Advertisements

Sunday, February 14, 2016

Bomu la Mbagala laua mama, mwanaye Dar

By Kalunde Jamal, Mwananchi kjamal@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hali ya taharuki ilizuka jana huko Mbagala, Kijichi, kata ya Mgeni Nani jijini Dar es Salaam, baada ya kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu, kulipuka na kusababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi wengine watatu.

Waliopoteza maisha ni Mariam Hassan (24) na mwanaye Juma Shabani mwenye umri wa miezi kumi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Andrew Satta alisema vifo hivyo vilisababishwa na mlipuko wa chuma kinachodhaniwa kuwa ni bomu.

Chuma hicho kiliwekwa kwenye moto na mtoto wa mpangaji wa nyumba hiyo, Salum Selemani (8) na baadaye kulipuka na kusababisha vifo hivyo.

Selemani alisema alikiokota chuma hicho kituo cha mabasi kiitwacho Mchicha wilayani Temeke. Inasadikiwa chuma hicho ni kati ya mabomu yaliyolipuka Mbagala mwaka 2009.

Kamanda Satta aliwataja waliojeruhiwa kwenye tukio hilo kuwa ni Mwanahamisi Salum (45), Dotto Abeid (7) na Yasir Abeid (5) na kwamba walikuwa jirani na kilipolipuka chuma hicho, wakipata chakula cha jioni.

Kwa mujibu wa maelezo ya mama mwenye nyumba hiyo, Mwanahamisi Salum mara baada ya Salum kuweka chuma hicho jikoni, aliingia ndani kwa ajili ya kupata chakula cha usiku na mama yake Neema Joshua, mpangajiwa nyumba hiyo ambao wakati mlipuko huo unatokea walikuwa ndani.

“Walipoingia ndani, baada ya dakika chache, kulisikika mlipuko mkubwa pamoja na moto, ndipo katika taharuki hiyo Mariamu na mtoto walionekana wapo chini wakiwa tayari wamefariki,” alisimulia mama huyo.

Kwa maelezo ya Salum, mtoto aliyeleta mabaki hayo ya bomu, alisema alikiokota chuma hicho ili akitumie kukatia mfuniko wake wa plastiki kwa ajili ya kuchezea.

“Nilikuja nacho nyumbani na nikaamua kukiweka kwenye jiko ili nikatie mfuniko wa plastiki nichezee,” alisema.

Mama wa mtoto huyo, Neema Joshua alisema mtoto wake alifika nyumbani na chuma hicho na kumwambia kuwa amekiokota.

“Baada ya hapo sikumfuatilia tena Salum alifanya nini na kile chuma alichokuja nacho zaidi ya kusikia mlipuko huo wakati tukiwa ndani tunakula ...sina la kusema,” alisema. Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa wa Mgeni Nani, Khuruka Mwinyimvua alisema alipata taarifa za tukio hilo na alipofika kwenye eneo hilo alikuta watu wawili wamefariki dunia.

“Tumekuwa tukitoa tahadhari kwa wakazi wa eneo hili kuhusu vyuma hasa watoto na hawa wanaookota vyuma chakavu kuwa maeneo yetu yaliathirika na mabomu mwaka 2009, hivyo wawe makini na vitu kama hivyo,” alisema.

Mazishi ya Mariam na mwanaye, yalifanyika jana saa 10 jioni kijijini kwao Chalinze mkoani Pwani.

No comments: