
Dar es Salaam. Rais John Magufuli analipwa Sh9.5 milioni kwa mwezi.
Huo ndiyo mshahara ambao mkuu wa nchi ameutangaza kwa umma bila ya kutoa ufafanuzi kama unajumuisha marupurupu mengine kulingana na cheo chake.
Rais ameamua kuweka hadharani masilahi yake wakati kukiwa na mjadala mkubwa uliotokana na tamko lake alilolitoa mapema wiki hii kuwa atapunguza mishahara ya watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kutoka Sh40 milioni hadi Sh15 milioni, akisema katika “Serikali ya Magufuli”, ambayo itadumu kwa miaka 10 iwapo atachaguliwa tena mwaka 2020, hakuna mtu atakayelipwa zaidi ya kiwango hicho.
Dk Magufuli, ambaye hivi sasa yuko nyumbani kwake Chato mkoani Geita kwa mapumziko aliamua kutangaza mshahara wake baada ya wabunge wawili, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo) na Tundu Lissu (Chadema) kuripotiwa kutaka atangaze mshahara wake baada ya tamko la kupunguza mishahara ya vigogo wa mashirika hayo ya umma.
Wakati wa kipindi cha asubuhi cha 360 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Clouds, watangazaji walisoma habari hiyo na kuanza kujadili mshahara wa Rais.
Wakati wakijadili ndipo Rais alipowapigia simu kuwatajia mshahara wake.
Meneja wa kipindi cha 360 ambacho hufanya uchambuzi wa magazeti, Hudson Kamoga aliithibitishia Mwananchi kuwa Rais Magufuli alimpigia simu kumtajia mshahara wake.
“Aliniuliza kwa nini sikuwapo kwenye kipindi, nikamjibu kuwa nipo Arusha kwa majukumu mengine,” alisema Kamoga.
“Akaniambia niwaambie wenzangu ambao wapo kwenye kipindi kuwa mshahara wake wa mwezi ni Sh9.5 milioni na mshahara huo ameukuta na kwamba akirudi Dar es Salaam, twende ofisini kwake akatuonyeshe salary slip.” Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa alisema Ikulu hakuna mtu anayelipwa zaidi ya Sh9.5 milioni.
“Kwa hiyo kama Rais ameamua kuzungumza nao (Clouds) kuhusu mshahara wake, naomba asubiriwe akirudi Dar es Salaam akawaonyeshe salary slip yake kama atafikia hatua hiyo,” alisema Msigwa. Lakini uamuzi wake wa Rais kutangaza mshahara wake, umekosolewa na Lissu.
“Mshahara alioutangaza Rais unaendelea kuwaweka wananchi njiapanda kwa kuwa hauna uchanganuzi,” alisema Lissu alipoulizwa maoni yake kuhusu kiwango cha mshahara wa mkuu wa nchi.
“Anapaswa kueleza iwapo ni fedha ya jumla, marupurupu yapo humo ndani kwa sababu mshahara wa mbunge ni Sh3.6 milioni na anapohesabiwa marupurupu yake inafikia kiasi cha Sh12 milioni na hizi ndizo anazoondoka nazo.
“Sasa tunahitaji kujua kama ndiyo fedha anayokwenda nayo nyumbani au ni vinginevyo.”
Kabla ya Dk Magufuli kufanya hivyo, kumekuwa na mjadala kwa muda mrefu kuhusu mshahara wa Rais, na kila vyombo vya habari vilipojaribu kutaja, Ikulu ilikanusha mara moja lakini haikutoa ufafanuzi wa kiwango sahihi cha mshahara.
Mtandao wa African Review mwaka jana ulifanya uchambuzi wa mishahara ya marais Afrika na uliwataja marais watano wanaoongoza kwa kuwa na mishahara mikubwa kwa mwaka kuwa ni Paul Biya wa Cameroon anayelipwa dola 610,000 za Marekani, akifuatiwa na kiongozi wa Morocco, Mfalme Mohammed VI (dola 480,000) na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini (dola 272,000).
Katika orodha hiyo, Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete alishika nafasi ya nne akitajwa kupata dola 192,000 na wa tano alikuwa Rais Abdel Aziz Bouteflika wa Algeria, anayelipwa Dola168,000.
Madhumuni ya utafiti wa mtandao huo yalikuwa ni kuangalia kiasi wanacholipwa marais wa Afrika kwa mwaka na kile inachopata taifa husika kwa muda huo.
Pia walilenga kuangalia uhusiano wa viongozi na wananchi wa kawaida wanaowangoza.
Kwa mujibu wa mtandao huo, vyanzo vya taarifa za mishahara ya marais hao vilipatikana kutoka mitandao na wanahabari wa nchi husika. Habari hizo ziliporipotiwa, Ikulu ilikuja juu lakini haikutaja mshahara halisi wa Rais.
Habari zaidi na Herieth Makwetta.
5 comments:
Hao akina Tundu Lisu waache kuwazingua watanzania . Tundu Lisu alikuwa anapiga kelele na kutaka kujijengea umaarufu katika suala la mshahara wa raisi. Muheshimiwa raisi kama watanzania wengi wanavyomkubali kutokana na uadilifu wake bila ya kusita ameeka hadharani kiwango cha mshahara anaolipwa. Sasa akina Lisu wanasema hapana tunataka kujua marupu rupu? Hapo utaona akina Lisu ni watu wenye kuendeleza siasa za kipuuzi hawapo serious. Tuwe wawazi kabisa kwa kazi anayoifanya Magufuli ni ya hiari zaidi na kujitolea tukija kwenye thanani halisi ya malipo na kazi anayoifanya Magufuli Tanzania haiwezi kumlipa itatubidi tutafute wafadhili wa nje watusaudie kupata fedha kulipa msharahara wa Magufuli.
Kwa kazi anayoifanya JPM hata hiyo milioni 9.5 haitoshi, alipwe zaidi. Ila, kwa kazi ya hayo wabungwe wala rushwa, hawastahili hata shilingi milioni moja.
tutafute wafadhiili wa nje watusaidie kupata fedha kulipa mshahara wa Magufuli.. Umeanza vizuri unamalizia na sentensi zisizona mwelekeo! Umekurupuka kuandika bila kutafakari. Huyu ni Rais wa nchi awe anafanya hafanyi kama aliyepita mshahara sio tija sana kwani ana mambo mengine anayotakiwa kuyapata bila kuainisha hivyo mshahara huo ni haki kwake kwani Ikulu sio kampuni, waTanzania tunaweza kulipa mshahara wake kwa kuwajibika ipasavyo hatuhitaji wafadhili.
Swala la hao wnaouliza ni haki yao, kwani Rais aliyetoka alikuwa na safari za nje ngapi kwa mwezi na alikuwa anasafiri na jopo la watu wangapi? je alikuwaa anatumia fedha kiasi gani mshahara wake ukiw auko palepale? Maagufuli hajasafiri na ameridhika na alichokikuta. Tulikuwa karibu na hizo safari tulikuw atunaona jinsi hoteli anazofikia na makundi hayo gharama yake wala usiguse?!! Sio kosa kuuliza na ndio jinsi ya siasa inavyokuwa popote pale. Jifikirie kwanini kima cha chini ni chini kweli kweli kwa wafanyakazi walio wengi?!!
Kudos annony wa hapo juu. all presidents are supposed to be taken care of people's tax money. The salary is just for his personal use. My little brother Tundu Lissi should shut up his big mouth and let the Super President do his job.
wanatupotezea tu MAGUFULI OYEEE
Post a Comment