Advertisements

Wednesday, April 27, 2016

WAZIRI UMMY ATAKA TAARIFA KUHUSU VIFAA VYA SH2 BILIONI AMBAVYO VIKO NJIANI KWENDA MUHIMBILI

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Musa Juma Assad imezichanganya Hospitali ya Taifa Muhimbili na Bohari ya Dawa (MSD), huku Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akihitaji maelezo ya kina kuhusu mkanganyiko huo.
Ummy ameitaka MSD kuandika maelezo ya kina kwa maandishi, kuhusu vifaa vya Sh2 bilioni ambavyo viko njiani kwenda Muhimbili kwa miaka minne sasa, kabla wizara yake haijatoa tamko rasmi.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mkurugenzi wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema bohari haina mzigo wowote ulio njiani kuelekea Muhimbili bali imekuwa ikisambaza dawa zake nchi nzima.
Bwanakunu alisema tatizo lililojitokeza ni mfumo wa kompyuta ambao unaonyesha mzigo upo njiani, hivyo muamala katika kompyuta unavyoshindwa kukamilika, mzigo lazima uonekane upo njiani.

“Mwaka 2012 tulibadilisha mfumo wa kompyuta kutoka wa awali mpaka tunaotumia sasa, hivyo kuna miamala ilihitaji kubadilishwa, mwaka huu tulifanya zoezi la kukamilisha baadhi na si kwa Muhimbili pekee kwa mfano kuna mzigo unatoka MSD Ubungo kwenda Muleba ukifika kule mtu anashindwa kuingiza kwenye mfumo kwamba umepokelewa,” alisema Bwanakunu.
Alifafanua kwamba majibu ya MSD kwa CAG yalieleza kuwa walitengeneza timu ya uchunguzi na baadhi ya watu walichukuliwa hatua, “nimeshachukua hatua za haraka baada ya kupata hiyo ripoti, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wale ambao hawakujaza hiyo miamala tulishawachukulia hatua, hakuna mali iliyopotea MSD.”
Taarifa zaidi zinaeleza kwamba kuna ripoti ya Muhimbili ambayo inaonyesha katika vitabu kwamba kuna mzigo ambao Muhimbili iliununua kutoka MSD, lakini haujafika, lakini Bwanakunu alipoulizwa alisema hakuna vitabu vinavyoonyesha kuwa Muhimbili inadai vifaa tiba na dawa MSD.
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru alisema kwa taarifa alizonazo mpaka sasa CAG alifanya ukaguzi katika vitabu vya MSD na si wao na alipouliza vifaa viko wapi alijibiwa kuwa vinakwenda MNH.

Source:Mwananchi

No comments: