Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akijadiliana jambo na Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni mara baada ya tukio la uapisho.
Rais John Magufuli amejipambanua kuwa kiongozi mwenye sura mbili; kwanza ya umadhubuti, mchapakazi, mtekelezaji wa ahadi na asiyependa uzembe na ufisadi, lakini pia baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wakimuona kama kiongozi asiyejali utawala bora.
Sura hizo zimemfanya Rais Magufuli ajijengee umaarufu mkubwa kwa wananchi wa kawaida ambao humshangilia kila anapotoa matamko dhidi ya matajiri na watendaji wanaodaiwa kutumia vibaya ofisi zao, lakini baadhi wanasema kuna mambo kadhaa yanayotia doa utawala wake.
Hatua za utawala wa Rais Magufuli zinazowafurahisha wananchi wa kawaida ni za kubana matumizi ya fedha za umma kwa kufuta safari za nje za watumishi zisizo na umuhimu, kuzuia mikutano kufanyika mahotelini, kuhimiza mamlaka husika kukusanya kodi, kupambana na watumishi hewa, kuwasimamisha au kutengua uteuzi wa watendaji aliodai ni wazembe na walioshindwa kwenda na kasi yake pamoja na kuwashughulikia wala rushwa na wahujumu uchumi.
Hata hivyo, baadhi ya wasomi na wanasiasa waliohojiwa jana, wanasema jitihada hizo zinafunikwa na baadhi ya mambo yanayotia doa utawala wake kama vile kauli tata anazotoa katika mikutano ya hadhara, mapambano ya wazi dhidi ya wafanyabiashara, njia anayotumia katika utumbuaji majipu, kuacha kwake kuingilia suala la Zanzibar, na Serikali yake kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.
Sura ya kwanza
Wachambuzi, wasomi na wanasiasa wanakiri kwamba Rais Magufuli amejijengea sifa kutokana na juhudi za ukusanyaji kodi, kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kupambana na ufisadi, uzembe na matumizi mabaya ya mali na fedha za umma. Udhibiti huo umeiwezesha serikali kupata fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Hatua nyingine zilizompa sifa ni utekelezaji wa ahadi yake ya elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari.
Mwenyekiti wa majaji wastaafu, Jaji Thomas Mihayo alisema tangu Rais Magufuli aingie madarakani haoni jambo baya alilofanya huku akitolea mfano jinsi anavyopambana na rushwa na ufisadi na jinsi anavyowachukulia hatua watumishi wanaofanya makossa.
Jaji Mihayo alisema mkuu huyo wa nchi ana kazi ya kubadili mtazamo wa Watanzania kwani ni watu waliozoea kutosikiliza jambo lolote. “Yeye ndiye aliyeibeba CCM maana aliusaka urais bila mbwembwe na hakuwachangisha matajiri na alikuwa sahihi tu,” alisema Jaji Mihayo.
Aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stola alisema Rais amefanya vyema katika ukusanyaji wa kodi jambo ambalo litaifanya Serikali kuwa na fedha ya kutosha ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Bila kujali changamoto zake suala la elimu bure ni zuri maana ada ilikuwa kikwazo kikubwa kwa wazazi. Pia amerejesha dhana ya kila mwananchi kufanya kazi na kurudisha nidhamu ya kazi sambamba na kubana matumizi ili fedha zisizo za lazima zipelekwe katika masuala ya msingi,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na wakili, Jesse James alisema, “Namsifia katika kupambana na ufisadi na kuweka misingi mizuri katika ukusanyaji wa mapato maana nchi ilikuwa imefikia pabaya kwani watendaji wa Serikali walikuwa wakishindana kutafuna mali za umma.”
Kuhusu utumbuaji majipu, Jesse alisema unafanyika bila kufuata sheria na taratibu kwa maelezo kuwa Rais anahukumu watumishi kuwa ni majipu na wezi wakati mamlaka za nidhamu zikiendelea kumchunguza mhusika. “Kwa mtindo huo mamlaka husika haziwezi kutoa ripoti inayoonyesha kuwa mtumishi husika hakuhusika na tuhuma zilizokuwa zikimkabili. Watumishi wa umma kabla ya kuchukuliwa hatua wachunguzwe kwanza, si ile hali ya kuwasimamisha watu kazi katika mikutano ya hadhara,” alisema Jesse.
Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu alisema Rais anaendesha nchi kama Serikali ni mali yake binafsi na akatoa rai kwamba anatakiwa kuongoza nchi kwa kufuata sheria na taratibu. “Kama kuna sheria anaitaka ni vyema akaileta bungeni ili ipitishwe na Bunge na kama kuna ambayo anataka kuibadilisha pia ailete bungeni. Anachokifanya sasa ni kujitungia sheria zake yeye mwenyewe na kuzitekeleza,” alisema Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema.
Aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, David Kafulila alisema Rais ameonyesha dhamira ya kudhibiti uzembe, ufisadi, kufanya kazi kwa mazoea na kutaka masikini waishi maisha mazuri.
Mhadhiri mwingine wa UDSM, Richard Mbunda alisema, “Amerejesha nidhamu kwa watumishi wa umma, amepunguza matumizi yasiyo ya lazima na kujitahidi kutenga fedha za maendeleo katika bajeti yake na kusimamia akitaka zote ziende.”
Sura ya pili
Jambo mojawapo linalochora sura ya pili ya Rais Magufuli ni kauli zake. Desemba 3, 2015 alipokutana na Wafanyabiashara kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) Ikulu ya Dar es Salaam alitoa kauli iliyoonyesha kuwa wafanyabiashara ni watu wa kuepukwa.
“Nilijiepusha na fedha au mchango wowote kutoka kwa wafanyabiashara, kama yupo mfanyabiashara yeyote alinichangia hata shilingi mbili asimame hapa aseme. Nilikwepa kwa sababu nilitaka iwe ‘Hapa Kazi Tu’,” alisema huku akishangiliwa.
Kauli nyingine aliitoa Machi 29 mwaka huu alipohutubia mkutano wa hadhara mjini Chato wakati akiwa kwenye mapumziko ya wiki moja. Kwa mtazamo wa Rais Magufuli wale wanaolipwa mishahara zaidi ya Sh 15 milioni wanaishi kama malaika na wanaolipwa chini ya hapo ni kama shetani.
Alisema katika utawala wake hakuna mtu atakayelipwa zaidi ya Sh 15 milioni; “Kuna watu wanalipwa Sh40 milioni, wanaishi kama malaika, ni lazima tuwashushe waishi kama shetani. Katika utawala wa serikali yangu, sikubali wachache waishi kama malaika.”
Lakini kauli iliyoonyesha udhaifu wa Rais Magufuli kuteua maneno ni aliyoitoa Mei 10 alipokuwa anazungumzia nafasi ya masikini na matajiri katika utawala wake. Alisema, “...Serikali ninayoiongoza, ilichaguliwa na masikini. Kama matajiri walifikiri nitakuwa upande wao basi wamenoa. Mimi nilichaguliwa na masikini na nitawatumikia masikini na si matajiri.”
Kuhusu kauli hizo Stola alisema, “Kauli za Rais na mawaziri wake haziendani na utawala bora. Inakuwaje mfanyakazi anasimamishwa kazi wakati uchunguzi unaendelea huku viongozi wanasikika wakimwita yeye ni jipu? Mtu kama katuhumiwa haina maana kuwa ametenda kosa.
Pia, alisema, “Rais ni wa watu wote si wa masikini au matajiri tu na hawezi kujieleza kuwa yeye ni wa masikini tu. Hata kauli kwamba “…wanaoishi kama malaika nitawashusha waishi kama shetani” si nzuri anapaswa kusimamia sheria na haki; masikini na matajiri wote wanaweza kufanya makosa na hapaswi kuwabagua.”
Utumbuaji majipu
Jambo la pili linalomfanya akosolewe ni utaratibu wa utumbuaji majipu. Mbunda aliungana na wakosoaji akisema utumbuaji majipu wa kiongozi huyo umegubikwa na changamoto nyingi, ikiwamo kutofuatwa kwa sheria na taratibu. “Siungi mkono watumishi wezi na wazembe lakini utumbuaji majipu ufuate sheria na staha. Mambo ya aina hii yapo mengi.”
Kafulila alikosoa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Rais kuwa hazifuati sheria, hasa utumbuaji wa majipu sambamba na sheria nyingine ili kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato, kupunguza matumizi.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema; “Hapa kazi tu! Umemfukuza huyu kazi halafu nini kitaendelea? Keshaondoka kakuacha, unaajiri mwingine? Tunahitaji mtu wa kujibu hayo maswali. Nchi yote sasa inavurugwa. Halmashauri zinavurugwa.”
Katibu mkuu huyo alisema kwa sasa kila kitu kinavurugwa jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa nchi na kwamba inaonekana wazi nchi inaelekea sehemu ambayo mbele kuna giza.
Lissu alisema kasoro ya kwanza ya kiongozi huyo na mawaziri wake ni kujichukulia maamuzi bila kuwepo kwa waraka wa kisheria wa maelezo ya majukumu ya wizara. “Pia, anafukuza watumishi wa Serikali bila kufuata taratibu za kisheria za ajira zao. Pia, uamuzi wake wa kuzuia sukari kutoka nje kuingizwa nchini wakati hajaweka utaratibu wa kuhakikisha nchi inazalisha sukari ya kutosha. Tatizo la uhaba wa sukari hivi sasa yeye hawezi kulikwepa,” alisema Lissu.
Lakini wananchi wa kawaida wanafurahia utaratibu huo wa kusimamishwa au kuondolewa kazini kwa baadhi ya watendaji wakuu wa idara wanaodaiwa kutumia vibaya madaraka yao, utaratibu unaotumika unaitia doa Serikali.
Baadhi ya watendaji kama aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe alitumbuliwa katika mkutano wa hadhara huku mashtaka yakionekana kuandaliwa kisiasa zaidi.
Mapambano na wafanyabiashara
Kauli ya Rais Magufuli anapowazungumzia wafanyabiashara mbalimbali ni ya mapambano.
“Wafanyabiashara hawa walinunua viwanda vya NMC wakafungua mashine na kwenda kuuza Msumbiji na wakisimama utawasikia CCM oyee…Watanzania tunaendeshwa na wafanyabiashara kati ya watano au kumi tu, ukienda kwenye sukari ni haohao, walioua viwanda ni haohao, nawahakikishia nitalala nao mbele hadi mwisho,” alisema.
Hii inatokana na dhana kwamba: “...Serikali ninayoiongoza, ilichaguliwa na masikini. Kama matajiri walifikiri nitakuwa upande wao basi wamenoa. Mimi nilichaguliwa na masikini na nitawatumikia masikini na si matajiri.”
Lakini Desemba 3, 2015 alipokutana nao katika Ikulu ya Dar es Salaam alionyesha kuwa watu muhimu. “Nataka niwahakikishie kama kuna mfanyabiashara yeyote anataka kufanya uwekezaji na akacheleweshwa na mtu yeyote ambaye yupo chini ya mamlaka ya uteuzi wangu, nasema hatabaki kwenye serikali kwa sababu atakuwa anatuchelewesha tunapotaka kwenda,” alisema Dk Magufuli.
Mhadhiri wa UDSM, James alisema, “Ukusanyaji wa mapato unaweka vita kati ya Serikali na wafanyabiashara wakati nchi inategema kodi kutoka kwao wakati hawajawekewa mazingira wezeshi ya biashara. Serikali na hawa watu (wafanyabiashara) wanategemeana hivyo kila mmoja anapaswa kutomkomoa mwenzake.”
Mwanasheria huyo pia aligusia suala la uhaba wa sukari nchini kwamba linaweza kuwa limesababishwa na Rais kutokana na kuzuia uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi bila kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo nchini.
2 comments:
Blah blah blah! Kabla hata uchunguzi mdogo wa ndani ya chama cha mapinduzi kuna kundi la watu tayari lilishakuwa lina muhofu Magufuli kutokana na msimamo wake wa kutoendekeza upuuzi wa kitanzania wa maneno mengi,ulaghai na kuendekeza rushwa,kuwaachia wafanya biashara kufanya wanalotaka ikiwemo kuwahonga baadhi ya watumishi wa umma kama si wote kuhujumu uchumi wa nchi kama vile kutolipa kodi na kujipatia maeneo muhimu ya nchi ya biashara kama vile viwanja na maeneo makubwa ya ardhi kwa njia za ubadhirifu. Kwa kiasi kikubwa Tanzania ilishafika mahali pabaya au kama ilivyokuwa inajulikana kwa jina la shamba la bibi kila mtu anajichukulia chake kwa nguvu zake za rushwa na madaraka bila ya kufuata taratibu za kisheria. Tanzania ilikuwa ni miongini mwa vinara wa rushwa na ubadhirifu duniani aidha kwa tabia ya mtanzania mmoja mmoja shirika au watumishi wa umma. Kwa hakika bila ya kumun'gunya maneno hata hao wanaojiita wasomi wanaomkosoa Magufuli katika mapambano yake dhidi ya ufisadi ni wasomi zalio lilotokana na corrupted system na mara nyingi hutumumiwa na aidha corrupted business people au politicians kumpiga vita Magufuli. Hakuna binaadamu au kiongozi aliemkamilifu hata hao viongozi waasisi wa mataifa makubwa tunayokimbilia kuwashitaki viongozi wetu kwa kutofuata utawala bora walifanya mambo ya ajabu na ya kishenzi kabisa kuzidumaza nchi zetu ikiwemo slavery . Hakuna kibaya anachokifanya Magufuli mpaka sasa isipokuwa anatakiwa kuwa mkatili zaidi katika utumbuaji wa majipu. Hakuna pande mbili wala tatu za Magufuli kilichokuwepo ni fitna za wapinzani kujaribu kumrejesha nyuma Magufuli katika kupambana na uozo uliokisiri ulioenea katika kila sekta ya maisha ya mtanzania. Maghufuli yupo vitani lakini watanzania tuliowengi tunaoitakia mema Tanzania tunamuhakikishia kuwa tutakuwa nyuma yake mpaka dakika ya mwisho,mpaka kieleweke tulishajua haitakuwa vita rahisi ni vita itakayojaa kila aina ya vitimbi na hujuma lakini tayari tumeshajiandaa kukabiliana na kila hila. Na tunawahakikishia wale wote wanaompiga vita Magufuli wajue kabisa yakuwa hivi vita ni endelevu sio vya mpito kati ya haki na batili tunajua kabisa Magufuli anapigania haki kwa watanzania waliowengi na wanaompinga tunajua kabisa yakuwa wanapigania kumkumbatia ufisadi na yale maovu yote yaliofanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi masikini na fukara duniani ilihali nchi yetu ikiwa imejaliwa rasimali za kila aina kama vijana wa kutosha wa kufanya kazi lakini kazi hakuna,madini,milango mikuu ya bahari yaani bandari kwa nchi zisizokuwa na bahari yaani ni vitega uchumi vya uhakika lakini wachache greed tanzanians ndio wanaojinufaisha,hakuna nchi duniani inayoweza kujiendesha bila yakuwa na misingi imara ya kudhibiti kodi zake na ndio maana hata kwenye maandiko yote ya dini kodi imeorodheshwa lakini kwetu sisi ni tofauti kabisa watu wanatafuta kila aina ya njia ya kukwepa kulipa kodi kwa kushirikiana na watumishi wa umma wasio waaminifu leo taratibu zinachukuliwa kudhibiti vitendo hivyo viovu watu wanaleta siasa za kipuuzi. La kushangaza watu na wanasiasa wa hovyo wanalifanya suala la sukari kuwa big deal wenzetu wanatushangaa. Sukari sio chakula zaidi ni matatizo katika afya ya mwanadamu kwanini liwe big deal kuliko ukosekenaji wa maji safi hasa vijijini? Hapo utaona kuna watu wanasubiri Magufuli ajikwae kidogo tu ili wa make big issue out of it.Ni watu wasioitakia mema Tanzania aidha kwa manufaa yao binafsi ya kisiasa,biashara,ufisadi au chuki za mtu binafsi lakini mwisho wa siku tunajua Tanzania ,Maghufuli na watanzania waliowengi watashinda hii vita.
Big up!!! Give me 5!!! mtoa maoni wa kwanza!! Kama ulikuwa kwenye kichwa changu na comments zako! Baba yetu mpendwa , Rais wetu wa kweli kaza uzi baba, hizi blaa blaaa za wanasiasa achana nazo kabisa zisikukoseshe usingizi! Tumbua majipu mpaka mwisho tuko nyuma yako sisi wananchi tulio Wazalendo Kama wewe! Tunazidi kukesha tukiendelea kukuombea kwa Mwenyezi Mungu. " MUNGU MMBARIKI RAIS WETU,MUNGU IBARIKI TANZANIA!
Post a Comment