ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 28, 2016

Simba yaisuta TFF, yatishia kugomea mechi ya Yanga

Uamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuiruhusu timu ya Azam FC kwenda Zambia kushiriki mashindano yasiyojulikana katika kalenda ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na lile la Dunia (Fifa) ni kuvunja kanuni na katiba, Simba imelalamika jana jijini Dar es Salaam.

Malalamiko ya Simba yanakwenda sambamba na kuitaka TFF kupanga mapema ratiba ya mechi za viporo vya mapema kwa timu zote ili watakapokutana na mahasimu wao Yanga katika mchezo wa marudiano Februari 20 wote wawe na mechi sawa, kinyume chake watagomea mchezo huo.

Akizungumza jana jijini, Msemaji wa Simba Haji Manara alisema kuwa mpira unaendeshwa kwa kanuni na kwa kutoa ruhusa hiyo, TFF imejikanganya yenyewe.

Manara alisema kanuni hizo zilitungwa na TFF kwa kushirikiana na klabu 16 zinazoshiriki ligi hiyo na kwa uamuzi huo wa kuiruhusu Azam FC kwenda kushiriki 'bonanza' huko Zambia ni sawa na kuvunja kanuni ilizoziandaa badala ya kuzisimamia wakiwa wao ndio waendeshaji wa ligi.

Alisema hakuna kipengele chochote katika kanuni ya 9 inayozungumzia sababu za timu kuahirishiwa mechi zake ambacho kinaruhusu mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Bara 2013/2014 kusafiri katikati ya ligi.

"Kanuni ya 9 (a), inaelezea timu itaahirishiwa mechi yake endapo wachezaji wake watano au zaidi watakaoitwa kwenye timu ya Taifa, kwa hiyo kanuni hiyo kwao haiwahusu, (b) ili timu ihairishiwe mchezo wake lazima iwe inacheza mechi ya kimataifa na taarifa ya kuahirishwa mechi yake itolewe ndani ya siku sita kabla, hili halikufanyika," alisema Manara.

Alisema pia mechi huarishwa kutokana na dharura za kibinadamu, yale mashindano hayawezi kuitwa ni dharua.

Alieleza kwamba Simba inaona Azam FC imekwenda Zambia kushiriki 'bonanza' kwa sababu wachezaji wa kikosi cha kwanza wa timu za nchi hiyo na Zimbabwe wako katika michuano ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa ndani (CHAN) inayoendelea jijini Kigali, Rwanda na ligi za nchi hizo mbili zimesimama.

"Sisi hatuwezi kufanya hivyo, ila mechi ya 20 na Yanga Africans itukute wote tuko ya 20, tutawaandikia barua TFF," alisema.

Aliongeza kwamba kuacha kucheza ligi na kwenda kucheza mechi hizo za kirafiki Zambia ni ukiukwaji wa kanuni na vilevile kanuni zinaeleza ili mechi yao ya ligi ihairishwe ni lazima uandike barua ndani ya siku 14 kabla ya mchezo husika.

TFF kupitia kwa Selestine Mwesigwa, Katibu Mkuu ilisema ilitoa ruhusa hiyo kwa Azam FC baada ya kuridhika na maombi yao na ilijiridhisha kwa kuwasiliana na wenyeji wao.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Kwani hakuna kanuni inayoruhusu uchaguzi kufanyika mapema kabla ya wakati wake katika shirika la mpira wa miguu Tanzania kama watanzania wataona shirika hilo limeshindwa kazi yake? Kwa sababu mambo wanayofanya ni aibu kwani hata hao wasomali waliokuwa hawana serikali hawawezi kufanya utumbo unaoendelea kufanywa na uongozi wa TFF.