ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 19, 2016

Wakuu 21 wa wilaya kwenye chekeche

Baada ya kufanya uteuzi wa wakuu wa mikoa uliowaondoa makada 12, homa ya chekeche la Rais John Magufuli sasa linahamia kwa wakuu wa wilaya, ambao baadhi wameshaanza kuaga wakisema hawana uhakika wa kuendelea kushika nafasi zao.
Hali hiyo inatokana na Rais kuweka bayana vigezo atakavyotumia kufanya uteuzi wa wakuu hao wa wilaya ambavyo ni pamoja na suala la migogoro ya ardhi, tatizo la elimu hasa upungufu wa madawati, njaa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.
“Nikisikia wilaya inaomba chakula wakati mvua zinanyesha wakati huu, nitakuwa na shaka na viongozi waliopo. Wanashindwaje kuhamasisha kilimo?” alihoji Rais.
Vigezo hivyo alivitangaza wakati akizungumza na wazee wa Jiji la Dar es Salaam, lakini katika uteuzi wa wakuu wa mikoa alizungumzia pia suala la wafanyakazi hewa ambao wamekuwa wakilipwa mishahara bila ya wahusika kuchukua hatua kudhibiti.
Kwa maana hiyo, vigezo vya Dk Magufuli vinaweza kuwa vingi zaidi kulingana na matatizo ya eneo la wilaya, hasa baada ya mkuu huyo wa nchi kuamua kutumia vijana wake kwenda kuchunguza matatizo kwenye maeneo ambayo anataka kusimika uongozi.
Suala la udhibiti wa fedha za umma, hasa mishahara ya wafanyakazi hewa, linaweza kuwa kigezo kikubwa cha Dk Magufuli hasa kutokana na tatizo hilo kuzungumzwa kwa muda mrefu bila ya kutafutiwa ufumbuzi na udhibiti wa mapato kuwa moja ya ajenda kubwa za Serikali ya Awamu ya Tano.
Kwa mujibu wa uchunguzi ambao Mwananchi imeufanya kwenye baadhi ya mikoa, chekeche hilo la Rais linawaweka kwenye hali ngumu wakuu wa wilaya 21 iwapo watabainika hawajachukua hatua madhubuti za kukabiliana na matatizo hayo manne.
Suala la njaa litakuwa limewagusa viongozi wa Wilaya ya Isimani mkoani Iringa, Chamwino (Dodoma) na Rorya (Mara) pamoja na Kilindi mkoani wa Tanga ambako kuliripotiwa baa la njaa.
Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na wazee mkoani Dar es Salaam Februari 15, Rais Magufuli aliitoa mfano wa Wilaya ya Bariadi iliyopo Mkoa wa Simiyu, akisema imejenga kilomita 4.5 za barabara ya lami kwa Sh9.2 bilioni, fedha ambazo zingetosha kujenga kilomita 22 mpaka 23 za lami.
“Viongozi wao wapo, mkuu wa mkoa yupo, mkuu wa wilaya yupo, mkurugenzi wa manispaa yupo, injinia yupo! Kwa hiyo, ninapozungumza kutumbua majipu, mniunge mkono nitumbue kwelikweli,” alisema.
Mkuu wa wilaya hiyo, Ponsiano Nyami, ambaye aliwahi kumuomba Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete atengue uteuzi wake kwa kushindwa kushughulikia kikamilifu ujenzi wa maabara, atakuwa akiangalia mlango wa kutokea.
Siku chache zilizopita alitoa kauli iliyoonekana kama anaaga baada ya kusema kwenye mkutano kuwa hakuna mwenye uhakika wa kubaki kwenye nafasi hizo.
Migogoro ya ardhi isiyokwisha mkoani Morogoro, hasa Wilaya ya Mvomero ambayo ilisababisha Dk Rajab Rutengwe avuliwe ukuu wa mkoa, itamuweka kwenye hali mbaya mkuu wa wilaya hiyo, Betty Mkwasa baada ya mapigano kutokea mara mbili tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani Novemba mwaka jana.
Hivi karibuni, zaidi ya mbuzi na kondoo 38 waliuawa kutokana na migogoro ya wakulima na wafugaji. Hii ilitokea wiki chache baada ya mtu mmoja kuuawa sawia na ng’ombe zaidi ya 71.
Wakati mapigano yalipotokea Desemba, Mkwasa alisema mapigano hayo yamekuja wakati Serikali ya wilaya ikijipanga kufanya operesheni ya kuwaondoa wafugaji wavamizi kwa kuwa asilimia kubwa kijiji hicho ni wakulima.
Mkwasa alisema mifugo inayoingia ni ile inayoondolewa katika Hifadhi ya Wami Mbiki na mingine inayotokea wilaya za Handeni na Kilindi za mkoani Tanga na Manyara, hivyo imekuwa ikiingia katika vijiji vya wakulima na kusababisha migogoro.
Migogoro ya ardhi pia iko wilayani Nyamagana ambako Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliunda kamati ya ushauri kuhusu kuhusika kwa maofisa ardhi kwenye migogoro hiyo.
Kutokana na wafanyakazi wa halmashauri kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi Nyamagana, tayari Waziri Lukuvi amesimamisha kazi wafanyakazi mara mbili baada ya kupelekewa malalamiko na wananchi.

Mkuu wa wilaya aaga watumishi
Suala la elimu ambalo lilimfanya Paul Makonda kupanda cheo kutoka mkuu wa wilaya hadi mkoa, litakuwa mwiba mchungu kwa mkuu wa Wilaya ya Nyamagana ambayo ina upungufu wa madawati 16,558 katika shule zake 153 za msingi na sekondari.
Mkuu wa wilaya hiyo, Baraka Konisaga jana alitumia mkutano wa kujitambulisha kwa mkuu mpya wa Mkoa wa Mwanza, kuaga watumishi wa Serikali akisema anaweza asiwemo kwenye uteuzi mpya.
“Naweza kuongea nanyi hapa muda huu nikiwa mkuu wa wilaya, lakini jioni mkasikia uteuzi wa wakuu wapya wa wilaya. Naweza kuwamo na nikabakishwa hapahapa Nyamagana, nikahamishiwa wilaya nyingine au nisiwemo kabisa kutokana na vigezo kadhaa ikiwamo utendaji na umri.”
Hata hivyo, alijimwagia sifa kuwa kwa kipindi chote alichokuwa mkuu wa wilaya hiyo kwa vipindi vitatu tofauti vya uteuzi, alifanya kazi kubwa kusimamia maendeleo, ulinzi na usalama wa wananchi, huku akikaimu nafasi ya mkuu wa mkoa.
Alipoulizwa mara baada ya kikao hicho kumalizika kwa nini aliamua kuaga, Konisaga alisema: “Ni jambo la kawaidia kuwaandaa kisaikolojia watumishi wenzako iwapo kutatokea mabadiliko yoyote. Hakuna ajabu na wala hii haimaanishi kwamba sijiamini katika utendaji wangu. Najiamini sana na nimetekeleza wajibu wangu kikamilifu.”
Mkoani Tanga, aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Mwantumu Mahiza alisema wakati akimkabidhi rasmi ofisi mbadala wake, Martin Shigela kuwa kwa migogoro ya ardhi kwenye maeneo sugu kama Jiji la Tanga na wilaya za Kilindi na Handeni, kamati iliyoundwa kushughulikia tatizo hilo imeshamaliza kazi na dawa imeshapatikana.
Pamoja na maelezo hayo ya Mwantumu, migogoro ya ardhi ni tatizo kubwa mkoani Tanga na kumekuwa na malalamiko mara kwa mara ya kutokuwa na imani hata na kamati ilivyofanya kazi hiyo ya kutafuta dawa ya migogoro isiyokwisha baina ya wafugaji na wakulima, pia ugomvi wa mipaka ya vijiji mkoa wa Tanga na Manyara.
Ikiwa kitafuatwa kigezo cha migogoro ya ardhi basi wakuu wa Wilaya za mkoa huo, Abdullah Lutavi (Tanga) Selemani Liwowa (Kilindi ) na Husna Rajab (Handeni) wanaweza kuwa katika hatihati ingawa maeneo yao kwa kipindi hiki yametulia ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Kipindupindu jipu Kyela
Mkoa wa Mbeya, Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Thea Ntara yuko kwenye hali ngumu kutokana na tatizo la ugonjwa wa kipindupindu.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Clemence Kasongo alisema ugonjwa huo unamnyima usingizi kutokana na kuibuka kwenye mwambao wa Ziwa Nyasa ambako kuna wagonjwa wengi ambao alisema hutokea Wilaya ya Ludewa.
Kutokana na tatizo hilo kuwa kubwa wilayani Kyela, mwezi uliopita wazee wawili wa kitongoji cha Bulinda waliuawa na wananchi kwa madai kuwa ndiyo wanaosababisha watu waugue kipindupindu kwa njia za kishirikina.
Ugonjwa huo pia uko kwenye wilaya za Musoma Vijijini, Ilala na Mpanda.
Wakuu wa wilaya mbili za mkoani Kilimanjaro wamekalia kuti kavu katika vigezo hivyo.
Wilaya ya Same inakabiliwa na migogoro ya ardhi baina ya wananchi wa jamii ya wafugaji wa Kimasai katika Kijiji cha Ruvu Mferejini na mwekezaji wa kampuni ya IBIS International Ltd.
Tangu mwaka 1988, mmiliki wa IBIS International Ltd ambaye ni raia wa Sweden aliingia mkataba na wananchi wa Kijiji cha Ruvu kabla ya kijiji hicho kugawanyika na kuunda kijiji kingine cha Ruvu Mferejini kwenye shamba lenye ukubwa wa ekari 642.
Pia, Wilaya ya Mwanga inakabiliwa na mgogoro wa ardhi baina ya wanakijiji cha Jipe na mwekezaji wa kampuni ya kitalii ya Asante Tours kuhusu eneo la ekari 3,000. Migogoro yote hiyo bado haijatatuliwa.
Mkoani Dodoma ukiacha Wilaya ya Chamwino ambayo imekuwa ikabiliwa na njaa, Kongwa kumekuwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji ambao pia umekuwa ukihusisha Wilaya ya Wilaya ya Kiteto na kusababisha mgongano kwa wanasiasa.
Mgogoro wa wakulima na wafugaji katika wilaya hizo mbili umekuwa wa muda mrefu na uliingia kwenye Bunge la Kumi.
Mauaji mengi yamekuwa yakitokea upande wa Kiteto lakini yakihusisha wakazi wa Kongwa, kiasi cha kusababisha mbunge wao, Job Ndugai, ambaye sasa ni Spika wa Bunge, kulalamika bungeni dhidi ya ungozi wa Wilaya ya Kiteto.

Arusha na migogoro ya ardhi
Wilaya tatu za Mkoa wa Arusha; Ngorongoro, Monduli na Arumeru, bado zinakabiliwa na tatizo la migogoro ya ardhi lakini kuna jitihada zinaendelea kuitatua.
Wilaya ya Ngorongoro ambayo mkuu wake ni Hashim Mgandilwa bado ina migogoro ya mipaka ambayo imekuwa ikisababisha mapigano ya jamii ya Wasonjo na Wamasai. Monduli, ambayo mkuu wake ni Francis Miti kulikuwa na migogoro ya ardhi ya mashamba kutokana na maofisa ardhi kugawa ovyo viwanja kwa masilahi yao.
Wilayani Arumeru, hasa eneo la Meru, ambako Mkuu wa Wilaya ni Wilson Nkumbaku kuna migogoro ya ardhi baina ya wamiliki wakubwa na vijiji. Wakuu wa wilaya hizo wameeleza changamoto zote zinaendelea kupatiwa ufumbuzi. Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mngandilwa alisema wilaya yake ni salama baada ya migogoro kupungua, wakati Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Fadhili Nkurlu alisema Arusha sasa ni shwari na wananchi wanashiriki mambo ya maendeleo.
Imeandaliwa na Burhani Yakub, Lauden Mwambona, Happiness Tesha, Sharon Sauwa, Ngollo John na Mussa Juma.

No comments: