Mshambuliaji wa klabu ya Azam FC ya Dar es Salaam, na timu ya taifa ya Burundi, Didier Kavumbangu, amenusurika katika ajali mbaya, Gari yake aina ya Toyota Premio imehariba vibaya. Kavumbangu ameongea na mtandao wa BIN ZUBEIRY SPORTS leo kwamba ajali hiyo imetokea leo asubuhi wakati anatoka nyumbani kwake, Kijichi kwenda hospitali ya Dk Gilbert, Mikocheni kwa matibabu ya majeruhi yake yanayomuweka nje tangu mwezi uliopita.
Hii ndo Toyota Premio ya Kavumbangu inavyoonekana baada ya ajali leo. Amesema wakati anakata kona kwenye mzunguko wa magari yanayotoka Kijichi na Mbagala kuelekea mjini, ndipo alipogongwa na gari kubwa la mizigo.
“Kisheria inatakiwa wale wanaotoka Mbagala watusubiri sisi tunaozunguka tupite, lakini jamaa hakusimama akapita na moto akaipitia gari yangu kwa mbele yote imeharibika sura,”amesema.
Kavumbangu amesikitishwa na jamaa baada ya kugonga hakusimama akakimbia na hakukuwa na trafiki karibu wa kuja japo kupima ajali.
“Kwa kuwa mimi sikuumia, nikaona hapa nitapoteza muda bure, nikaita gari la kuvuta gari yangu, mimi nikaenda zangu kwa Dokta Gilbert,”amesema mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga SC.
Source: binzubeiry
No comments:
Post a Comment