ya soka mahakamani siyo jambo nzuri, kwani ni kinyume na Sheria za Fifa na kuahidi kulishughulikia jambo hilo.

Katika swali la msingi la mbunge huyo, aliyetaka kujua tamko la serikali kuhusu makosa yanayofanyika katika klabu za soka.
CHANZO: NIPASHE

No comments: