ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 1, 2016

KAULI YA JPM YAMKUNA BALOZI WA KOREA KUSINI

Balozi wa Korea Kusini, Geum Young Song amesema Serikali ya nchi yake imefurahishwa na kaulimbiu ya Rais John Magufuli ya “Hapa ni Kazi Tu”.
Ameahidi kuiunga mkono kwa vitendo kwa kusukuma mbele miradi ya maendeleo inayotekelezwa na nchi yake nchini.
Akizungumza mbele ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati wa ufunguzi wa warsha ya pili ya Mpango wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira, balozi huyo alisema kazi ndiyo huzalisha maendeleo.
Alitoa rai kwa Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Magufuli kwa vitendo na muda si mrefu wataona faida yake.
Akizungumzia mpango wa kimataifa wa uhifadhi wa mazingira ambao Serikali ya Korea Kusini kupitia shirika lake la Koica linalo usimamia, Balozi Song alisema Tanzania imeonyesha mafanikio katika miaka miwili ya mradi.
Makamu wa Rais ambaye alikuwa mgeni rasmi katika warsha hiyo, alisema Serikali itafanya kila njia kuhakikisha mradi huo wa uhifadhi wa mazingira unaleta tija kwa Taifa.
“Tumeshuhudia jinsi mradi huu ulivyowawezesha wanavijiji kuibua miradi ya ufugaji wa vipepeo, nyuki, uyoga na kujipatia vipato, badala ya kutegemea uvunaji wa bidhaa za misitu, hili linatakikwa kuigwa na wananchi wa vijiji vya mikoa yote nchini,” alisema Samia.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Boneventura Baya alisema mpango huo wa miaka mitatu ulianza 2014, lakini umeongezewa mwaka mmoja.
Alisema faida ya mradi huo ambao wadau wake ni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Unesco, Koica na Serikali ya Tanzania kupitia NEMC, ni kuamsha wananchi kupunguza matumizi ya rasilimali za misitu kwa kufanya shughuli mbadala.

MWANANCHI

No comments: