Picha kutoka Maktaba
MSUKUMA AMSEMA KIKWETE KWA MAJALIWA
Mbunge wa Geita vijijini, Joseph Kasheku maarufu kama Msukuma ameyatoa ya moyoni kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu mgogoro wa Machimbo ya Nyarugusu mkoani Geita akimvaa Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete kuwa alishindwa kulitatua.
Msukuma ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita, alimueleza Waziri Mkuu kuwa suala hilo limekuwa likiwatatiza wakazi wa eneo hilo hususan wachimbaji wadogo kwa kipindi cha takribani miaka 30 na kwamba Dk. Kikwete aliahidi kulitatua suala hilo tangu alipokuwa Waziri wa Madini miaka ya 1990s lakini hata alipoingia Ikulu (2005 – 2015) alishindwa kulitatua.
“Hili tatizo la Nyarugusu ni la muda mrefu sana. Tuliliweka hadi kwenye ilani ya CCM mwaka 2010 na Kikwete aliwahi kwenda pale akaahidi kulishughulikia,” Msukuma anakaririwa.
Alisema kuwa Wananchi wa Mkoa huo wanaamini utendaji wa Waziri Mkuu hivyo wanaamini ataweza kulisimamia na kulitatua tatizo hilo.
Naye Waziri Mkuu aliwahakikishia wananchi hao kuwa wiki ijayo atamtuma Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Mhongo katika eneo hilo na kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Geita kulitatua tatizo hilo.
“Nitamuita Waziri mwenye dhamana [Mhongo] aje Geita pamoja na watalaam wa madini kwa ajili ya kulitafutia ufumbuzi. Wiki ijayo watafika hapa,” alisema Majaliwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwasimamisha kazi watumishi wawili na kuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita kurudishwa Wizarani atakapopangiwa majukumu mengine.
No comments:
Post a Comment