Siku tatu baada ya mwandishi wa Mwananchi na DW, Salma Said kutoweka, jana alipatikana baada ya kukutwa katika Hospitali ya Regency ya jijini Dar es Salaam na kupelekwa kituo kikuu cha polisi kuhojiwa.
Habari zilizopatikana jana jioni na kuthibitishwa na mumewe, Ali Salim Khamis na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi, Simon Siro zilisema Salma alisajiliwa jana mchana katika hospitali hiyo.
Ali aliyekuwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, alisema kwa ufupi kuwa amepata taarifa hizo na kufika Dar es Salaam kuzifuatilia.
Kamanda Siro alisema ni kweli Salma amepatikana na ametumwa mkuu wa upelelezi wa kanda hiyo kumfuata hospitali ampeleke kituoni kwa mahojiano.
“ Tumefungua jalada la uchunguzi wa tukio hili juzi,” alisema Sirro na kuongeza.
“Wapelelezi
walizungumza na mume wa Salma na kuna mambo amewaeleza lakini hatuwezi
kuyaweka wazi kwa sasa, hadi uchunguzi utakapokamilika, tumeipata namba
ya simu aliyowasiliana nayo na mumewe akiwa huko kunakoaminika
amefichwa,” alisema.
Wakati huo huo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika tamko lake ililolitoa jana ilieleza kuwa kutekwa kwa mwanahabari huyo kumezua maswali mengi kwa wananchi, familia yake, wadau na wanahabari wa ndani ya nchi na wale wa jumuia za kimataifa.
“Kutekwa kwa Salma kunatokana na kazi yake ya uanahabari, ndiyo maana ushahidi wa awali uliopatikana kwa njia ya ujumbe wa sauti ukiwa na sauti inayoaminika kuwa ni yake, ulieleza wazi kutekwa kwake kunatokana na yeye kuripoti dosari zinazoendelea katika uchaguzi wa marudio Zanzibar,” alisema Joseph Mbilinyi, Waziri Kivuli wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo wa Kambi ya Upinzani.
Mbilinyi ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema) alidai kuwa matukio mbalimbali yanayoendelea Zanzibar yakiwamo ya matumizi ya nguvu, vitisho na hata vitendo vya kikatili dhidi ya wanaosimamia haki, vinaendelea kuitia Serikali ya CCM doa, Taifa na dunia nzima.

1 comment:
Hivyo hao wanaojiita watu wa kambi ya upizani bungeni katika vichwa vyao hamna kitu kinachoitwa busara? Au kuilaumu serikali kwa kila jambo hata kama matapeli wanafanya uhalifu wakijisingizia kuwa wao ni watu wa serikali basi upizani wao kazi yao ni kuilaumu serikali tu bila ya hata wao kuwa na facts na wanachokilaumu? Ikiwa mtu katekwa nyara na hajulikani nani aliemteka nyara yaani bado suala lipo kwenye uchunguzi vipi mtu leo anathubutu kuinyoshea kidole serikali bila hata ya kuwa na ushahidi? Huu upizani gani tunaosema tuna upizani wa kisiasa bugeni kama si wasaliti na upuuzi mtupu? Tusubiri na tuone uchunguzi utakapokamilika wa hiyo filamu tujue nani kausika na kwa bahati nzuri hii ni serikali ya mwendo wa kasi tunaimani uchunguzi utakamilika haraka kuutambua ukweli. Ila kutokana na kelele za upinzani wakiongozwa na CUF katika suala hili dhahiri wameonyesha jinsi gani wanavyosheherekea na kuiombea nchi kuingia katika matatizo yaani ni kama kwamba walishajua nini kitatokea na tayari walishazielekeza makombora ya lawama zao sehemu fulani kwa kweli ni jambo la hatari sana.
Post a Comment