Kikosi kazi maalumu cha kuchunguza makosa makubwa ya kihalifu kimewatia
mbaroni vigogo wawili wa Wizara ya Maliasili na Utalii, wakihusishwa na
utoaji wa kibali cha kusafirisha tumbili 61 kwenda nchini Albania.
Maofisa
hao ni Mkurugenzi wa Idara ya Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Dk
Charles Mulokozi na ofisa mfawidhi wa kituo cha uwindaji wa kitalii,
utalii wa picha na Sites cha jijini Arusha, Nyangabo Musika.
Kikosi
hicho kinaundwa na wachunguzi kutoka Polisi, Idara ya Uhamiaji, Usalama
wa Taifa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kikosi cha kupambana
na ujangili nchini na Takukuru.
Wakati Dk Mulokozi anakamatwa,
tayari alikuwa amesimamishwa kazi kwa agizo la Waziri wa Maliasili na
Utalii, Profesa Jumanne Maghembe kwa kutoa kibali wakati Serikali
ilishazuia.
Vyanzo mbalimbali vimesema jana kuwa
Dk Mulokozi alikamatwa mwishoni mwa wiki na jana alisafirishwa chini ya
ulinzi kwenda kituo cha polisi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Kilimanjaro (Kia).
“Hivi tunavyozungumza, Dk Mulokozi yuko njiani anapelekwa Kia chini ya ulinzi mkali wa polisi.Nyangabo yeye tayari yuko mikononi mwa vyombo vya ulinzi na usalama pale Kia,” kilidokeza chanzo chetu cha uhakika.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa alipoulizwa jana
hakukanusha wala kukiri kuwa na taarifa za kukamatwa vigogo hao, lakini
alisema atakuwa na mamlaka ya kuliongelea wakiingia mkoani kwake.
“Bado
sijapewa hizo taarifa, lakini hata kama ningezijua nisingeweza
kuzungumzia tukio la kukamatwa kwao lililofanyika mkoa mwingine.
Nikikabidhiwa ndiyo naweza kusema chochote,” alisema Kamanda
huyo.
Hata hivyo, Waziri Maghembe alithibitisha kukamatwa kwa
vigogo hao, akisema katika tukio hilo yeyote aliyetia mkono wake lazima
akamatwe na kushitakiwa.
“Ni kweli Dk Mulokozi amekamatwa na
siyo yeye tu kuna ofisa mwingine pale ofisi yetu ya Arusha naye
tumemkamata. Hatuna mchezo katika suala hili,” alisisitiza.
Profesa
Maghembe alitumia fursa hiyo kusisitiza kuwa raia wa Uholanzi
waliokamatwa na polisi hawakuwa na vibali halali vya kufanya biashara ya
kusafirisha wanyama hai kwenda nje ya nchi kama baadhi ya watu
wanavyodai.
“Hawa Waholanzi walikuwa na tourist visa (waliingia
kama watalii). Halafu Watanzania waelewe mtu hawezi kupata kibali cha
kusafirisha mnyama hai kabla ya kumkamata, kuhesabiwa, akakaguliwa na
kupata vibali stahiki,” alisisitiza.
Raia hao wa kigeni
ambao ni ndugu wa familia moja, Artem Alik Vardanyian (52) ni mkurugenzi
wa mgahawa huko Uholanzi na Eduard Alik Vardanyian (44), meneja wa
hoteli huko huko Uholanzi.
Hata hivyo, vyanzo vingine
vimedai kuwa pamoja na kuwapo kwa vibali hivyo, lakini
hapakuwapo na “release order” inayotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), kama sheria inavyoelekeza.
Chanzo hicho kilidai wanyama
hao walikuwa wasafirishwe kwa kutumia ndege ya mizigo ya kukodi ambayo
ilitokea Afrika Kusini na ilikuwa iwapeleke wanyama hao Albania kupitia
Nairobi nchini Kenya na Nigeria.
“Hao marubani wa hiyo ndege
waliitwa pale Polisi (Kia), wakaandikisha maelezo yao kuwa walikuja
kuchukua wanyama hao na wakaambiwa wao waondoke tu hakuna mnyama
anaondoka,” alidokeza ofisa mmoja katika uwanja wa Kia.
2 comments:
Huyu waziri kweli alikuwa mzigo,hii ni biashara halali watu wanavibali halali.sijui ni kwa nini?hata hakuwauliza watalaamu wake,huyu kakurupuka tu.Tanzania inaruhisiwa kuuza nje nyani wasiopungua 6000 kwa mwaka na ipo national quota ambayo imekuwa approved na CITES-GEVEVA,amesimamisha watu kutofanya chochote wakati watu wanawanyama,vibali vyakukamata hawa wanyama,je watakaa nao hadi lini?? nani atalipa gharama za kuwatunza.kwa kweli hawa mawaziri wa aina wasiojua adhali kwa wanannchi wake ni hawafai.je hawa waholanzi wakidai fidia nani?? atawalipa??? ni kuwaonea tu kwa kuwa wao sio wahisika wa kukamata porini kampuni iliyopewa order ndiyo inayohusika kukamata porini na kuwasafirisha.yaelelkea huyu waziri hajui hili au hajui taratibu za hioi biashara ya nyara zinavyofanywa.
Anon wa 10:55am, Hivyo vibali halali ulivotoa wewe? Biashara gani halali unayoithibitisha kufanyika wakati kiongozi wa juu wa hiyo biashara hana taarifa? Waziri ni kiongozi mkuu wa wizara na kitu chochote kitakachofanyika katika wuzara yake ni haki yake kujua na kama hana taarifa kwa nini asihoji? Au ulitaka mpaka hao wanyama wasifrishwe hata kwa vibali halali alafu muanze kusema waziri Maghembe anauza rasilimali za taifa nje nakadhalika nakadhalika? Tena badala ya tumbili 60 mngesema kasifirisha tumbili 6000' Na tunapozungumzia mali asili kusafirishwa nje bila ya vibali husika maalum huo ni uhujumu wa uchumi na usaliti wa nchi yetu kwani unapochukuwa wanyama hai kuwapeleka nchi nyengine bila ya vitambulisho maalum ambavyo hata jumuia ya kimataifa inatakiwa kuwa hivyo ili kulinda uasili wa wale wanyama ili muepusha ile nchi ngeni kuja kuandika haki miliki yakuwa wao ndio wenye uasili wa wale wanyama na ikitokezea nchi ngeni kufanikiwa kujimilikisha uasili ya hao wanyama basi wanayo haki ya kuwadai hata wale wanyama waliobaki Tanzania. Tunaweza kulichukuliwa jambo hili kirahisi rahisi kutokana na upumbavu wetu watanzania wa kutojimbua. Hao waholanzi kama ingelikuwa wao ndio watanzania wamefanya kosa hilo huko uholanzi basi watanzania wote tungezuiliwa visa ya kuingia uholanzi na kuambiwa wezi.Yaani kuna mijitu sijui haija tembea dunia au vipi? Si zungumzi kwa ubaguzi lakini inakera kuona mtanzania au mwaafrica anamkingia kifua mzungu na kumtukana waziri wa nchi kwa kitendo cha kulinda rasilimali zetu zisitoroshwe. Yaani kuna wapuuzi wanawaona wazungu watu wa maana sana. Hao wazungu wamezoea kwenda Africa kufanya vitendo vya kipuuzi kwa kujua yakwamba waafrica ni wapuuzi sasa tumepata viongozi wa kuwaambia enough is enough basi baada ya kuwaunga mkono viongozi wetu katika mapambano ya kupinga kuonekana watu wa hovyo ndio kwanza mijitu inafanya mikakati ya kuwavunja nguvu ama kweli uafrica ni shida sana. Nna wasi wasi kuna wakenya wanatoa maoni hapa wakijufanya watanzania kwani wazungu wanatabia ya kufanya wanavyotaka kutoka kwa ndugu zetu wale nchi jirani na pengine mshenga wa hii biashara tumbili ni kutoka huko huko nchi jirani siamini mtanzania angeweza kumlaumu waziri katika hili jibu au huyo mtanzania anayemlaumu muheshimiwa waziri atakuwa jibu tena la utosini. Hongera muheshimiwa waziri wa maliasili tena unastahili pongezi sana na zidisha kukaza buti kwani wizara yako ni moja ya wizara yenye changamoto sana na inaonekana kuna watu hawakutakii mema kwa watanzania tunaamini asiekutakia mema haitakii mema Tanzania kwa hivyo tunaendelea na tutaendelea kukuunga mkono mpka kieleweke.
Post a Comment