Waziri Mkuu wa Zamani, Edward Lowassa amewahakikishia wananchi wa Monduli kuwa bado yupo nao katika kuwaletea maendeleo.
Lowassa ambaye alikuwa mbunge wa Jimbo la Monduli karibu miongo miwili enzi akiwa mwanachama wa CCM, alisema juzi kuwa bado atashirikiana na wananchi wa jimbo hilo.
Lowassa alihamia Chadema na kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana.
Akizungumza katika mahafali ya shule ya sekondari ya Irkisongo iliyopo wilayani humo juzi, Lowassa alielezea miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofanyika wilayani humo kwa kushirikiana na wananchi.
Alitaja baadhi ya miradi hiyo kama maji ya kutosha mpaka miaka 20 ijayo na hospitali kubwa ya kisasa ambayo itawafanya wananchi wengi kupata huduma za afya bila kulazimika kwenda mjini Arusha.
Mafanikio mengine ni pamoja na kukubaliana kuhifadhi shule za sekondari za wasichana zilizopo Monduli ambazo ni Masai, Enyorata,Irkisongo na Kipok.
"Bado nitaendelea kuyahifadhi mambo ya Monduli, ntashirikiana na mbunge si kumwangusha bali kuhakikisha maendeleo ya Monduli yanabaki palepale." Alisema
Aliwataka wazazi kuhakikisha wanaendelea kuwasomesha watoto wao licha ya kuwapo kwa shida kubwa ya ajira
Alisema wanafunzi hao na wengine wanamaliza masomo yao wakati mgumu,dunia ikiwa imebadilika.
"Wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne, cha sita na vyuo vikuu hawakutani na ajira, Ajira imekuwa tatizo kubwa."Alisema
Alisema pamoja na ukubwa wa tatizo hilo, silaha pekee wanayoweza kuwapatia watoto wao ni elimu.
"Hizi fedha, nyumba na magari yataisha na kupotea,lakini elimu itabaki vichwani."Alisema
No comments:
Post a Comment