Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeruhusu washtakiwa 11 wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kula njama na kuisababishia Serikali hasara ya Sh12.7 bilioni, kwenda kuhojiwa polisi.
Wakili wa Serikali, Estazia Wilson jana alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaid kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa, upelelezi bado haujakamilika.
Baada ya kutoa maelezo hayo, Wilson aliiomba mahakama kuipangia tarehe nyingine ya kusikilizwa.
Hata hivyo, alielezea juu ya kusudio la barua kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Kanda (ZCO) iliyoomba washtakiwa kwenda ofisini kwake kuhojiwa.
Hakimu Shaidi aliruhusu na alimtaka Wakili Shaid kufuatilia ili kujua utaratibu wa namna ya kuwafikisha katika ofisi hiyo.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 29, 2016 na dhamana kwa washtakiwa inaendelea.
Wakati huohuo, Mahakama hiyo ya Kisutu, Machi 3, inatarajia kutoa uamuzi kama Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea aliyeshtakiwa kwa kosa la kumtolea lugha chafu Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ana kesi ya kujibu ama la.
Hatua hiyo ilifikiwa jana mahakamani hapo baada ya mashahidi watatu wa upande wa mashtaka ambao ni Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Denis Mujumba, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Makonda na askari mwenye namba F 4829 DC, Gabriel, kutoa ushahidi wao na kuufunga.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment